29.7 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

BOMOABOMOA YA KARNE

Na MWANDISHI WETU- Sumbawanga

NI bomoa bomoa ya karne. Ndivyo unavyoweza kusema, baada ya Serikali kutangaza kuanza mara moja kutekeleza  bomoa bomoa nchi nzima kwa watu  wote waliojenga bila kibali.

Vilevile imesema itataifisha mara moja ardhi inayotumika kama dhamana bila kuendelezwa.

Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipofanya ziara wilayani Sumbawanga Mkoa wa Rukwa   alikokwenda kutatua mgogoro wa ardhi.

Waziri alisema tatizo la ujenzi holela lianaanza wakurugenzi wa halmashauri, maofisa ardhi, maofisa ujenzi na maofisa mipango miji wanapoacha majengo yanaibuka katika miji yao bila kujua ujenzi husika una kibali au nyumba inajengwa katika kiwanja chenye hati na muhusika wa hati hiyo ndiye anayejenga.

Aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri, maofisa ardhi, maofisa ujenzi na maofisa mipango miji kuweka alama za X na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila kibali na yale yanayojengwa katika viwanja vya watu wengine walio na hati miliki zao za ardhi kwa dhuluma.

“Hatuwezi kuendelea kurasimisha makazi kila siku wakati chanzo cha tatizo hilo kinajulikana.

“Naagiza wakurugenzi, maofisa ardhi, maofisa ujenzi na maofisa mipango miji kuweka X katika majengo yote yanayojengwa bila vibali na ujenzi unaofanywa kwenye viwanja vya watu masikini kwa dhuluma,” alisema Lukuvi.

Alisema atapambana na viongozi hao   atakapokuta majengo yamekithiri katika miji yao na hayana vibali vya ujenzi au yamejengwa katika maeneo ambayo hayaruhusiwi au katika kiwanja cha mtu mwingine.

MASHAMBA

Wakati huohuo, Waziri Lukuvi alisema Serikali inakusudia kuwanyang’anya mashamba watu wote waliokopeshwa na kuyatumia kama dhamana ya kupata mikopo.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakikopa fedha kwenye benki za ndani na nje, lakini mikopo hiyo hawaitumii kuinufaisha nchi wala kuendeleza ardhi waliyotumia kama dhamana.

Lukuvi alisema kumekuwa na changamoto kubwa ya wawekezaji wengi wenye mashamba makubwa kutumia ardhi kama dhamana lakini mikopo hiyo wanaitumia kuwekeza nje ya nchi na kujenga majengo Ulaya, Dubai na kwingineko duniani.

Alisema haiwezekani mtu atumie ardhi kujipatia fedha halafu aendeleze nchi nyingine na kuiacha ardhi kama pori jambo ambalo linaleta migogoro mikubwa katika jamii inayoyazunguka maeneo hayo.

“Wizara yangu imekusudia mwezi ujao kupeleka Bungeni marekebisho ya sheria namba 24 ya mwaka 1999 kuongeza vifungu ambavyo vitadhibiti mikopo inayopatikana kwa kutumia ardhi kama dhamana,” alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha fedha zinazopatikana kutokana na mikopo iliyotolewa itumike kuendeleza sehemu ya ardhi husika iliyotumika kama dhamana ya kuomba mkopo.

Alisema tathmini inaonyesha baadhi ya wawekezaji hao hawazitumii fedha wanazokopa kuendeleza ardhi husika au katika uwekezaji wowote nchini.

Waziri alisema kuanzia mwezi ujao tatizo hilo litakwisha kwa kuwa jukumu hilo zitapewa benki na wakopeshaji wote ambao watafuatilia kwa karibu maombi ya mikopo kutokana na mpango mkakati uliowasilishwa katika benki husika.

“Kama benki husika haitawafuatilia na kuamua kumuachia mtu kuwekeza anavyotaka bila kuendeleza ardhi husika, Serikali itamyang’anya mkopeshwaji shamba kwa kuwa atakuwa amekiuka sheria.

“Na benki ambayo itamuachia mtu achukue fedha bila kuendeleza shamba itakuwa imekula hasara yenyewe,” alisema Lukuvi.

MGOGORO WA ARDHI

Waziri Lukuvi, aliagiza eneo la lililokuwa shamba la mifugo la Malonje wilayani Sumbawanga, lenye ukubwa wa ekari 12,750, lirejeshwe serikalini kwa vile utaratibu wa kuligawa umekiukwa kwa kiwango kikubwa  na masharti ya uendeshaji hayajazingatiwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelote Stephen, alimhakikishia waziri  kuwa atayafanyia kazi mapendekezo yake kwa ukamilifu na kwa haraka kuondoa migogoro na kero zinazoukabili mkoa huo katika masuala yote ya ardhi.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles