24.3 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

BENKI YA NMB KUTOA MIKOPO YA NYUMBA

Na FARAJA MASINDE  -DAR ES SALAAM

BENKI ya NMB Plc imetangaza kampeni ya kutoa mikopo ya nyumba kwa Watanzania yenye masharti nafuu itakayodumu hadi Machi 31, mwakani.

Kampeni hiyo ilitangazwa jana Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Omary Mtiga.

Mtiga, alisema kuwa wamefikia hatua ya kutoa mikopo hiyo baada ya kutambua umuhimu wa makazi kwa maisha ya binadamu.

Alisema mikopo huo utakuwa ni wa aina tatu ambapo mtu anaweza kupata hadi Sh milioni 700 huku muda wa kurejesha ukiwa ni hadi miaka 15.

“Tumefikia uamuzi huu wa kutoa mikopo ya nyumba kwa Watanzania kama ambavyo tunatambua umuhimu wa makazi, hivyo kuanzia leo (jana) hadi Machi 31, mwakani tutakuwa tukitoa mikopo ya nyumba yenye masharti nafuu ambayo pia haitakuwa na gharama za uendeshaji.

“Mikopo yetu itakuwa na aina tatu ambapo aina ya kwanza ni ile inayohusisha mteja kununua nyumba yoyote anayoipenda iwe imejengwa na shirika au mtu anauza basi anakuja kwetu tunampa mkopo.

“Pia aina ya pili ni kwa mteja ambaye tayari amejenga nyumba na anahitaji pesa kwa ajili ya kufanya mambo mengine basi akija kwetu tunampa mkopo iwapo tu nyumba hiyo itakuwa na hati na mkopo wa tatu ni kumrahisishia mteja ambaye nyumba yake imefikia hatua ya linta, basi sisi tutakusaidia hadi hatua ya mwisho ambayo ni kupaua, kwani eneo hili limekuwa likiwashinda wengi na hivyo kumfanya mtu ajenge nyumba kwa muda mrefu,” alisema Mtiga.

Katika hatua nyingine, Ally Ngingite ambaye ni Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Wateja Binafsi, alisema ili mtu aweze kupata mkopo huo mbali na nyumba yake kuwa na hatimiliki, anatakiwa kuwasilisha risiti ya mishahara mitatu hata kama haipitii kwenye benki hiyo.

“Jambo jingine iwapo ni mwajiriwa anatakiwa kuambatanisha barua ya mwajiri wake, hivyo mtu yeyote anastahili kupata mkopo huu awe ni mfanyabiashara, Watanzania waishio nje (Diaspora) au mfanyakazi.

“Mkopo huu pia unaweza kuchukuliwa kidogo kidogo ndani ya miaka 15, hivyo mteja ana uhuru wa kuchukua kwa awamu, lakini pia mtu anaruhusiwa kuchukua mkopo na mwenza wake kwa maana rafiki, mke au yeyote yule ambaye wanashirikiana na wanaweza kununua nyumba kokote kule nchini,” alisema Ngingite.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles