24.8 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

RT waweka mikakati kuelekea Olimpiki 2020

Sulle (kushoto), na Dickson Marwa

NA WINFRIDA MTOI

MWEZI huu umekuwa wa neema kwa wanariadha nchini baada ya kufanya vizuri katika mashindano waliyoshiriki kwa kufanikiwa kurejea nyumbani na medali.

Miongoni mwa wanariadha hao, aliyekuwa gumzo zaidi ni Augustino Sulle kutoka Manyara, aliyefanikiwa kuweka rekodi mpya ya taifa kwa  kuvunja ile aliyokuwa nayo  mwanariadha mkongwe, Juma Ikangaa.

Ikangaa ni kati ya wanariadha waliotamba miaka ya nyuma na kuitangaza vema Tanzania kutokana na kufanya vizuri katika mchezo huo akikimbia mbio za marathoni na kufanikiwa kuchukua medali kupitia michuano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi aliyoshiriki.

Mwaka 1989, Ikangaa aliweka rekodi ya taifa baada ya kufanya vizuri katika mbio za New York Marathon nchini Marekani kwa kumaliza kilomita 42 akitumia saa 2:8:1 na tangu hapo hakuna mwanariadha wa Tanzania aliyewahi kufikia muda huo.

Hata hivyo, ikiwa ni miaka 29 sasa tangu Ikangaa aweke rekodi hiyo ya taifa, wiki hii, mwanariadha Sulle, alifanikiwa kuvunja rekodi hiyo, baada ya kukimbia kilomita 42 kwa saa 2:7:44 katika mbio za Toronto Marathon, nchini Canada.

Muda aliotumia Sulle, pia amempita  kwa dakika mbili mwanariadha mwingine, Alphonce Simbu, ambaye alishika nafasi ya tano katika michezo ya Olimpiki mwaka 2016.

Ushindi huo wa Sulle ulipokewa  kwa furaha kubwa kwa wadau wa riadha na viongozi wa mchezo huo kwa sababu ni muda mrefu wanariadha  wa Tanzania wameshindwa  kuweka rekodi mpya  na kuwafanya baadhi ya wakongwe wa nchini kuendelea kubaki na rekodi zao.

Kutokana na uwezo na muda binafsi aliotumia Sulle, inaonyesha wazi kuna kitu wanariadha wanaanza kukionyesha kwa sababu ni wakati ambao inaelekea  katika michuano ya dunia ikiwamo Olimpiki 2020.

Ushindi wa Sulle umeongeza idadi ya wanariadha wanaoaminiwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali, tofauti na awali jina kubwa lilikuwa la Simbu baada ya kushika namba tano kwenye Olimpiki.

Pia itaongeza hamasa  na morali kwa wanariadha wa Tanzania kufanya vizuri katika mashindano wanayotarajia kushiriki kwa kujiamini na  kuondoa ile hofu ya kushindwa iliyokuwa imetawala kwa muda mrefu.

Tofauti na Sulle, Jumapili wiki iliyopita, tulishuhudia wanariadha saba kati ya wanane Watanzania, walikwenda kushiriki mbio za Nagai Marathon, nchini  Japan, wakifanya vizuri na  kutwaa medali, hali inayoleta matumaini katika kusuka timu ya riadha Olimpiki 2020.

Katika mbio hizo zilizoshirikisha wanariadha 1,000, Marco Joseph, Fabian Joseph na Amina Mohamed, wameibuka na medali za dhahabu.

Marco alishinda katika mbio ndefu kilomita 42 huku Fabian na Amina walishinda mbio fupi kilomita 21, wakati Rosalia Fabian, akishika nafasi ya pili, ya tatu ni Silvia Masatu kwa wanawake na wanaume nafasi ya pili ilikwenda kwa Wilbert Peter.

RT waeleza mikakati yao

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday, anasema wameweka mikakati ya kuhakikisha wanatoa wanariadha walio bora zaidi ili kurudisha heshima ya mchezo huo.

Anasema katika kufanikisha hilo, wamekuja na mpango wa kambi za riadha ambazo zipo Arusha na Manyara, kwa kuwapa nafasi wanariadha wengi kujifua kabla ya kwenda kushiriki mashindano.

Gidabuday anasema kambi moja kati ya hizo inadhaminiwa na DSTV, lakini nyingine wameamua kama viongozi wa RT kuigharamia kwa kushirikiana na wadau wengine.

“Kambi tulizoweka ni kwa ajili ya mashindano yote tutakayoshiriki, hatuangalii Jumuiya ya Madola pekee au Olimpiki, lengo letu ni kutengeneza wanariadha bora kama ulivyoona kwa Sulle,” anasema Gidabuday.

Anafafanua kuwa mafanikio ya Sulle ni baada ya RT kuamua kuwekeza nguvu zao zote katika kutengeneza wanariadha bora na kuwapa nafasi ya kushiriki mashindano mbalimbali kulingana na mialiko inayotokea.

“Hatuangalii mwanariadha mmoja mmoja, tunataka kuwa na kundi kubwa la wanariadha bora, mfano kipindi kile kama tungemwangalia Simbu peke yake kwa sababu kafanya vizuri, leo hii asingekuwepo Sulle.

“Hivyo basi, kwa rekodi mpya ya Sulle, inatupa nguvu sisi viongozi wa shirikisho la riadha kutengeneza wengine na kuandaa timu kuelekea mashindano yanayotukabili na ninaamini medali zitakuja nyingi,” anaeleza.

Aliyataja mashindano makubwa yaliyopo mbele yao ni yale ya dunia yanayotarajia kufanyika Qatar na Olimpiki mwaka 2020.

Katibu huyo amewataka wanariadha kutumia kambi zilizowekwa kujiandaa kwa kujituma  kufanya mazoezi kwa sababu makocha waliopo wana uwezo mkubwa wa kuwafikisha mbali.

“Kambi zetu ni bora na zina makocha wazuri, ni jukumu la wanariadha wenyewe kujituma kufanya mazoezi na kuepuka kuyumbishwa na watu  pamoja na kuzingatia nidhamu kwa sababu katika michezo nidhamu ni moja ya njia ya mafanikio,” anaeleza katibu huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles