23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

DC Msoma aridhishwa na maendeleo ya miradi ya maji wilayani humo

Na Shomary Binda, Musoma

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk. Halfan Haule ametembelea na kukagua miradi mitano ya maji inayotekelezwa na Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika Halmashauri ya wilaya ya Musoma, ambapo ameridhishwa na Maendeleo ya miradi hiyo na amesisitiza juhudi thabiti za usimamizi ziendelee kufanywa na (RUWASA) ili ikamilike mapema na ianze kutoa huduma kwa wananchi.

Dk. Haule ameyasema hayo Julai 13, 2021 alipotembelea miradi hiyo akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama pamoja na Wataalamu wa ( RUWASA) ambapo alisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuona Wananchi wanaondokana na tatizo la maji hususan kinamama ambao hutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya kazi za uzalishaji mali.

“Serikali imekusudia kumtua ndoo mama, haitapendeza hata kidogo kuona kinamama wanateseka kutafuta maji badala ya kuyapata kwa urahisi kabisa. Niombe juhudi zifanyike katika miradi yote mitano ambayo bado haijaanza kutoa huduma kusudi wananchi sasa wasitafute maji kwa shida bali watumie muda mwingi kufanya kazi kukuza uchumi wao,” alisema Dk. Haule.

Miradi iliyotembelewa ni pamoja na mradi wa maji wa Kigera etuma -Kakisheri wenye thamani ya Sh bilioni 1.1 ingawa hadi sasa serikali imetoa zaidi ya Sh milioni 300 na ulianza kuteketezwa Desemba 1, mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Agosti 30, 2021 iwapo serikali itakamilisha utoaji wa fedha kumalizia mradi huo.

Mbali na huo, mradi mwingine ni ukarabati wa mradi wa maji Butata, Kastamu na Kakisheri wenye thamani ya Sh milioni 286 ambapo kwa sasa upo hatua nzuri kwani shughuli zilizobakia ni ufungaji wa mfumo wa umeme, ujenzi wa nyumba ya mashine upo hatua ya mwisho, huku mradi mwingine ni wa Makojo Chitar, ambao walipata Sh milioni 35 na hadi sasa umekamilika na hatua iliyobakia ni kufunga pampu kwa ajili ya kuufanyia majaribio ikiwa ni hatua ya kutoa huduma ya maji kwa wananchi.

Aidha, mradi wa maji wa Suguti unaogharimu Sh bilioni 1 pia ulitembelewa ambapo umekamilika na kwamba, hatua iliyobakia ni kufanya upanuzi wa mradi huo katika maeneo mengine kuwezesha yapaye huduma ya maji na utakamilika ifikapo Julai 30, 2021.

Pia mradi wa maji wa Hospitali ya wilaya unaojengwa Kwikonero na vijiji vya seka na Kaboni ulioanza kujengwa Juni 20, 2021 ukiendelea vizuri kwani kilichosalia ni ujenzi wa tenki na ulazaji wa mabomba unaendelea na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 20, 2021.

Dk. Haule alizungumza pia na kamati za maji ambazo zinajukumu la kusimamia fedha za mauzo ya maji kwa nyakati tofauti katika kila eneo la mradi, ambapo alizitaka kuongeza ubunifu hususan kuwapelekea huduma ya maji majumbani mwao wananchi, hatua ambayo itarahisisha pia makusanyo ya ankara za maji. Huku akizionya kutotumia fedha hizo kwa manufaa yao na kwamba, serikali itachukua hatua kali kwa kamati itakayofuja fedha.

Pia, alizitaka kamati hizo na wananchi kwa ujumla, kuwa walinzi wa miundombinu ya maji inayojengwa kwa kutojihusisha na vitendo vya wizi kwani serikali imetumia fedha nyingi kuhakikisha wananchi wake wanaondokana na adha hiyo.

Kwa Upande wake Meneja wa RUWASA wilaya ya Musoma, Mhandisi Edward Sironga alisema hadi kufikia Juni 2021, ilikuwa na wakazi 276,586 ambapo jumla ya wakazi 165, 952 sawa na asilimia 60.5 wanapata huduma ya maji safi na salama hiyo ni ongezeko la asilimia 4.5 ukilinganisha na asilimia 55.7 iliyokiwepo hadi kufikia Desemba 2020, huku akibainisha kuwa miradi yote inayojengwa sasa ikimalizika watafikia asilimia 65.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles