20.5 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

ASILIMIA 70 WANAOUGUA SELIMUNDU HUFARIKI KABLA MIAKA MITANO

 

 

NA VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM

ASILIMIA 70 ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa wa selimundu (sickle cell) nchini, hufariki dunia kabla hawajafikisha umri wa miaka mitano.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na daktari bingwa wa selimundu, Dk. Deogratius Soka, alipozungumza na waandishi wa habari.

Dk. Soka ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Selimundu (TANSCDA), alisema hali hiyo inatokana na watoto wengi kutotambulika mapema na kupewa matibabu sahihi.

“Tafiti zinaonyesha asilimia 15 ya Watanzania wana uwezekano wa kuzaa watoto wenye selimundu kwa sababu wana vinasaba vya ugonjwa huu,” alisema.

Pia alisema uelewa wa watu kujitokeza mapema kupima iwapo wana vinasaba hivyo kabla ya kuamua kuzaa watoto bado ni mdogo na kusababisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo kuwa duni.

“Ili mtoto azaliwe na ugonjwa, lazima baba na mama yake wote wawili wawe na vinasaba hivi, sasa mkipima mapema ikagundulika mna vinasaba, mtafanya uamuzi sahihi iwapo mzae watoto au la, na ikiwa mtazaa mtoto mwenye selimundu kwa kuwa amegundulika mapema atapewa tiba sahihi,” alisema.

Alitaja mikoa yenye wagonjwa wengi wa selimundu kuwa ni Kagera, Mara, Shinyanga, Kigoma, Geita, Pwani, Tanga, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.

“Lakini si kwamba katika mikoa mingine hakuna ugonjwa huu, bali upo kwa kiwango cha chini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles