32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 1, 2023

Contact us: [email protected]

Bashiru: Waropokaji kutekwa kwa Mo wameumbuka

*Adai walitaka kuomyesha Tanzania si sehemu salama kwa uwekezaji

Na EVANS MAGEGE, Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema kitendo cha mfanyabiashara Mohammed Dewji maarufu kwa jina la Mo kutekwa na watu wasiojulikana na kupatikana wiki iliyopita kiliitia doa kubwa taifa na kupatikana kwake wiki iliyopita kumewaumbua waropokaji ambao ni maadui wa nchi.

Mo alitekwa hivi karibuni katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam mahali alikokuwa anakwenda kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwili (gym).

Akizungumza Dar es Salaama jana muda mfupi baada ya kuwasili nchini akitokea China alikokuwa na ziara ya siku 10 ya kujifunza masuala mbalimbali ya maendeleo na utawala huku akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Dk. Bashiru, alisema  kupatikana kwa Mo baada ya kutelekezwa eneo la Viwanja vya Gymkhana, kumewaumbua maadui wa ndani waliokuwa wameanza kuitumia nafasi ya kupotea kwake kuichafua nchi.

Alisema maadui hao wa ndani walitumia nafasi ya kupotea kwa Dewji kuiingiza nchi katika mgogoro wa kiuchumi ili wawekezaji wapoteze imani ya kuja kuwekeza hapa nchini.

“Ningependa kushukuru vyombo vya ulinzi na usalama na niwapongeze Watanzania  kwa ndugu yetu Dewji kupatikana maana mimi niliacha kizaa zaa hapa lakini nilipokuwa China nikapewa habari kwamba amepatikana.

“Hili lilikuwa ni doa kubwa, kulikuwa na maadui wa ndani walishaanza kuitumia hiyo nafasi kutuchafua na kutuingiza katika mgogoro wa kiuchumi ili wawekezaji wapoteze imani, kwa hiyo wale walioanza kuropoka wameumbuka na mimi nilipokuwa naondoka nilisema masuala ya ulinzi na usalama ni nyeti katika dunia ya sasa, tuyajadili kwa umakini,” alisema.

Pia alisema vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kupongezwa  kwa sababu vinafanya kazi nzuri  kitaifa na kimataifa hivyo havitakiwi kukatishwa tamaa.

Awali kabla ya kuzungumzia suala la Mo, alizungumzia ziara yake ya China na alisema amejifunza mambo manne ambayo ni kichocheo cha maendeleo kwa nchi.

Alitaja mambo hayo kuwa ni mwafaka wa kitaifa kuhusu maendeleo ya nchi, uwekezaji wa maarifa kwa wananchi, mfumo wa kusimamia masuala ya umma pamoja na uwekezaji wa maendeleo ya jamii.

Alisema China imepiga hatua kubwa kimaendeleo kwa sababu tayari wananchi wake wameshajiwekea mwafaka imara juu ya kusimamia maendeleo yao.

Alisema ndani ya mifumo ya nchi hiyo wanamini kuwa kila taifa hilo linapoendelea, mahitaji ya wananchi yanaongezeka hivyo kwa msingi huo wanahangaika kwa kila mbinu kuuondoa umasikini katika jamii.

Pia alisema mfumo wa utawala wa nchi hiyo umewekeza kwa kiasi kikubwa maarifa kwa wananchi.

Alisema licha ya baadhi kupata ujuzi nje ya nchi, kutumia kampuni za kimataifa katika miradi yao ya maendeleo lakini kila hatua wananchi wanashiriki na dhamira hiyo imewasaidia kupata kiwango kikubwa cha wataalaamu wa ndani.

Alisema nchi hiyo ina mfumo mzuri wa kuwatayarisha vijana kuwa wabunifu pia imewekeza zaidi katika mafunzo kwa vitendo.

“Hatua hii inawafanya Wachina waseme kidogo, watende zaidi, wana msemo wa kwamba maneno matupu yazulu nchi,” alisema.

Pia alisema mifumo ya nchi hiyo inajitosheleza kwa kiwango cha wataalamu wanaowahitaji.

Alisema nchi hiyo ina mifumo  madhubuti ya kusimamia masuala ya umma kwa kuweka taratibu bora za kuwajibishana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles