22.7 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

Sengerema yapata baraza la ardhi, Mbunge Tabasamu asaidia vifaa

Na Clara matimo, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amewaapisha wajumbe wanne wa Baraza jipya la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Sengerema ambalo litapunguza mlundikano wa kesi za migogoro ya ardhi zilizokuwa zinapelekwa mkoani Geita, huku Mbunge wa Jimbo la Sengerema Hamis Mwagao ‘Tabasamu’ akitoa msaada wa samani za ofisi hiyo na kuikarabati.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel akimuapisha Mjumbe wa Baraza la ardhi na nyumba wilaya ya Sengerema, Martha Kanizyo, ofisini kwake leo . Picha na Clara Matimo.

Wajumbe hao wameapishwa leo Julai 28, katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambaye amewataka kufanya kazi kwa weledi kuepuka vishawishi vya rushwa, kwani kuna watu ambao watajaribu kuwarubuni ili kupindisha haki, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanakuwa faraja na siyo kukuza mgogoro na kuchelewesha upatikanaji wa haki.

“Watumishi wote wa mabaraza ya ardhi na nyumba  ya wilaya mnapaswa kutimiza majukumu yenu kwa weledi na kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo na itakayokuwa inatolewa ili kuboresha utoaji wa huduma ya utatuzi wa migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi na kuhakikisha kwamba mashauri yanasikilizwa na kuisha katika kipindi kisichozidi miaka miwili tangu shauri kufunguliwa katika baraza,” amesisitiza Mhandisi Gabriel.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Gabriel amempongeza Mbunge Tabasamu kwa kujitolea kukarabati na kuliwekea samani za ofisi jengo litakalotumiwa na baraza, kwani sasa wananchi wa Sengerema watapata huduma karibu zaidi kuliko awali walipokuwa wanalazimika kwenda mkoani Geita.

Vilevile, ametoa rai kwa halmashauri zote za mkoa huo kuhuisha mabaraza ya ardhi ya kata na vijiji yaliyomaliza muda wake na kutoa elimu kwa wajumbe wa mabaraza hayo ili wajue majukumu yao pia zitenge bajeti kwa ajili ya kuwawezesha washauri kupata vitendea kazi.

 Kwa upande wake, Mbunge Hamis Mwagao Tabasamu amesema hatua hiyo ni sehemu ya ahadi yake kwa wananchi wakati wa kampeni aliwaahidi kufanikisha uwepo wa mahakama ya ardhi na baraza la ardhi kabla ya mwaka 2022 kufuatia malalamiko ya wananchi ambao husafiri takribani Km 100 hadi Geita kutafuta huduma hiyo, huku  wakazi wa Buchosa, Maisome, Kaunda na Sengerema wakisafiri kwa umbali wa Km 160.

“Watu wa baraza la ardhi walilalamika kwa msajili wa baraza la ardhi na nyumba Kanda ya Ziwa wakasema bajeti hakuna, nikasema nitatafuta ofisi nilishirikiana na DAS tukaomba ofisi ya kata ya Nyambulukana tumeifanyia marekebisho na tunatarajia kuanzia Jumatatu ijayo itaanza kutoa huduma,” amefafanua.

Tabasamu amesema Mwenyekiti wa baraza la ardhi la Geita alimshauri afanye juhudi ili wilaya ya Sengerema ipate baraza lake kutokana na ofisi hiyo kuwa na mashauri 92 kutoka wilaya ya Sengerema, hivyo uanzishwaji wa baraza hilo ni faraja kubwa kwa wananchi wa jimbo lake.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga, amesema kuwa asilimia 85 hadi 90 ya wananchi wilayani humo wanaofika ofisini kwake wanalalamikia migogoro ya ardhi, huku akisisitiza kuwa uuhishwaji wa mabaraza ya ardhi ni chachu kwa wananchi.

Mmoja wa wajumbe waliokula kiapo leo, Yohana Kasenga amesema baraza hilo litafanya kazi kwa bidii kubwa ili kutatua changamoto za ardhi zinazoikabili wilaya hiyo, huku akibainisha kuwa watakaa na mwenyekiti wa baraza ili kuweka mipango mizuri ya kuwahudumia Wana Sengerema. Wajumbe waliokula kiapo ni Yohana Kasenga, Yohana Hamisi, Rose Gasanzwe na Martha Kanizyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,283FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles