25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 7, 2024

Contact us: [email protected]

FAMILIA YA LISSU YAMJIBU IGP SIRRO          

Johanes Respichius na Asha Bani


WAKATI Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, akiendelea na matibabu yake katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, familia yake imecharuka kwa kuwajibu viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwamo Mkuu wa Polisi, IGP Simon Sirro na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, familia ya mwanasheria huyo, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ilionyesha kushangazwa na kauli za viongozi hao, huku wakitaka ndugu yao asifanywe kama mpira wa kona.

Kaka mkubwa wa Lissu, Alute Mughwa na mdogo wake, Vincent, walishangazwa pia kwa kitendo cha kuona mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo na badala yake wanadai kumsubiri dereva wa Mbunge huyo, Simon  Bakari,  ambaye naye yupo Nairobi kwa matibabu ya kisaikolojia.

Walishangaa pia polisi kushindwa kumhoji dereva huyo akiwa Nairobi, ambapo Tanzania ina ubalozi, ama kumhakikishia usalama wake ili aje kuhojiwa sehemu salama na siyo mahabusu kama mhalifu.

Dereva wa Lissu

Akizungumzia kauli ya Sirro kuhusu dereva wa Lissu, Mughwa alisema: “Nimeona kwenye magazeti ya leo yakimnukuu IGP Simon Sirro akizungumzia habari za dereva wa Lissu  aliyeko Nairobi nchini Kenya kwamba arudi nchini ili aje ahojiwe … Ushauri wa familia ni kwamba kwanini Polisi msifuate kule Nairobi?

“Na kama hao watu walivyofyatua risasi zingewapata wote wakafa, je, polisi wasingefanya uchunguzi wao? Na kama ambavyo tunaambiwa hao wahalifu hawajakamatwa, si maisha yake (dereva) yatakuwa hatarini?

“Kuna utaratibu wowote juu ya kuhakikisha usalama wake? Isije ikawa anavuka pale Namanga tukasikia kakatishwa pale njia, kwahiyo kama watahitaji kwenda kumchukua busara inaelekeza kwamba anapaswa kuhifadhiwa.

“Anapaswa kuhakikishiwa usalama wake kwanza, ndiyo aletwe huku kwa mahojiano na si kumweka mahabusu kwasababu yeye ni shahidi tu,” alisema Mughwa.

Alisema familia haina masilahi yoyote tofauti na kuhakikisha Lissu anapata tiba na waovu waliotaka kumuua wanakamatwa na kupelekwa kwenye mikono ya sheria.

“Hatuko tayari kuona suala hili linafanywa siasa, haifai Lissu kumfanya mpira wa kona,” alisema Mughwa.

Naye Vincent akimzungumzia dereva huyo, alisema: “Dereva wa Tundu ni kama mtoto wake kwasababu alianza kufanya naye kazi akiwa mdogo, kwahiyo amekulia pale kwa miaka 25, kwahiyo ni mtoto wake, anakula na kulala kwake, sasa mambo haya yametokea ameathiriwa.

“Na Sirro kusema anasubiri mtu mmoja zoezi limesimama au labda zoezi linaendelea, lakini sisi kama familia tunaona hakuna umakini kwasababu mtu alitaka kuuawa, mtu mwenye mchango mkubwa nchini hata kama ni upande wa pili jambo hili haliendi kama inavyotakiwa, ndiyo maana tunashauri washirikishwe watu kutoka nje.”

Afya ya Lissu

Akizungumzia hali ya Mbunge huyo, Alute alisema mbunge huyo anaendelea vizuri na afya yake inazidi kuimarika.

“Amefanyiwa upasuaji mara kadhaa na ameanza kula kwa njia ya kawaida, pia anazungumza vizuri.

“Ndugu yetu ambaye amekwenda kule (Nairobi) kwa mara ya mwisho ametuletea salamu kwamba yupo sawa sawa na jana (juzi) tulizungumza na mke wake.

“Septemba 9 nilipokwenda Nairobi tulifanya kikao cha wanafamilia, Uongozi wa Chadema, Uongozi wa TLS kwamba atakayekuwa anatoa taarifa za maendeleo ni Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe) pekee,” alisema Mughwa.

“Nilikuja Dar es Salaam tangu siku ya Jumapili kwa shughuli zinazomhusu Tundu Lissu, siku ya Jumatatu tulifanya kikao cha faragha, mazungumzo yalikuwa mazuri na baadaye tukakubaliana tukiahirishe ili tuweze kufanya mashauriano yanayopaswa kwa upande wetu sisi (familia) na vilevile kwa upande wa Chadema, ambao tumekuwa nao toka mwanzo jambo hili lilipotokea mpaka sasa hivi, tunapenda vilevile tumalize nao,” alisema Mughwa.

Uchunguzi wa tukio

Akizungumzia uchunguzi wa tukio la Lissu kupigwa risasi Septemba 7 nyumbani kwake Dodoma, Mughwa alisema familia imeshaandika barua serikalini kuomba uchunguzi wa tukio hilo ufanywe kwa kina, haraka na kitaalamu.

“Hawa waovu waweze kujulikana, kukamatwa na kupelekwa kwenye mikono ya sheria, suala hilo tumelifuatilia jana (juzi) kwa Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, na leo (jana) tumetoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufuatilia barua yetu imefikia wapi na tumearifiwa kuwa inashugulikiwa na tayari ameshaijibu barua tuliyoiandika na ameituma Arusha,” alisema Mughwa.

Alisema ili waweze kufanikiwa, hawawezi kuipuuza Serikali, hivyo ni lazima waende nayo mpaka hapo watakapoona njia hiyo imefungwa.

“Tunataka jambo hilo lishughulikiwe bila kuingiza siasa na kama itakuja ije wakati Tundu anatembea barabarani na si wakati huu.

“Katika barua yetu tulipendekeza kwamba, katika mazingira ya shauri hili, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inapaswa kushirikisha wataalamu wa uchunguzi kutoka nje ili kila upande uweze kuridhika.

“Kuna vyombo vya habari viliripoti habari ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwiguli Nchemba, sijui kama ilikuwa sawa sawa au la! Kwamba alisema Tanzania ni nchi huru, inajitegemea na ina vyombo vyote vya kufanya uchunguzi, hivyo haioni sababu ya kuhitajika vingine kutoka nje.

“Kwa mujibu wa sheria ya Ushirikiano wa Mambo ya Jinai, ni kweli Tanzania ni huru, lakini ni mwanachama wa Jumuiya ya Kimataifa, kwahiyo tunashirikiana kwa mambo mbalimbali ili tuweze kuimarisha uhuru na maendeleo yetu.”

Alisema mwaka 1984 jengo la Benki Kuu (BoT) liliungua na Polisi katika kutafuta chanzo cha moto waliwatafuta wataalamu  kutoka nje wakafanya uchunguzi na wahusika wakapatikana.

“Mbali na hilo, mwaka 1998 Ofisi za Ubalozi wa Marekani hapa Dar es Salaam zilipigwa mabomu na magaidi, Serikali yetu ilichukua wapelelezi kutoka Marekani, FBI walikuja kufanya upelelezi na wahalifu walipatikana na wakashtakiwa na sasa hivi wapo jela.

“Kwa hiyo tunachokitaka sisi katika suala hili la ndugu yetu  si kitu kigeni na ndiyo maana tunaiomba Serikali iweze kuruhusu na  ieleweke kuwa katika hili hatufanyi siasa hata kidogo, tunataka twende na Serikali  katika jambo hili na kama ni siasa itasubiri Lissu akipona na kurudi katika majukumu yake,” alisema.

Kwa upande wa mdogo wa Mbunge huyo, Vicent Mughwa, alisema inatia wasiwasi kwa kuona unakaribia mwezi mmoja ikiwa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo la kushambuliwa kwa kaka yake.

“Isitoshe Agosti, Lissu alifanya mkutano na waandishi wa habari na kusema kuna watu wanamfuatilia, alimwambia IGP na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa kwamba awaambie vijana wake waache kumfuatilia,” alisema Mughwa.

Alisema Lissu kazi anayoifanya ni ya siasa, na kazi ya wabunge wa upinzani ni kufukua mambo ambayo yanakwenda vibaya dhidi ya utawala ili yarekebishwe.

Alisema upinzani kwenye siasa zake ukifanikiwa pia unaweza kuchukua dola, jambo ambalo si kosa, ndiyo maana wabunge wanalipwa mshahara kwa shughuli hiyo.

Alisema kwenye mkutano wa Lissu na waandishi wa habari, alitaja gari na namba zake na kusema linamfuatilia, lakini anashangaa kusikia hakuna mtu yeyote aliyekamatwa na kwamba hilo gari halijawahi kufika Dar es Salaam, “kumbe mnajua ni la nani?”

“Pia tunaambiwa kuwa alikuwa anaishi sehemu ambayo ina ulinzi wa kutosha, hivyo inashangaza walinzi wote walikuwa wapi?”

CHADEMA NAO

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje, John Mrema, alisema wanamshangaa Sirro, lakini wanamtaka pia awatafute wataalamu wa saikolojia wamweleze mwenye matatizo hayo anakuwaje.

“Eti anang’aa katika picha, IGP Sirro anafikiri mgonjwa wa saikolojia anatakiwa aweje na kama alikuwa haelewi anavyokuwa si bora angewauliza wataalamu wa saikolojia  wamweleweshe kwanza.

“Anatushangaza kusema kuwa anapiga picha, sasa sijui hakutakiwa kuona sura yake, ni kweli dereva wa Lissu yupo hospitali anatibiwa kutokana na tatizo la kisaikolojia, wamsubiri apone kwanza,” alisema Mrema.

“Sisi hatumzuii, akipona atakwenda kutoa maelezo yake endapo pia ataruhusiwa na madaktari wanaomwangalia na atasema nini ambacho anakifahamu.”

 

Kauli ya Sirro

Akiwa mkoani Mtwara juzi, Sirro alisema: “Tunamhitaji sana yule kijana (dereva) ambaye yuko Nairobi, ambaye wanasema amepata tatizo la kisaikolojia, lakini ukimuona yule kijana kwenye picha anazoweka kwenye mitandao anawaka tu na yuko vizuri, tulisikia anakuja, lakini bado hajaja na tunamsubiri ili aweze kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi nchini,” alisema.

Alisema upelelezi wa tukio la Lissu bado unaendelea, lakini bado yapo maswali mengi ambayo dereva huyo angeweza kuyajibu ili kukamilisha upelelezi.

IGP Sirro alisema hadi sasa watu wanaotuhumiwa kwenye tukio hilo wamekwisha kukamatwa na kuhojiwa sambamba na magari yanayohisiwa kuwa yalitumika katika tukio hilo bado yamo mikononi mwa Polisi.

“Lissu hana tofauti na Watanzania wengine, pia ana haki kama wengine, nina kesi nyingi nchini si ya Lissu tu, mimi nawahudumia Watanzania wote, kwanini Lissu? Hatuwezi kuchukulia kesi ya Lissu kupigwa risasi kama iko peke yake, ni vema mkasubiri uchunguzi ukamilike,” alisema.

Pamoja na tukio hilo kutikisa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, vyombo vya dola havijaeleza hatima ya wahusika wa tukio hilo, ambalo Chadema wanavituhumu vyombo vya dola kuhusika nalo, hivyo kutaka lichunguzwe na watu kutoka nje ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles