28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

EWURA yatoa angalizo kwa watumiaji wa Gesi majumbani

Na Sheila Katikula, Mwanza

Kufuatia kuongezeka kwa matukio ya moto kwenye maeneo tofauti nchini Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewashauri watumiaji wa mitungi ya gesi ya kupikia kuikagua mara kwa mara ili kubaini endapo gesi inavuja na kuchukua tahadhari ya kuzuia ajali ya moto.

Ushauri huo umetolewa leo Julai 29, 2021 na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina wakati wa mahojiano Maalum na Mtanzania Digital ofisini kwake ambapo amesema kuwa kusisitiza tahadhari hiyo inapaswa kuzingatiwa kwani kwa sasa kuna idadi kubwa ya watumiaji wa niashati ya gesi kufuatia elimu inayotolewa kuachana na matumzi ya kuni na mkaa.

Mhina amesema endapo mtumiaji wa mtungi wa gesi atahisi gesi inavuja ni vyema akachukua tahadhari ya mapema kwa kufungua madirisha ili kuruhusu hewa kutoka nje iingie, kuzima taa, feni, friji (jokofu) na baada ya hapo kutoa mtungi wa gesi nje ya nyumba kwa ajili ya uchunguzi zaidi ama marekebisho.

Ameongeza kuwa, ikitokea kwa bahati mbaya ajali ya moto uliotokana na gesi kulipuka basi wananchi watumie kifaa maalum cha kuzimia moto (fire extinguisher) ingawa katika maisha ya kawaida si rahisi kuwa nayo hivyo wanashauriwa kutumia mchanga kuzima moto huo badala ya maji kama ilivyozoeleka.

“Tunakataza watu wasitumie maji kwa sababu maji muundo (composition) wake una oksijeni ambayo ni chakula cha moto, ndio maana inapotokea hata gari imelipuka unaambiwa kama una blanketi funika ili kuondoa oksijeni, kwa hiyo tunasisitiza watu watumie mchanga zaidi endapo itatokea moto umeanza kuwaka kuliko kutumia maji,”alisema Mhina.

Pia amebainisha kuwa ni vema wananchi wachukue tahadhari kwa kuhakikisha usafirishaji wa gesi ni mzuri, mtungi hauvuji, mahali pa kuhifadhia gesi ni salama na kuweka mbali na vyanzo vingine vya moto au hakuna shughuli za uchomoleaji au za moto angalau kwa umbali kidogo.

“Na wanaponunua gesi wahakikishe mtungi hauna mvujo na kizibo chake kiwe kimeziba vizuri, na njia rahisi ya kujua kama mtungi unavuja au hauvuji wanaweza kuchukua povu la sabuni wakamwagia kwenye mtungi wao na kuweza kubaini.

“Mtungi wa gesi unatakiwa usafirishwe ukiwa wima ingawa kwa Watanzania usafirishaji wake ni mgumu na ukifika nyumbani kama umesafiri kwa umbali kidogo hakikisha una upumzisha mtungi hata dakika tano kabla ujaanza kuutumia,”amesema Mhina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,307FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles