28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

CAG aanika upigaji mashirikanya umma

Na Fredy Azzah-Dar es Salaam

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2017/18, imeanika ubadhirifu wa mabilioni ya fedha na hatari ya kupata hasara kutokana na maamuzi mbalimbali ya viongozi wa taasisi hizo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kanuni ya 203 (1) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma za mwaka 2013 (marekebisho ya 2016) inataka kufanyika kwa tathmini ya zabuni kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa katika nyaraka za zabuni na tathmini hiyo itafanywa kwa kutumia vigezo vilivyotajwa wazi katika nyaraka za zabuni na Kanuni ya 213 hutoa vigezo vya mzabuni wa chini.

NEMBO YA BENKI YA TPB KWA SH MILIONI 495.75

 “Benki ya Posta (TPB) ilihusika na manunuzi ya kuchapa nembo mpya ya benki. Timu ya tathmini ya zabuni ilipendekeza M/s. CI Group Marketing Solution kwa bei ya Sh milioni 224 kama mtoa zabuni.

“Hata hivyo, Bodi ya Zabuni kupitia azimio lake iliazimia kazi hiyo asipewe M/s.CI Group Marketing Solution kwa kigezo kuwa alichelewa kukamilisha kazi ya tawi la Kijitonyama lililotumika kama tawi la mfano.

“Bodi ya zabuni iliamua kumpa kazi hiyo mzabuni aliyeshika nafasi ya pili, M/s. Jupiter Company Limited kwa gharama ya Sh milioni 495.

“Maamuzi yaliyofanywa na Bodi ya Zabuni yaliongeza gharama kwa Sh milioni 271 ambayo ni asilimia 120 ya bei ya mzabuni aliyependekezwa awali, ambaye pia alikuwa na uzoefu wa kazi hiyo.

“Kwa hiyo, benki iliingia gharama kubwa ili tu kutochelewa kwa kuchapa nembo ambayo haiwezi kuzuia shughuli za benki.

“Huu ni uamuzi unaotia shaka sababu gharama na ongezeko la Sh milioni 271 haliwezi kuwa sahihi kwa kutengeneza nembo,” inasema ripoti hiyo.

UDART INAJIENDESHA KWA HASARA YA SH BILIONI 6.78

Ripoti hiyo inasema mradi wa mabasi ya mwendokasi Dar es Salaam ulianza Mei 10, 2016 na katika tathmini ya miezi minane kuanzia tarehe ya kuanza kwa mradi hadi Desemba 30, 2016, CAG alibaini Kampuni ya Udart imekuwa ikifanya kazi kwa hasara.

Inasema matumizi ya kampuni hiyo yalikuwa makubwa zaidi ya mapato kwa kiasi cha Sh bilioni 6.78.

“Jumla ya matumizi ilikuwa Sh bilioni 26.57 wakati mapato yalikuwa Sh bilioni 19.78. Pia nilibaini kuwa hasara hii ilitokana na kutunza vibaya,” inasema ripoti hiyo.

Inafafanua kwamba Udart ilitoa taarifa za gharama za mafuta kuwa Sh bilioni 6.02, wakati leja ya mafuta ilionesha kiasi cha mafuta ni Sh bilioni 4.79, hivyo taarifa iliongeza Sh bilioni 1.25.

UPIGAJI MILIONI 750 UJENZI WA UZIO UDART

Ripoti hiyo inasema Udart ililipa Sh milioni 750 kwa M/s. Longway Engineering Services kwa kujenga uzio katika kituo cha mabasi Kimara, Kivukoni, Ubungo na Morocco. Hata hivyo, uzio ulijengwa Kimara tu kwa Sh milioni 241.69 wakati hakukuwa na ujenzi wa katika vituo vingine vitatu vilivyotajwa.

“Kiasi kilicholipwa cha Sh milioni 508.31 kwa ajili ya fensi katika vituo vitatu hakikuthibitika kama kilirejeshwa, hivyo kuwa na uwezekano mkubwa kuwa kilitumika vibaya,” inasema ripoti hiyo.

MAAJABU KADI MWENDOKASI

Ripoti Inasema kutolewa kwa kadi za kulipia usafiri wa mabasi ya mwendokasi kulisitishwa kwa sababu ya gharama kubwa ya uzalishaji wake.

 “Gharama hiyo ni kubwa kuliko mauzo yake kwa abiria. Nilibaini kuwa gharama ya kuzalisha kadi moja ni Sh 4,500 ikiwa ni pamoja na kodi za Serikali na gharama za uagizaji, wakati Serikali ilitangaza kadi moja kuuzwa kwa Sh 500,” inasema ripoti hiyo.

DENI LA TRA SH BILIONI 5.35

Ripoti inasema Sh bilioni 5.35 za TRA hazikuripotiwa kwenye taarifa za fedha za UDA kama sehemu ya deni lake.

“Deni hili lilithibitishwa na TRA kupitia barua yenye Kumb. Na. TRA/CCE/C/1 ya 31/1/2018. Kati ya deni hilo, Sh bilioni 2.11 zilikuwa adhabu ya kuchelewesha kulipa kwa wakati.

 “Ninapendekeza UDA itambue deni la TRA la Sh bilioni 5.35 katika taarifa zake za hesabu,” anasema CAG.

MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA COSTECH

Kuhusu Tume ya Sayansi (COSTECH), ripoti hiyo inasema taasisi hiyo ilitoa Sh milioni 800 kwa Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) katika vipindi tofauti bila kuwa na mamlaka sahihi ya Bodi ya Makamishina wa COSTECH.

“Taasisi ya Afya Ifakara ilikiri kupata fedha hizo na kuzitumia, lakini sikuweza kutambua fedha hizo zilitumika kwa matumizi gani. Hii ni kwa kuwa fedha hizo zilichanganywa na fedha nyingine.

“Zaidi ya hayo, COSTECH iliipatia Dar Techno Hama Business Incubator (DTBi) kiasi cha Sh bilioni 1.1 kwa vipindi tofauti bila ya kuwa na makubaliano yoyote.

“Pia DTBi inahudumiwa na COSTECH na wamepewa ofisi bure, ikiwa ni pamoja na kulipiwa gharama nyingine kama umeme na maji.

“Gharama hizi zinalipwa na COSTECH ingawa DTBi ni taasisi binafsi tokea mwaka 2011.

“Ninapendekeza COSTECH kufuata taratibu zilizopo katika kutoa ruzuku.

“Pia ihakikishe kuwa taasisi hizi mbili (IHI na DTBi) zilizopewa fedha zinatumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Aidha, pawe na uwajibikaji wa fedha hizo, ikiwa ni pamoja na kuzitolea taarifa kwa COSTECH,” inasema ripoti hiyo ya CAG.

UPIGAJI SH BILIONI 3.80 UNUNUZI ARDHI

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa (NSSF) uliingia mikataba Septemba 16, 2010 naOktoba 12, 2010 ya kununua ekari 277 (Muuzaji wa kwanza) na ekari 180 (Muuzaji wa pili) eneo la Kiluvya kwa Sh bilioni 3.32 na Sh bilioni 1.62, Mtawalia.

“Kufuatia mapitio ya taarifa ya tathmini ya ekari 277, nilibaini kuwa thamani ya ardhi hiyo kwa kipindi cha Oktoba 2010 ilikuwa Sh milioni 416.40, wakati makadirio ya thamani ya soko kwa ekari 180 ilikuwa Sh milioni 720.

“Kwahiyo, gharama ya ardhi iliyonunuliwa ilizidishwa kwa kiasi cha Sh bilioni 2.90 na Sh milioni 900 Mtawalia, na hivyo kusababisha jumla ya hasara kuwa Sh bilioni 3.80.

“Nilibaini pia kuwa muuzaji wa kwanza aliripoti mauzo yake kwa TRA kwa Sh milioni 900 badala ya Sh bilioni 3.32, kwa sababu hiyo kodi (stamp duty) ya Sh milioni 24.24 haikulipwa,” ilisema ripoti hiyo.

MADUDU TANAPA

Sehemu ya madudu yaliyo kwenye ripoti hiyo ni Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), ambayo ilifanya miradi miwili na mkandarasi JECCS Construction & Supplies Ltd na Secao Builder Co Ltd ambapo gharama ya mikataba yote miwili ilikuwa ni Sh milioni 961.

“Kipindi cha mkataba kwa miradi hii miwili kilimalizika Februari 17, 2018 na Oktoba 10, 2017, Mtawalia.

“Hata hivyo, hadi wakati wa kuandika ripoti yangu Februari 2019, yapata mwaka mmoja kutoka tarehe iliyopangwa kukamilisha miradi hiyo, miradi hiyo haikuwa imekamilika,” inasema.

MASHARTI MABOVU MKATABA MAJI

Ripoti ya CAG inasema Oktoba 2012, Wizara ya Fedha ilikopa Dola za Marekani milioni 178.13 kutoka Benki ya India ijulikanayo kwa jina la Export-Import Bank of India kuiwezesha DAWASA kutekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Chalinze.

“Sharti mojawapo la mkataba wa mkopo huo linataka asilimia 75 ya bidhaa zinazonunuliwa na huduma zitoke nchini India. Maana yake kuanzia vifaa, mkandarasi, mashine na vifaa muhimu vipatikane kutoka India,” inasema ripoti hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,455FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles