23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu Rwabutikula atoa darasa la corona kwa wachungaji, waumini

Nyemo Malecela – Kagera

ASKOFU wa Kanisa la Calvary Assemblies of God (CAG) jimbo la Kagera, Damian Rwabutikula amewataka wachungaji mkoani humo kuwafundisha na kuwasimamia waumini wao jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa corona.

Askofu Rwabutikula ametoa wito huo katika ibada ya kuwasimika wachungaji wa kanisa hilo waliomaliza elimu ya Diploma na Viongozi wa vijana wa jimbo hilo, iliyofanyika katika Kanisa la Chonyonyo lililopo wilayani Karagwe mkoani Kagera.

Alisema wachungaji hao wanatakiwa kuzingatia masharti na maelekezo ya wataalamu wa afya katika utendaji wao wa kutoa huduma za kichungaji kwani wilaya hiyo iko mpakani, hivyo wana hatari ya kupata waumini wageni kutoka nchi jirani ambako ndiko ugonjwa wa corona unatajwa kushamiri zaidi.

“Mpeleke elimu sahihi kwa waumini wenu, waelimisheni na kuwaelekeza jinsi ya kujikinga na corona, ugonjwa huu upo na unaua, wafundisheni umuhimu wa kuvaa barakoa na kuweka vibuyu chirizi vyenye maji tiririka pamoja na sabuni na kunawa mikoni mara kwa mara ili kujikinga na ugonjwa huo.

“Fuateni masharti na maelekezo ya wataalam wa afya, kwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kupunguza msongamano kanisani, kwa kuwapanga waumini katika mpangilio unawapa nafasi ya kutosha kati ya muumini mmoja na mwenzake,” alisisitiza.

Katika ibada hiyo iliyowashirikisha maaskofu kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Arusha na Kagera, wachungaji, viongozi na waumini kutoka Wilaya ya Ngara, Karagwe, Kyerwa, Muleba na Misenyi walifuata taratibu zinazoelekezwa na wataalamu wa afya kwa kukaa katika umbali ili kuepuka msongamano.

“Natamani Mungu aendelee kuwainua viongozi wengine ambao watawajenga kiroho wananchi waweze kujiamini katika mapambano dhidi ya kinga ya ugonjwa wa Corona kama alivyokuwa akifanya Hayati Dk.John Magufuli ambapo aliwatia moyo wananchi kwa kuwataka wamuamini Mungu.

“Wananchi wanatakiwa kuacha woga yanapotokea majanga katika jamii, kwa kuwa woga unasababisha kufanya maamuzi yasiyo sahihi, badala yake wanatakiwa kufuata maelekezo wanayopatiwa na watawala wakati huo wakiendelea kumuomba Mungu,” amesema.

Askofu Rwabutikula alisema wachungaji wanatakiwa kusimama katika uongozi na kuangalia aliyewaita siyo kufuata wanadamu wanataka nini na wakikutana na changamoto hautakiwi kupambana nao bali waongeze nguvu katika uwajibikaji na maombi.

Naye Katibu wa kanisa hilo Mkoa wa Kagera, Mchungaji Agnes Charles amewataka wachungaji wawe na utamaduni wa kujiendeleza kielimu kwa kushiriki mafunzo mbalimbali ya uongozi ili kujikumbusha miiko na maadili katika kazi yao.

“Mnatakiwa kujiongezea upeo kwa kushiriki mafunzo mbalimbali ya uongozi yatakayowasaidia kuongeza nguvu katika maombi, kujielewa, kuelewa nani aliyewaita katika huduma na msiangalie upinzani unaowakabili katika kazi zenu na badala yake muongeze jitihada na ubunifu katika kazi ili muweze kuendana na wakati tulionao sasa,” alisema Agnes.

Wakati huo Katibu Msaidizi wa kanisa la The Love of Calvary Church kutoka Arusha, Mwalimu Lodrick Daffa alisema wachungaji wanatakiwa kuwa na maono, mpangilio katika utendaji wa kazi zao, nidhamu, mawasiliano na uhusiano katika utendaji wa kazi.

“Endapo viongozi wakiwemo wachungaji watafuata mambo hayo itawasaidia kufanana na nafasi zao wanazoziongoza pamoja na kuwa na maono na kuweka kumbukumbu katika jamii ambayo wanaiongoza,” alisema.

Pia Katibu Msaidizi wa Kanda ya Mashariki (C.A.G), Askofu Amos Peter kutoka jijini Dar es Salaam amewaonya wachungaji kuacha tabia ya kushabikia kitu chochote kinachoipinga serikali kwani itawapunguzia hali ya kuaminiwa na serikali na jamii kwa ujumla.

“Wachungaji ni watu wa kuaminiwa tangu enzi, ni kioo cha jamii na ili uaminiwe na kuheshimiwa na unaowaongoza inatakiwa kutengeneza imani kwa serikali ili taifa linapohitaji majibu liyapate kutoka kwao,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles