25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Chaguo la Mbowe lang’oka Chadema

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vicent Mashinji, amehitimisha safari yake ya uanachama ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dk. Mashinji ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu, amejiunga na CCM jana katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo Lumumba, Dar es Salaam na kupokewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho tawala, Humphrey Polepole.

Katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema, alikuwa ni chaguo la Freeman Mbowe, ambaye mwaka 2016 alipata wakati mgumu kushawishi kikao cha Baraza Kuu la chama hicho kilichofanyika Mwanza kukubali kupitisha jina lake amrithi Dk. Wilbroad Slaa aliyejiuzulu mwaka 2015 wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Kutokana na hali hiyo, Mbowe ilibidi aombe msaada kutoka kwa wazee wa chama hicho walioshiriki kikao hicho na kufanikiwa kukishawishi na jina la Dk. Mashinji likapita.

Baada ya hapo jina la Dk. Mashinji lilipitishwa kwa kura za kunyoosha mikono na kuwaacha wajumbe midomo wazi.

Wakati huo aliyekuwa anapewa nafasi kubwa kurithi nafasi ya Dk. Slaa alikuwa ni Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye ambaye alikuwa amepata jina kwenye chama hicho baada ya kuzunguka nchi nzima kufanya kampeni akimnadi mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.

Baada ya Dk. Mashinji kushika nafasi hiyo, baadaye yaliibuka malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanachama, wakisema mtendaji huyo mkuu wa chama amepwaya kwenye viatu vya Dk. Slaa.

Hata hivyo, baadhi walisema yeye amekuwa akifanya vizuri zaidi kwenye miradi ya kujenga chama, ikiwa ni pamoja na mpango wa ‘Chadema ni Msingi’, ambao umewezesha chama hicho kwa mara ya kwanza kuwa na uongozi kuanzia ngazi ya mtaa.

Katika Mkutano Mkuu wa Chadema wa Desemba mwaka jana, Mbowe hakumteua tena Dk. Mashinji kuwa katibu mkuu na badala yake akapendekeza jina la Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na kupigiwa kura na Baraza Kuu.

Hata hivyo, baada ya Dk. Mashinji kukosa nafasi hiyo, alinukuliwa na gazeti moja la kila siku akisema alitamani kuendelea kuwa katibu mkuu ili aweze kumalizia mipango aliyokuwa nayo, ikiwamo maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

“Nilipanga kuhakikisha tunapata wagombea wanaotokana na wananchi, tungekwenda kutekeleza agizo la Kamati Kuu la kuwaomba wanaotaka kugombea urais, ubunge na udiwani wajitokeze.

“Wangetangazwa mapema ili wananchi waanze kuwatafiti, hatimaye kumpata kiongozi anayetokana nao. Hilo lingefanyika kuanzia Januari mwakani (mwaka huu).

“Katika nchi nyingine, wagombea urais wanajulikana hata mwaka mmoja au miwili kabla na hili linawafanya watu wachambue makandokando yake. Hata tukija kufanya kura ya maoni tunafanya kwa mtu anayejulikana,” alisema Dk. Mashinji huku akisisitiza kuwa iwapo Mnyika ataona inafaa anaweza kulifanyia kazi hilo.

KUHAMIA CCM

Katika maelezo yake ya jana, Dk. Mashinji alisema baada ya kutafakari kwa kina, ameona CCM ndicho chama kinachosikiliza maoni ya watu na anaona ndicho kitakachomkuza zaidi kwa sababu bado yeye ni kijana.

“Baada ya kukaa na kutafakari kwa kina na kuangalia mwenendo mzima wa siasa, uchumi, shughuli za kijamii, nikaona ni muda mwafaka kuongeza kasi ya maendeleo ya watu na vitu.

“Sasa katika kuangalia utayari kwamba kina nani wako tayari, kwa upande wetu Chadema tuliona tuko mbali sana kuchochea hayo maendeleo.

“Pamoja na kwamba tulitengeneza sera, lakini kwa bahati mbaya tulikosa uelewa wa pamoja ndani na nje ya Chadema, nakumbuka kwenye shereha za Uhuru mwenyekiti (Freeman Mbowe) alisisitiza kuwepo na maridhiano, ni kweli tunahitaji maridhiano, sasa huwezi kuwa na maridhiano kama huna uelewa wa pamoja,” alisema Dk. Mashinji.

Alisema pamoja na kwamba Tanzania haiundwi na malaika bali na binadamu, hivyo lazima kuwe na upungufu, lakini ameona CCM inasikiliza watu kwa sababu kuna baadhi ya mambo wameyatoa upinzani na kuyafanyia kazi.

“Sasa kukaa na kulumbana asubuhi na mchana tutaendelea siku gani, nikaona ni heri nije hapa Lumumba niongee na wenzangu kama nitapata fursa ya kutoa mchango wangu kwenye taifa langu, mimi bado ni kijana, nina miaka 47, kwa umri huu bado ni kijana, naamini CCM kinaweza kunilea na kunikuza.

“Kama Rais anavyosisitiza maendeleo hayana chama na ni kweli, tutake tusitake maendeleo hayana chama, kwa hiyo nimwombe Mwenyekiti wa CCM (Rais Magufuli) nijiunge na CCM kuchangia maendeleo ya nchi yangu, ninaona kabisa CCM kiko tayari kuendeleza Watanzania, huko nilikotoka huo utayari siuoni,” alisema Dk. Mashinji.

Kutokana na hilo, Polepole alimkaribisha na kumhakikishia kuwa kwa niaba ya wakuu wa chama hicho tawala wakiongozwa na Rais Magufuli wamempokea rasmi kujiunga na CCM.

CHADEMA WAMJIBU

Akimzungumzia Dk. Mashinji, Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema walijua mapema kuwa angehamia CCM na ndio sababu Baraza Kuu la chama halikumteua tena kuwa katibu mkuu.

“Mashinji ni katibu mkuu pekee katika historia ya Chadema aliyedumu kwa muda mfupi sana na baada ya mgombea urais wake Sumaye kwenda na mwenyekiti wake Mwambe (Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe) kuhama tulijua kuwa asingebaki,” alisema Mrema.

Alisema timu ya intelinjesia ya chama hicho iliwapelekea taarifa mapema kuhusu mikakati miovu ya Dk. Mashinji na kwamba ndio maana hawakuteuliwa na chama.

“Hawa waliohama sio wa mwisho, wako wengine wengi nao watakihama chama, ni suala la muda tu,” alisema Mrema.

Alisema wanafahamu kwamba CCM wanapanga hayo ili kuwahamisha wananchi kwenye mijadala ya kudai tume huru ya uchaguzi na kuanza kujadili waliohama Chadema.

Pamoja na hilo, alisema Chadema itaendelea kuwa imara na kusonga mbele.

HISTORIA YA DK. MASHINJI

Dk. Mashinji alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chadema mwaka 2015.

Alikuwa katibu mkuu wa nne wa chama hicho kikuu cha upinzani tangu kianzishwe baada ya Bob Makani, Dk. Walid Aman Kabourou na Dk. Slaa.

Dk. Mashinji aliyezaliwa katika Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, alianza elimu ya msingi katika Shule ya Iligamba Januari mwaka 1981 hadi Oktoba 1987 na kisha kuendelea na masomo Shule ya Sekondari Makoko Seminari kuanzia Januari 1988 hadi Oktoba 1991 alipohitimu na kufaulu kujiunga na Shule ya Sekondari Mzumbe kuanzia Julai 1992 hadi Juni 1994 alipohitimu kidato cha sita.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda mwaka 1995 hadi alipohitimu mwaka 2001 na kutunukiwa shahada ya udaktari.

Mwaka 2003 hadi 2005 alisomea Shahada ya Uzamili ya Anaesthesiology Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (Muhas) na mwaka 2007-2010, alijiunga na Taasisi ya Teknolojia ya Blekinge ya Sweden ambako alisomea shahada nyingine ya uzamili, safari hii katika Utawala na Biashara (MBA).

Mwaka 2016 alikuwa mwanafunzi wa shahada nyingine ya uzamili katika afya ya jamii aliyosomea Chuo Kikuu cha Roehampton, Uingereza na pia Shahada ya Uzamivu ya Uongozi katika Chuo Kikuu Huria.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,526FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles