22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Slaa: Sina barua ya msajili

Dk. Wilbrod Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa

NA ELIZABETH HOMBO

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema hajawahi kupokea barua yoyote kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, inayowataka waitishe mkutano wa Kamati Kuu ili kufanya marekebisho ya Katiba yao.

Wakati Dk. Slaa anatoa kauli hiyo, Julai, mwaka huu, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho, John Mnyika, alizungumza na vyombo vya habari kuwa Agosti, 2006 walifanya marekebisho makubwa ya Katiba ikiwamo kifungu kilichokuwa kinaweka ukomo wa uongozi.

Juzi, Jaji Mutungi akizungumza na gazeti hili, alieleza kuwa kinachotokea sasa ndani ya chama hicho ni matokeo ya kupuuzwa ushauri wake wa kukitaka kifanye marekebisho ya Katiba yake.

Kauli za viongozi hao zilitokana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuwekewa pingamizi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk, ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya uenyekiti taifa, akidai chama chake kimekiuka Katiba na maagizo ya msajili.

Barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema ya Januari 15, mwaka huu, ilitaka chama hicho kuitisha mkutano rasmi na halali kwa mujibu wa Katiba yao.

“Chama chenu kiitishe mkutano (forum) rasmi na halali kwa mujibu wa Katiba yenu, kisha mlifanyie upya tafakari stahiki suala linalohusu marekebisho ya ibara 6.3.2(c) kwa kuzingatia taratibu na hatua zinazopaswa ili kuwezesha kuwasilishwa kwa ibara hiyo katika Mkutano Mkuu, kwa lengo la kupitishwa rasmi na mkutano huo ambao ndio wenye mamlaka halali kwa mujibu wa Katiba ya chama chenu, ili kuwezesha kutumika kihalali,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Jana, Dk. Slaa alisema hakuna barua yoyote ndani ya ofisi yake ambayo imetoka kwa msajili huyo.

“Sijawahi kupokea barua ya Jaji Mutungi na wala hakuna barua ya aina hiyo ofisini kwake inayoitaka ofisi yangu kuitisha mkutano wa Kamati Kuu ili kufanya marekebisho ya Katiba ya chama,” alisema Dk. Slaa.

Akizungumzia rufaa ya Mbarouk, Dk. Slaa alieleza kushangazwa kwa kitendo cha kupelekwa kwenye magazeti badala ya kufika kwanza ofisini kwake.

“Kwanza siwezi kuzungumzia rufaa ya Mbarouk kwa sababu kuna taratibu zake… lakini kilichonishangaza ni kitendo cha rufaa kupitia kwanza kwenye magazeti badala ya kuletwa kwanza ofisini,” alisema.

Alipotakiwa kuzungumzia kauli ya msajili kuwa walipuuza ushauri wake, alisema hata habari iliyokuwa imeandikwa haikuwa ya kweli bali jaji huyo alilishwa maneno ambayo hayakusema.

“Bora hata umejileta mwenyewe… nimetoka kuzungumza na Jaji Mutungi amesema maneno yaliyoandikwa katika gazeti lenu hayakuwa yake kabisa.

“Ninajua kwanini mnayaandika na malengo yenu nayajua sasa kama mnafanya propaganda tumieni akili.

“Sasa kaandike hivyo hivyo na usipoandika hayo niliyokueleza ni wazi gazeti lenu litakuwa na nia mbaya na Chadema… ukiwa na swali jingine wewe niulize tu,” alisema Dk. Slaa.

Mwandishi wa gazeti hili alipomtafuta Jaji Mutungi ili kujua kama ni kweli amemweleza Dk. Slaa kuwa hakuyasema maneno hayo, alisema hawezi kuzungumza kwenye simu na badala yake atafutwe leo.

- Advertisement -

Related Articles

3 COMMENTS

  1. Wadau wa siasa za mfumo wa vyama vingi hatushangai yanayoendele katika ofisi ya msajili kupitia kivuli cha Msajili wa vyama vya siasa. Jina hili ‘MSAJILI’ halistahili kutumika hapa badala yake litumike ‘KIRANJA WA KUSIMAMIA VYAMA VYA SIASA’. Ninasema hivi kwa sababu takribani WASAJLi wote waliopitia ofisi hiyo ya msajili wamekuwa makada wa CCM wanaofanya kazi kwa hulka ya UCCM. Yaani wanafika mahala wanahamu kuhasi taaluma na weledi wao kwa maslahi ya chama kimoja. Lakini msajili mpya ndugu Mtungi anahitaji kujua ukweli kuwa ‘Mfumo wa Chama Kimoja’ ni mfu ambaye hatafufuka tena. Hivyo, ni wakati wake wa sasa kuhakikisha anasajili vyama na siyo kusimamia vyama hivyo maana mfumo wa vyama vingi unasimamiwa na sheria ya mwaka 1992 na anayevunja sheria hiyo anapaswa kupelekwa mahakamani siyo malumbano kwenye magazeti.

  2. Sasa ninaamini Chadema nimpango wa Mungu jinsi kinavyopigwa vita na maadui mbali mbali. Yesu alipigwa vita kubwa sana maadui walipoishiwa minu basi waliamua kumtumia mmoja wa mfuasi wake “Yuda iskarioti”. Ni sawa na chani ya chadema, CCM imejaribu kila mbinu ,imeshindwa na sasa imeamua kutumia hata wanaChadema ili kuibomoa, lakini nadhani inavyoonekana hiki chama kina nguvu za Mungu. Hivi ni wazi mbinu chafu hata kutoka ofisi za msajili hazitafanikiwa Mtume paulo anasema” Kama Mungu yuo upande wetu nani ataweza kuwa mpinzani wetu?” CCM oneni jinsi mlivyoshindwa kuwaletea watanzania katiba mpya pamoja na kiburi chote hiki, sasa yametimia” Hakuna katiba mpya”. Sasa ni wakati kwa Watanzania kuungana na kuachana na CCMambayo haina uwezo wa kuleta katiba mpya, imeonyesha wazi sasa wala hakuna ubishi. Hawawezi kuleta katiba mya ya Watanzania, bali katiba ya mabavu ya CCM, ambayo haitakiwi. Poleni sana CCM, hongereni Ukawa kwa kutetea maoni ya wananch chini ya Tume ya warioba.

  3. Sasa baada ya rais kuwa amebaini katiba bora ya wananchi ni vigimu kupatikana kwa mtindo unaoendelea wa bunge letu la katiba,anapaswa awabaini viongozi wale wote walio karibu naye ambao ndio walikuwa wakimshauri vibaya na kuwaweka kando.Rais anatakiwa ajue sasa kuwa hao hawakuwa nae katika wazo lake zuri la kuwa na katiba inayoendana na wakati tulionao.Hao walikuwa na lao jambo la mifukoni tu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles