25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Bishop Bagume kutoka Marekani awapa somo vijana

ATLANTA, MAREKANI

KUELEKEA kongamano la Bishop & Pastors Fire Conference 2020 litakalofanyika Septemba 22 hadi 26, katika ukumbi wa Triple J Bahari Beach jijini Dar es Salaam, mgeni rasmi kutoka Atlanta, Marekani, Bishop Deusdedit Bagume, amezianika changamoto kadhaa zinazowakumba vijana wa sasa.

Bishop Bagume ni mzaliwa wa Mwanza, Tanzania na kitaaluma ni mwalimu aliyewahi kufanya kazi kama Mratibu wa Elimu maeneo ya Msalato na Miyuji jijini Dodoma kabla hajakwenda Marekani ambako alijikita katika kumtumikia Mungu.

Akizungumza na Swaggaz, Bagume anasema : “Mimi na Mke wangu Margrette tumekuwa wachungaji wa kanisa la Veyula Dodoma kwenye miaka ya 1984 hadi 1994 kisha tukaendelea na huduma Marekani na kujiendeleza elimu ya juu. Tukiwa huku tulifanya kazi ya Mungu sehemu mbalimbali na tukaishia kuwa na huduma mbili.

“Moja ipo Birmingham Alabama inayoitwa Heaven on Earth Apostolic Ministries Inc, hii ni kanisa na nyingine ipo Atlanta Georgia inayoitwa Emmanuel Trustees of Christ Inc ambayo inajishugulisha sana na kusaidia wasio na makazi (homeless). Tunamshukuru Mungu alitupatia watoto watano ambapo mmoja msichana aliishatangulia mbinguni na wanne ni Neema, Gloria, Isaac na Emmanuel na sasa ni watu wazima nao wametuletea wajukuu watano.”

Akizungumzia changamoto zinazowakumba vijana wa kileo, Bishop Bagume anasema: “Changamoto kubwa ni mawazo hafifu kunakowafanya vijana kushindwa kuzamisha maisha yao kwenye mambo ya msingi kiasi cha imani kuonekana si kitu kwa vijana wa kizazi kipya, leo hii kuna vijana wanaochakarika kutafuta maisha, vijana wanaojitoa sadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya mambo ya maisha bila Mungu.

“Kanisa halina budi kuwasaidia vijana kuratibu na kudhibiti matamanio yao pamoja na kuwawezesha kwa kuwapatia nafasi kunahitajika ubunifu unaofumbatwa kwenye wongofu, kuwasaidia kufanya mang’amuzi ya miito yao ndani ya kanisa.”

Aliongeza kwa kutaja sababu za vijana wengi kushindwa kufika kwenye nyumba za ibada ambapo alisema: “Mwamko umekuwa mdogo kwa vijana kwenye nyumba za ibada kwa sababu kanisa kutokidhi haja zao, wanahitaji mafundisho juu ya uhitaji wao wa pesa, ajira, shinikizo la rika, mahusiano, uhusiano nk ili kufanikisha azma hii, vijana wanapaswa kufundwa barabara kwenye misingi ya imani, kanuni na maadili pamoja na ujenzi wa utamaduni wa maisha ya kumpenda Mungu. Kwa kufanya hivi kwa hakika vijana watakuwa ni chemchemi ya furaha kwenye jamii yetu.”

Ikiwa Bishop Bagume asili yake ni Tanzania, Swaggaz lilitaka kufahamu amejipanga vipi kusaidia vijana wa hapa Bongo naye anasema.

“Nilishaanza kusaidia vijana wachache Dar es Salaam, tunawasaidia kuwa na miradi midogo midogo kama wale wanaofanya mapambo kwenye sherehe, kuna wale wamekuwa na saloon zao, zaidi tunatazamia kuwa na kongamano zuri tu ‘online’ la vijana kuwaelimisha zaidi juu ya maswala ya kujikwamua kiroho na kiuchumi.

“Ikumbukwe kwamba imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayomtaka mwamini kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Baba wa milele, bila imani na kujiaminisha kwa Mungu ni kazi bure kuzungumzia tunu ya imani. Mungu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha ya ujana, bila tunu msingi za maisha ya kiutu na kimaadili, ujana si kitu cha kujivunia tena, huu ni mwanzo wa kuchuma majanga kwa familia. Mungu anapenda kuwashirikisha vijana furaha na hatimaye, maisha ya uzima wa milele,” anasema Bishop Bagume.

Aliongeza kwa kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua za kiroho alizozichukua baada ya Dunia kutikishwa na janga la corona.

“Tunamshukuru Mungu kwa kutuletea Rais anayemjua Mungu, hii imekuwa changamoto kubwa hata kwa watumishi wa Mungu. Ukiangalia kwenye maandiko kulikuwa na Mfalme Daudi ambaye alikutana na changamoto nyingi na Mungu akawa ngao yao, ni kweli Mungu ameipigania Tanzania,” anasema.

Aidha Bishop Bagume aliwaomba watumishi wa Mungu wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kwenye kongamano la Bishop & Pastors Fire Conference 2020 kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 11 jioni ambapo litaongozwa na Archbishop Solomon Maganga pia nitakuwa na ziara mwezi Oktoba jijini Dodoma na Mwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles