27.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Doto Biteko: Mchango wa sanaa katika pato la Taifa ni duni

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema sekta ya sanaa inakuwa kwa kasi kwa ya asilimia 19 lakini mchango wake katika pato la Taifa ni duni asilimia 0.3.

Ameyasema hayo leo Februari 29, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wadau wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa uliohudhuliwa na viongozi mbalimbali na wadau wa mfuko huo.

Ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuweka mazingira mazuri kwa wasanii ili kukuza sekta ya hiyo sambamba na ukuaji wa uchumi.

Dk. Biteko ameitaka Wizara kuwa kiungo cha wasanii na Serikali hasa katika kazi ambazo wananchi wanapaswa kupata ujumbe au kuhamasishwa, huku wakipata mapato stahiki.

” Nawapongeza wasanii wote ambao wamekuwa wakizingatia vigezo na masharti ya kukopa na kurejesha mikopo kwa wakati na hivyo kuwataka wasanii kuhimizana juu ya umuhimu wa kukopa na kurejesha mikopo ili iweze kuwanufaisha wengine,”amesema.

Aidha amesema watanzania wana kila sababu ya kulinda utamaduni na utu wao na kuepuka kuudhalilisha dhidi ya utamaduni wa kigeni.

“Kupitia kazi za sanaa lazima tuoneshe kuupenda utamaduni wetu na kuuishi na tunataka utamaduni huo uende mpaka nje ya mipaka ya nchi, kwani Taifa lisilo na utamaduni ni Taifa mfu hivyo tuuenzi utamaduni wetu ambao ni mzuri na utamaduni una nguvu kuzidi teknolojia,” amesema Dk. Biteko.

Amewasifu wasanii nchini kwa kukataa kupuuza utamaduni wa Taifa na kuamua kwa pamoja kuupa heshima utamaduni huo kupitia kazi zao za sanaa.

Amesema wasanii wana wajibu mkubwa wa kulifanya Taifa kuwa hai, kuliondoa kwenye wimbi la kupotea duniani na kuwafanya watanzania waone lugha yao, tamaduni zao na desturi zao zinapaswa kuheshimiwa na kila mtu.

Ameongeza kuwa kwa miaka mingi kazi ya sanaa ilikuwa ni kuelimisha na kuburudisha lakini sasa imepanuka na imekuwa ni nyenzo ya kutengeneza ajira na ndio maana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliamua kuufufua mfuko huo ambao ulianzishwa mwaka 1992 na ambao ulikuwa ukisuasua.

Amewataka wasanii kutumia kazi zao kuhamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu ili wananchi waweze kujitokeza kwa wingi na kuchagua viongozi wanaopenda maendeleo na kuunganisha wananchi.

Naye Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, amemshukuru Rais, Dk. Samia kwa maono yake na upendo kwa wasanii nchini ndio maana ameufufua mfuko huo na kuweka fedha ambazo zinawasaidia wasanii katika kuanzisha, kuboressha na kupanua shughuli zao za sanaa.

Amesema pamoja na faida za mfuko bado kuna changamoto mbalimbali kama vile wakopaji kutorejesha mikopo kwa wakati na mfuko kuwa na chanzo kidogo cha fedha ambapo Wizara inachukua hatua mbalimbali kushughulikia changamoto hizo.

Katika Mfuko huu utaanzishwa sehemu ya kutoa mafunzo maalum kwa wasanii wachanga ya kuwanoa na kuwawezesha kuunda taasisi ambayo itakua na itakubalika kwenye benki ili kupata mikopo,”amesema Dk. Ndumbaro.

Ameongeza kuwa wizara hiyo inaangalia sekta ya sanaa na utamaduni kama chanzo cha ajira na uchumi hivyo ameomba wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi hizo za Serikali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Abdulmajid Nsekela amesema mfuko huo unatoa huduma kuu tatu ambazo ni mikopo ya masharti nafuu kwa walengwa katika sekta, kuwajengea uwezo wasanii kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ujasiriamali, urasimishaji, nidhamu ya biashara na kuwapa nafasi ya kuona fursa mpya zilizopo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles