27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 1, 2024

Contact us: [email protected]

Asasi ya Agenda yabainisha madhara ya kemikali zilizopo kwenye Plastiki

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojiunga katika kupunguza matumizi ya plastiki kama njia mojawapo ya kutunza na kuhifadhi mazingira.

Katika kutekeleza suala hilo Juni mosi mwaka 2019 Tanzania ilitangaza marufuku ya kutengeneza, kusambaza, kutumia au kutunza mifuko ya plastiki.

Katazo hili lilifuatia tangazo lililotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira kwa wakati huo, January Makamba na kwamba hatua hiyo ni utekelezaji wa kifungu cha 230 (2)(f) ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.

Licha ya kuwepo kwa sheria hizo lakini usimamizi na utekelezaji umekuwa wa kusuasua, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Asasi ya AGENDA inayojihusisha na masuala ya Mazingira na Maendeleo nchini mwaka 2020.

Utafiti huo ulibaini kuwa plastiki zilizorejelezwa (recycled plastic pellets) zina kemikali zaidi ya 500 zikijumuisha kemikali zinazotumika kwenye viuatilifu, mafuta ya transfoma (PCBs), kemikali za viwandani pamoja na kemikali nyingine hatarishi.

Mfano, sampuli moja ya plastiki ilikutwa na kemikali 6 za brominated flame retardants (kuzuia moto kuwaka), UV stabilizers (Kupunguza nguvu ya mionzi) nne, na moja  ya Bisphenol A.

Akizungumza Dar es Salaam leo Aprili 18, 2024 kuhusu hali ya matumizi ya plastiki nchini na athari za mazingira zinazojitokeza, Katibu Mtendaji wa Asasi ya AGENDA, Dorah Swai, amesema utafiti uliofanywa hivi karibuni katika nchi 13 duniani ikiwemo Tanzania umeonesha kuwa  plastiki zinazorejelezwa zinaweza kuwa na masalia ya kemikali hatarishi.

Akitolea mfano vifungashio vya kuhifadhia viuatilifu vikirejelezwa, sumu za kemikali hizo zitaishia kwenye bidhaa zitakazorejelezwa na kuzalisha kemikali mpya ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira yake. 

“Ni muhimu wakati huu kuwa na wawakilishi wa Serikali kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania kushiriki mkutano wa majadiliano ya kuwa na Mkataba wa Kimataifa wa kusimamia plastiki utakaofanyika wiki ijayo jijini Ottawa nchini Canada ili kutoa mapendekezo ya kupunguza matatizo yanayotokana na matumizi ya plastiki kwa kutumia njia ya urejelezwaji,” amesema Dorah.

Akifafanua zaidi kuhusu madhara ya kemikali zilizopo kwenye plastiki, amesema zinachangia maradhi ya saratani (kansa), matatizo ya moyo, matatizo  katika mfumo wa uzazi, kisukari, unene uliopitiliza pamoja na shida nyingine za kiafya.

Kwa upande wake Afisa Programu Mkuu wa Asasi ya Agenda, Silvani Mng’anya amesema plastiki zinatengenezwa na kemikali hatarishi, hivyo plastiki hizo zinaporejelezwa, kemikali zilizopo hubakia kwenye bidhaa.

Mng’anya amesema ili kudhibiti matumizi ya plastiki kunahitajika kuwepo na mkataba bora wa plastiki wenye kulinda afya za watu pamoja na mazingira kutokana na kemikali hatarishi zilizopo kwenye plastiki na kudhibiti uzalishaji wake.

“Katika utafiti wetu tulioufanya mwaka 2020, Agenda tulichukua sampuli za chenga chenga za plastiki (recycled plastic pellets) kutoka kwenye viwanda vya kurejeleza plastiki na kuzifanyia tathmini ya kubaini uwepo wa kemikali hatarishi.

“Hata hivyo, tafiti nyingi zilizopita zinaonesha kuwa plastiki zilizorejelezwa ni sehemu ya usambaaji wa kemikali hatarishi kwa sababu zimeundwa kwa kemikali zaidi ya 16,000 na zaidi ya asilimia 25 zinafahamika kama ni kemikali hatarishi na kwa kemikali zilizobakia taarifa za madhara yake kwa afya ya binadamu na mazingira bado hazijatambulika,” amesema Mng’anya.

Mapungufu katika usimamizi

Afisa huyo amefafanua zaidi kuwa bado kuna mapungufu katika usimamizi na udhibiti wa matumizi ya plastiki ikiwemo kutokuwepo kwa  matakwa ya kimataifa ya kusimamia kemikali zilizopo kwenye plastiki zilizorejelezwa, uwekaji wazi wa taarifa za viambata au kemikali zilizopo kwenye bidhaa za plastiki zilizorejelezwa.

“Hii ina maana kwamba, usambaaji wa kemikali kutoka kwenye plastiki zilizorejelezwa kwa sasa hauwezi kufuatiliwa na kudhibitiwa, udhibiti wa kimataifa unahitajika ili kudhibiti biashara ya kimataifa ya kemikali, plastiki na taka za plastiki,” amesema mtaalamu huyo.

Ameongeza kuwa uwepo wa bidhaa hizo unasababisha uwepo wa majanga makubwa matatu duniani ambayo ni mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bayonuai na uchafuzi wa mazingira unaotokana na vitu mbalimbali ikiwamo plastiki ambayo hii inaunganisha majanga yote matatu.

“Mfano upotevu wa bayonuai unatokana kwamba bidhaa hizi za plastiki haiozi mapema, hivyo mkutano huu utakaofanyika Canada unapaswa kudhibiti plastiki kwa upana wake kwani ni sehemu ya kuelezea kwa nini plastiki zina madhara,” amesema Mng’anya na kuongeza kuwa:

“Ni wakati wa kuangalia kwamba plastiki zina changamoto gani katika nyanja ya kiuchumi, kimazingira na kijamii kwa maana ya afya.

Hivyo kwa kuzingatia majibu ya utafiti ambao umeshafanyika, ni muhimu Serikali yetu kuunga mkono umuhimu wa mkataba huo kwa kuangalia pande zote za uchumi na madhara yake, kwani kama plastik inaathiri afya ni ngumu kuweza kupambana kiuchumi,” amesema Mng’anya.

Thamani ya Plastiki iliyoingizwa nchini pamoja na bidhaa zake kwa mwaka 2022/2023 ilikuwa ni sh trilioni 1.678 taarifa hii ni kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania BoT.

Ni ongezeko la asilimia 72  ikilinganishwa na mwaka 2020/2022 ambapo ilikuwa Sh trilioni 1.833 na asilimia 57 kwa kiasi cha Sh trilioni 1.006 ya mwaka 2019/2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles