27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe: Wazalishaji chanzo cha sukari kupanda bei

Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

SERIKALI imewatuhumu wazalishaji wa sukari nchini (ambao ni wamiliki wa viwanda vya kuzalisha sukari) kwa ‘kutengeneza’ uhaba wa bidhaa hiyo ambayo bei yake imekuwa ikipanda kwa kasi kuanzia mwishoni mwa mwaka jana wa 2023 na kusababisha mzigo mkubwa wa gharama kwa watumiaji wake.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kutokana na uhaba wa sukari nchini uliosababishwa na mvua za el-nino, serikali ilitoa vibali kwa wazalishaji (viwanda) kuagiza sukari kutoka nje ili kufidia nakisi iliyojitokeza, lakini wahusika wameagiza kiasi kidogo sana cha sukari na kusababisha uhaba uliopo sasa.

“Tulitoa vibali vya kuagiza tani 50,000 kwa maana ya tati kumikumi kwa viwanda vitano, lakini walioagiza hizo tani zote 10 ni kiwanda cha Bagamoyo Sugar (Bakhresa) peke yao, wengine hawakuagiza sukari kadri ya vibali walivyopewa, ndiyo maana tunakwenda kubadili sheria ili hawa wazalishaji wasiwe na haki ya kipekee ya kuagiza sukari, bali washindane na waagizaji wengine wa ndani na nje,”amesema Bashe.

Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari, Prof. Kenneth Besegi akitoa ufafanuzi kuhusu uhitaji wa sukari wakati akizungumza na waharir pamoja na waandishi wa Habari katika mkutano uliondaliwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam leo Februari 22,2024.

Amesema kitendo cha wazalishaji hao kushindwa kuingiza tani za sukari kulingana na kiwango walichopewa, ndiyo sababu ya Serikali iliamua kuingilia kati na kuamua kutumia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuingiza sukari kutoka nje ya nchi ikishirikiana na kampuni walizoingia nayo makubaliano.

Mbali na Bagamoyo Sugar, Bashe ametaja viwanda vingine ambavyo vilipewa kibali cha kuingiza sukari kuwa ni Kagera Sugar, TPC, Kilombero na Mtibwa Sugar ambacho kimeagiza tani mbili za sukari ambayo iko kwenye mchakato wa kushushwa bandarini.

Waziri Bashe ametaja changamoto nyingine kuwa ni mtandao wa usambazaji wa wazalishaji hao, kwani wana mawakala wachache sana kiasi cha kuathiri usambazaji wa sukari. “Mfano Kagera Sugar wana wakala mkubwa mmoja tu ambaye yuko Mwanza ambaye anasambaza sukari kwenye mikoa 11 ukiwamo mkoa wa Kagera.

Amesema katika muktadha huo, wakazi wa Kagera hupokea sukari kutoka Mwanza ambayo huwa imesafirishwa kutoka kutoka mkoani humo hivyo kuongeza gharama zisizo za lazima. Kutokana na hali hiyo amesema Serikali imewapelekea waraka wenye viwanda ili wabadilishe mifumo ya usambazaji na kuhakikisha kila kiwanda kina kituo cha usambazaji kila mkoa.

“Wafanyabiashara wana ‘option’ mbili tu, waache kuuza sukari, serikali itatafuta ‘option’ nyingine wenye viwanda wana’option’ mbili tu, kufuata utaratibu wa Serikali hawawezi waache, na tumewapelekea walaka wa kubadilisgha mfumo wa usambazaji. Haiwezekani mfano Kagera Sugar ana msambazaji mmoja yupo Mwanza anahudumia mikoa 11,”amesema.

Kuhusu hali ya sukati, Bashe amesema: “Mwaka huu tulitarajia kufika uzalishaji wa tani 550,000, TMA walitoa hali ya mvua itakavyokuwa. Mwezi wa 10 tukaanza ‘preparation’ (maandalizi) kwa ajili ya kuruhusu uingizaji wa sukari ya nje, tukatoa vibali vya kiwango kisichopungua tani 100,000 na mpaka sasa sukari iliyopo bandarini na iliyoanza kusambazwa ni wastani wa tani kama 31,000.

“Hivi sasa tunavyoongea kuna meli ya tani kama 25,000 inashusha sukari na mwaka huu tutaingiza jumla ya tani 300,000 na kufikia Marchi 15, 2024, tutakuwa tumeingiza tani zisizopungua 60,000 ili kukabiliana na upungufu wa sukari.”

Waziri Bashe alikuwa akizungumza leo Februari 22, 2024, Ikulu Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Wahariri, Waandishi wa Habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Raisi, Ikulu, kuelezea yaliyojiri katika ziara ya Raisi Dk. Samia Suluhu Hassan katika nchi za Vatican, Norway pamoja na Ethiopia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles