Emery: Ozil hastahili kuwa Arsenal

0
890

LONDON, ENGLAND

BAADA ya timu ya Arsenal kufanikiwa kushinda mabao 4-0, juzi dhidi ya Standard Liege kwenye michuano ya Kombe la Europa, kocha wa timu hiyo Unai Emery, ameweka wazi kuwa kiungo wake Mesut Ozil hastahili kuwa kwenye kikosi chake.

Kauli hiyo ameitoa mara baada ya safu yake ya kiungo kuwa bora kwenye mchezo huo ambapo Ozil alikuwa nje ya uwanja, hivyo kuamini kuwa wachezaji hao walikuwa na kiwango kizuri tofauti na mchezaji huyo katika michezo aliyowahi kucheza.

Mbali na Ozil kuwa mchezaji anayelipwa fedha nyingi ndani ya kikosi hicho, lakini anasugua benchi kwenye michezo mbalimbali tangu msimu huu umeanza na anatajwa kutakiwa kutolewa kwa mkopo.

Emery amesisitiza kuwa, wachezaji ambao aliwapanga kwenye mchezo wa juzi wanastahili kuwa kwenye kikosi chake.

“Nadhani kila siku nimekuwa nikichagua wachezaji ambao wanastahili kucheza kwenye mchezo husika kutokana na uwezo wao ambao unaweza kuisaidia timu, ukiona wachezaji nawaacha nje ujue hawastahili kuwa hapo.

“Lakini wanaweza kufaa kwenye mchezo mwingine, ila kwa wachezaji ambao hawapati nafasi kabisa basi watakuwa hawafai kuwa kwenye kikosi hicho,” alisema kocha huyo.

Ozil ni mmoja kati ya wachezaji ambao wamekuwa benchi kwenye michezo mingi msimu huu, hivyo kauli ya kocha huyo inamaana hafai kwenye kikosi chake.

Mchezaji ambaye anapewa nafasi kubwa sasa ndani ya kikosi hicho kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Ozil ni Gabriel Martinelli mwenye umri wa miaka 18, raia wa nchini Brazil. Kwenye mchezo huo wa juzi alipachika mabao mawili peke yake.

Hata hivyo kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya Nottingham Forest katika michuano ya Kombe la Carabao alifanikiwa kupachika mabao mawili huku Arsenal ikishinda mabao 5-0.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here