25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Gavana asubiri amri ya Mahakama kutaja waliochota mabilioni Escrow

Elizabeth Hombo -Dar Es Salaam

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florence Luoga, amesema endapo Mahakama itamruhusu kutoa orordha ya watu waliopokea fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, atafanya hivyo.

Profesa Luoga ametoa kauli hiyo ikiwa imepita wiki chache tangu James Rugemalira anayeshtakiwa kwa uhujumu uchumi, kudai mahakamani kwamba amemuandikia barua Gavana huyo akimtaka atoe orodha ya waliopewa fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo na kwamba yeye hakupata hata senti moja.

“Fedha nilizolipwa na PAP ni kutokana na amri ya mahakama, naomba Gavana aorodheshe majina ya wote waliopewa fedha kutoka katika akaunti ya Escrow ili mimi niwe msafi,”alidai Rugemalira akiwa mahakamani.

Akijibu swali la mwandishi wa habari hii kwenye mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Luoga alisema taratibu za kibenki haziruhusu wao kutoa taarifa za mteja bila ruhusa yake.

“Taratibu za kibenki haziruhusu sisi BoT kutoa taarifa za mteja bila ruhusa yake na hilo suala liko mahakamani pia zile fedha sio za BoT, sasa mimi sivunjishi siri za wateja na ukweli kuhusu suala hilo utajulikana mahakamani.

“Mimi nitafanya hivyo endapo mteja ataniruhusu kufanya hivyo au mahakama ndio nitatoa orodha hiyo,”alisema Profesa Luoga.

Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd na mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Harbinder Singh Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Pan Africa Power Solution Tanzania Limited (PAP), wanadaiwa kutenda makosa ya uhujumu uchumi katika Jiji la Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.     

Washtakiwa wanadaiwa kati ya Oktoba 18 ,2011 na Machi 19, 2014 katika Jiji Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa mwingine, Mwanasheria wa kampuni ya  kufua umeme ya IPTL, Joseph Makandege, anakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 980,000.

Kampuni ya VIP Engineering inayomilikiwa na Rugemalira na Kampuni ya Mechmar walikuwa wabia walioanzisha biashara kupitia kampuni ya IPTL.  Mradi huo wa kufua umeme ulianza mwaka 1994, ukawa na mgogoro mkubwa, ukachelewa kuanza hadi mwaka 2000.

Mwaka 2006 waliingia kwenye mgogoro mwingine Tanesco wakalamika kutozwa capacity charge, hivyo wakafungua kesi kwenye mahakama ya kimataifa ya usuluhishi.

Kutokana na mgogoro huo, akaunti maalum ya Tegeta Escrow ilifunguliwa BoT ili Tanesco waendelee kuweka fedha wakati shauri hilo likiwa bado mahakamani.

Baadaye mahakama iliridhika kwamba Tanesco ilikuwa inatozwa fedha nyingi hivyo wakae wapige upya hesabu ijulikane ni kiasi gani IPTL ilipaswa kulipwa na kiasi gani kilizidi, jambo ambalo halikufanyika na badalala yake fedha zikatolewa na kupewa PAP ambayo ilidai kuinunua IPTL.

Mwaka 2014 jambo hilo liliingia bungeni ambapo lilisababisha kuondolewa madarakani kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi.

Pia aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliwajibishwa kwa kashfa hiyo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,522FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles