22 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

CHANJO YATIBU ASILIMIA 97 YA SARATANI MWILINI MWA PANYA

JOSEPH HIZA Na MTANDAO


SARATANI ni maradhi hatari na mzigo mkubwa na gharama kwa maisha na kiuchumi, tatizo ambalo dunia linaikabili kwa muda mrefu sasa.

Wakati wataalamu wa afya wakiendelea na tafiti na kupata mwanga zaidi kuhusu njia tofauti za kutibu saratani, inafahamika sasa kuna nafasi kubwa sana kutumia mifumo yetu ya kinga mwilini kuiangamiza saratani.

Njia za tiba kama vile chemotherapy zinafaa kutibu saratani, lakini pia zina athari kwa mifumo yetu ya kinga.

Mwezi uliopita habari njema zilipatikana zikitangaza ujio wa chanjo mpya ya saratani, ambayo itaanza majaribio miilini mwa wanadamu baada ya kuonesha mafanikio makubwa katika majaribio ya wanyama.

Jarida la Sayansi la Translational Medicine lilichapisha utafiti wa chanjo hiyo ambayo imeweza kutibu asilimia 97 ya maradhi hayo katika panya, itajaribiwa kwa wagonjwa ambao wana uvimbe ulio katika hatua za mwanzo baadaye mwaka huu.

Wagonjwa wapokeao chanjo hiyo, ambayo ina dawa mbili, hawatahitaji tiba yoyote ya chemotherapy, huku dozi yake ikiwa na madhara yanayotarajia kuwa homa na maumivu katika eneo lililochomwa sindano ya chanjo tu.

Kwa taarifa, Chemotherapy ni tiba inayotumia kemikali ambazo zinavuruga tendo la seli za mwili kujigawa na kusababisha seli hizo kujiua zenyewe.

Tiba hii hulenga zile seli ambazo zinajigawa kwa haraka na kwa kawaida hutumika kutibu saratani zilizoenea kutoka eneo moja la mwili hadi jingine kwa sababu kemikali hizi zina uwezo wa kusambaa katika mwili wote wa mgonjwa. Hii ni tiba ya lazima kwa aina fulani ya saratani za aina ya leukemia na lymphoma.

Kwa kifupi, Chemotherapy hutolewa kwa vipindi ili mwili uweze kupona katikati ya dozi moja na nyingine.

Madhara ya tiba hii ni pamoja na kunyonyoka nywele, kichefuchefu, uchovu wa mwili na kutapika.

Ni tiba ambayo wakati mwingine hutolewa kwenda sambamba na tiba nyingine za saratani.

Tukirudia kuhusu chanjo hii mpya; iwapo itathibitishwa, watafiti hawatarajii kama itakuwa tayari kutibu watu kwa mwaka au miaka miwili ijayo.

Badala ya kutengeneza kinga ya kudumu, dozi inafanya kazi kwa kuuchangamsha mfumo wa kinga kushambulia vivimbe vya saratani.

Hili linatarajia kuleta ufanisi kwa maradhi ya saratani ya lymphoma yaliyo hatua za awali, ambayo huathiri aina fulani ya chembe nyeupe za damu na kuitikia matibabu, kwa sababu hii mara nyingi kubainishwa na mfumo wa kinga, tofauti na aina nyingine za maradhi kama vile saratani ya utumbo.

Mwandishi mwenza wa utafiti huo, Dk. Ronald Levy, kutoka Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani anasema: “Tuna tatizo kubwa katika maradhi ya saratani na kamwe hatutaridhika hadi tupate suluhu kwa kila mtu.”

 

Utafiti utahusisha nini?

Chanjo itajaribiwa kupitia tafiti mbili. Jumla ya wagonjwa 35 wa saratani ya lymphoma watashiriki katika majaribio hayo. Kila mshiriki atapokea kiwango cha chini cha dozi ya mionzi sambamba raundi mbili za chanjo kipindi cha wiki sita.

Maelezo zaidi kama vile muda unaotenganisha baina ya chanjo hizo mbili ndani ya kipindi hicho bado haujafahamika.

Chanjo nyingine kama hiyo tayari imepitishwa kwa ajili ya saratani aina ya leukemia na lymphoma.

Kwa ufupi leukemia ni aina ya saratani zinazoanzia ndani ya ute wa mifupa na kukusanyika katika mishipa ya damu.

Kadhalika lymphoma, ni aina ya saratani zinazoanza kwenye mkono wa vifundo vya limfu na kwenye tishu za kinga ya mwili.

Chanjo hii mpya inahusisha kuondoa chembe za mfumo wa kinga kutoka miili ya wagonjwa na kuziingiza kama jeni kushambulia vivimbe kabla ya kurudishwa tena.

Matibabu hayo huitwa CAR-T, hugharimu dola nusu milioni kwa kila mgonjwa na zinaweza kusababisha homa, mkanganyiko, viungo kushindwa kufanya kazi na mfumo wa kinga kuvurugika.

Mtaalamu wa saratani, Dk. Michelle Hermiston kutoka Chuo Kikuu cha California, San Fransisco, anasema: “Hii si tiba ndogo.”

“Utafiti unapaswa kufanyika kuangalia iwapo vivimbe vinaweza kudhibitiwa ili kuvifanya viitikie vizuri kwa mfumo wa kinga.

“Tunaweza kutengeneza uvimbe uonekane zaidi katika mfumo wa kinga? Tuna kazi kubwa mno kwa sasa.”

Kuponya saratani kwa panya

Watafiti waliingiza vivimbe viwili vinavyofanana katika maeneo mawili tofauti ya miili ya panya.

Moja ya vivimbe ilichomwa sindano ya chanjo, kitu kilichofanya  kuamka kwa seli T. Seli hizo huzindua mfumo wa kinga  kuitikia kukabili mashambulizi kutoka kwa adui kama vile virusi, katika miili ya wanyama.

Watafiti walibaini wakati walipowasilisha panya 90, waliokuwa na maradhi ya lymphoma,  87 miongoni mwao waliponywa kabisa saratani.

Wale watatu waliobakia waliorudiwa tena na maradhi, lakini matibabu ya ziada yakatokomeza mara moja saratani hiyo.

Hilo linawakilisha mafanikio makubwa ya kutibu saratani kama lymphoma.

Hata hivyo, tiba hii pamoja na kuonesha kuwa na uwezo wa kutibu aina nyingine za saratani na kuzuia maradhi hayo kutokea tena haiwezi kukabili aina nyingine nyingi.

Kwa mfano panya waliokuwa na saratani ya titi waliweza kuitikia matibabu lakini si kwa ufanisi kama wale wa lymphoma.

Kadhalika panya wenye saratani ya utumbo mkubwa hawakuweza kabisa kuitikia tiba hiyo.

Hiyo inamaanisha dawa iliyotumika si kwa ajili ya aina zote za saratani, lakini mafanikio yanamaanisha kuwapo uwezekano wa kuondoa changamoto hiyo siku za usoni.

Mwisho

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,284FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles