DEFOE: PICHA ZA BRADLEY LOWERY ZITANITESA

0
1785

LONDON, ENGLAND

MASHAMBULIAJI mpya wa klabu ya A.F.C. Bournemouth, Jermain Defoe, ameweka wazi kuwa picha za marehemu Bradley Lowery ambaye alikuwa ni shabiki mkubwa wa klabu ya Sunderland, zitamtesa kwa kiasi kikubwa.

Bradley ambaye alikuwa na umri wa miaka sita, amepoteza maisha juzi baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa saratani tangu akiwa na miezi 18 baada ya kuzaliwa kwake.

Mtoto huyo aliteka hisia za mashabiki wengi wa soka duniani kwa kuwa na mapenzi ya dhati na klabu ya Sunderland pamoja na aliyekuwa mshambuliaji wa klabu hiyo Defoe.

Defoe alikuwa anatumia muda mwingi kumpa faraja mtoto huyo kwa kuwa alionesha upendo wa dhati kwake, hivyo amedai picha alizopiga naye wakati wa uhai wake zitamtesa kwa kuwa atakuwa anayakumbuka baadhi ya mambo ambayo walikuwa wanayaongea.

“Bradley alinifanya niwe karibu na familia yake, alikuwa rafiki wa kweli kwangu kwa kuwa alionesha upendo wa dhati, kila nikimwangalia macho yake yalikuwa yanajieleza kwamba ananipenda sana, upendo wake hauelezeki.

Nitaendelea kulia kila wakati nikimkumbuka, ninashindwa kuzuia hisia zangu kwa kuwa nimekuwa nikikaa naye na kujua tatizo linalomsumbua kwa kipindi kirefu, ilikuwa haiwezi kupita siku moja bila ya kuwapigia simu wazazi wake au kumfikiria Bradley.

“Nitaendelea kumkumbuka maishani mwangu na ninaamini picha zake zitanitesa sana kwa kuwa zitanifanya nikumbuke ukaribu wake kwangu.

“Picha zake nyingi zipo kwangu, hata nyumbani kwao kuna picha zetu nyingi ambazo wameziweka ukutani, lakini leo hii ameondoka, ninaamini ipo siku tutaonana,” alisema Defoe.

Desemba mwaka jana, mtoto huyo alishtua mashabiki duniani baada ya madaktari kudai hali aliyonayo mtoto huyo hawezi kuishi zaidi ya miezi miwili, hivyo walitangaza kwamba hadi kufikia mwezi wa pili mwaka huu angepoteza maisha.

Kauli hiyo iliwafanya mashabiki wengi kuanza kumjua na kufuatilia hali ya afya yake, lakini ilipita mwezi wa pili huku akiwa hai, ila hali yake bado ilionekana kuwa mbaya siku hadi siku hadi juzi alipopoteza maisha akiwa mikononi mwa mama na baba yake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here