23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

BONGO REGGAE: MKIAMUA KULALA MSIKOROME, SIMBA WA KALE WANAAMKA

HUSEMWA kuwa aliyelala usimwamshe ukimwamsha utalala wewe lakini pia ukilala usikorome ili usikere wengine waliokuwa karibu yako, lakini sizungumzii usingizi wa binadamu nazungumzia usingizi wa miondoko ya kuruka matope a.k.a Reggae lakini sio huko duniani bali hapa Bongo.

Ilikamata ikabamba miaka iliyopita katika ‘Back’ ya hisia kali za ukombozi Kusini mwa bara la Afrika, ukombozi ukapatikana nyimbo zikageuka kuimbwa kwa Kiswahili kwa mambo ya hapa nyumbani katika ‘Front’ mpya lakini baadaye maendeleo yakasonga na mikong’osio ya kila aina ikagubika, maudhui yakapotea kwani Reggae yenye ujumbe mgumu ikapoteza mashiko yakaibuka mengine laini kuliko Reggae za Kibitonga zinavyopaswa kuwa kwani kanuni zilipindwa.

 ‘Front’ mpya ikawa kukwepa kujikita kwenye weledi kwa kurahisisha kama ilivyo mitindo mingine inayotegemea kupigiwa badala ya kupiga na kuwakilisha kiukweli, hapo ndipo kona ya usingizi mpya ikajiri ambayo inasumbua hadi sasa.

Wakongwe wakalaumiwa kwamba wanautosa muziki huo lakini ukweli ni kuwa walishafanya yao makubwa zaidi ndiyo maana vizazi vilivyofuatia, vilipata njia ya kukubalika kirahisi kwa kuwa kuna waliojenga msingi iliyorahisisha kujenga ukuta.

Uhafidhina wa kiimani ukarudi upya na kubaguana makundi kukajiri na kilichoafuatia katika ‘Bongo Reggae’ ni kuoneshana vidole kwa kupimia imani badala ya muziki, kwani Reggae si mtindo wa muziki kama ilivyo mingine ila tu una maudhui na mashiko yake yanayojitofautisha?

Hiyo ndiyo mikoromo ya waliolala waliodharau yaliyofanywa na simba wa kale ambao hawakujali sana kedi zao waliendelea kivyao kwa mfumo wa kuusoma mchezo, mbinu zao kwa sasa zimefutikwa chini ya zulia lakini ‘Front’ italipuka muda si mrefu kwa kuwa simba wa kale wameamua kurudi kwenye ‘Ufalme’ wa pori na kutimiza kilichoshindwa kutimizwa na waliodandia treni likiwa limeshashika kasi na matokeo yake ni ajali ya kikazi kwenye muziki.

Weledi haukuwatamalakia bali uliwatupa kama walivyoamua kuutupa na hakuna jana kama haikuwepo juzi wala leo isingekuwepo bila jana na kesho na keshokutwa hazitajiri kama leo isingejiri.

Sio fumbo mfumbie mjinga mwerevu atang’amua ila ni ukweli mchungu kuhusu kilichojiri hata mineso ikapoteza mashiko katika ‘Front’ ya sasa, wakati waliofanya makubwa zamani wapo na walioendeleza mashiko wapo na waliokuja baadaye nao pia wapo ingawa kuna somo moja kubwa kwa hali ilipofikia sasa.

Msingi ni muziki (mtindo) wenyewe ambao ukisimamiwa vyema utaakisi mashiko (utamaduni) wake vyema na kibaya hakitajitembeza kwani chema kitajiuza kutokana na ubora wake, ndivyo alivyofanya Bob Marley kwa kujikita mno kwenye weledi kimuziki na mashiko ya alichokiimba yakasambaa ulimwenguni kote hata kusikotarajiwa kuhusudiwa mikong’osio hiyo.

Dhambi ya ubaguzi kwenye fani hutafuna wanaoitenda na hata wanaotendewa kama ambavyo wengi hawajui kinachoisibu Bongo Reggae, lakini Majemedari (simba wa kale) wamegundua askari mamluki waliojipenyeza kwenye mstari wa mbele wa vita ya kuuinua mtindo huo na kinachofuata sasa ni kurudisha ‘Front’ kwa weledi wa zamani (Back) kwani walipokaa kando waliopokea kijiti hawakujishughulisha kuhimili kuufikia ipasavyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles