25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango aongoza waombolezaji kuaga mwili wa Hayati Ali Hassan Mwinyi

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, amewaongoza waombolezaji katika kutoa heshima za mwisho wakati wa kuaga mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Ali Hassan Mwinyi kwenye Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salam.

Akitoa salamu za pole leo Machi 1,2025 kwa waombolezaji, Dk. Mpango amesema Hayati Mwinyi atakumbukwa kwa kuwa kisima cha hekima, chemchem ya elimu na shule ya uzalendo, uadilifu na uongozi.

Amesema Hayati Mwinyi alijitoa kwa dhati kulitumikia Taifa kwa moyo wake wote na kutoa mchango mkubwa kwa nafasi zote alizoshika katika utumishi wa umma.

“Hayati Ali Hassan Mwinyi amekuwa kielelezo cha kutetea na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, alikuwa na karama kubwa ya uongozi na alizingatia kwa dhati masharti ya uongozi ikiwemo uwajibikaji pamoja na kutoa mchango mkubwa katika kukuza matumizi ya lugha ya kiswahili na kuifanya kutambulika na kutumika kimataifa,”amesema Dk.Mpango.

Ameongeza kuwa Hayati Mwinyi aliasisi mageuzi ya kiuchumi na kisiasa hapa nchini, alijijengea sifa kubwa katika kuhamasisha kilimo bora pamoja na kuwa na bidii katika kumwabudu Mwenyezi Mungu.

Naya Rais wa Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete amesema Hayati Mzee Mwinyi akiwa Rais alivunja baraza la mawaziri mara mbili.

“Nawashukuru kwa miaka yote tumekuwa pamoja ila wenzangu naomba mwende mkajiuzulu alivyosema hivyo akaondoka tukawa tunajiuliza unakwenda je? Kuandika barua baada ya mda ikaja taarifa msiandike barua ikaja barua tuondoke ofisini twende nyumbani, “amesema Dk. Kikwete.

Ameeleza kuwa kwa mara ya pili haikuwa kama mwanzo waliona kwenye vyombo vya habari amevunja baraza la mawaziri alikuwa jasiri.

“Mzee Mwinyi alikuwa hajikwezi alikuwa mtu mwenye mapenzi na watu wote aliishi maisha ya kawaida ya uungwana na msikivu na alikuwa mtu wa kupokea maoni na zaidi ya yote alinifundisha kuwa na maamuzi hasa kwenye vitu vyenye maslahi na Taifa, yeye ndiye baba wa mageuzi ya kiuchumi na siasa hapa nchini Tanzania,” “ameeleza.

Naye Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema ni majonzi kuondokewa na Mzee Mwinyi lakini siku ya furaha ya kusherekea maisha yake kwa mengi aliyofanya kutumikia Taifa hili kwani amekuwa na juhudi nyingi za kuleta maendeleo hasa kwenye nyanja ya uchumi na siasa.

Amesema Mzee Mwinyi alipokea nchi ikiwa kwenye matatizo makubwa lakini aliweza kupambana kuitoa nchi kwe uhaba wa uchumi.

“Mzee Mwinyi aliposhika uongozi hali ilivyokuwa wakati huo ilikuwa mbaya sana sasa hivi nchi tuna matatizo tuna upungufu wa sukari, matatizo ya umeme tuna matatizo ya maji lakini matatizo tuliyonayo sasa hivi ni madogo sana ukilinganisha na wakati wa Mwinyi aliposhika uongozi, “amesema Jaji warioba.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) , Abdulrhaman Kinana amesema sote leo ni mashahidi kwamba Hayati Mzee Mwinyi alifanya jitihada za kuitoa Tanzania kwenye chama kimoja kwenda kwenye mfumo wa vyama vyingi.

Amesema suala hilo halikuwa rahisi vilevile aliwapeleka kwenye uchumi hiari, alifanya hayo yote na mengine mengi kwa kumshirikisha Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere kwa lengo la kuhakikisha mabadiliko yanafanyika kwa utulivu ili kulinda umoja wetu na amani yetu.

Tukio la kuagwa kwa Mwili wa Rais huyo Mstaafu wa Awamu ya Pili wa limehudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali, viongozi mbalimbali wa kitaifa, Mabalozi wa Mataifa mbalimbali, viongozi wa ulinzi na Usalama, viongozi wa dini zote pamoja na wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles