24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Armenia na Azerbaijan zalaumiana

YEREVAN, ARMENIA

MUDA  mchache baada ya Armenia na Azerbaijan kukubaliana kusitisha mapigano, vikosi vya nchi hizo mbili vimetupiana lawama ya mashambulizi mapya siku ya Jumamosi mnamo wakati usitishaji mapigano ukianza kutekelezwa.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Armenia Shushan Stepanyan amesema ” kwa kupuuza makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyotangazwa awali, vikosi vya Azerbaijan vimeanzisha mashambulizi kuelekea Karakhanbeyli” eneo linaloongoza kwa makabiliano.

Dakika 30 kabla ya kuanza makubaliano ya kusitisha mapigano wizara ya ulinzi ya Azerbaijan nayo imeripoti kuwa vikosi vya Armenia vimezishambulia wilaya za Terter na Agdam. 

Katika taarifa wizara yake ya ulinzi imesema “Armenia inakiuka waziwazi usitishaji mapigano”.

Pande zote mbili zilikubaliana kutekeleza usitishaji mapigano kuanzia Jumamosi mchana baada ya saa 11 za mazungumzo mjini Moscow. 

Eneo hilo la Karabakh lilijitenga kutoka Azerbaijan katika miaka ya tisini katika vita iliyosababisha mauaji ya watu 30,000.

Serikali yake ina uungwaji mkono mkubwa kutoka taifa la Armenia, ambalo kama Azerbaijan lilipata uhuru baada ya kuanguka kwa Muungano wa kisovieti mwaka 1991.

Mashambulizi makali yaliibuka tena Septemba 27 mwaka huu, na kusababisha watu zaidi ya 450 kuuwawa, maelfu kulazimika kuyakimbia makaazi yao na hofu kwamba mapigano hayo yanaweza kuongezeka na kugeuka kuwa mzozo mkubwa.

Mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP mjini  Stepanakert  ameripoti kusikia milipuko katika mji huo mkuu wa jimbo la Nagorno-Karabakh muda mchache kabla ya muda wa kuanza utekelezaji wa usitishaji mapigano. 

Ingawa hadi kufikia mchana hali ilikuwa tulivu, milipuko kadhaa ilikuwa ikisikika kwa mbali. 

Baadhi ya raia wa mji huo wameshuhudiwa wakitoka majumbani mwao baada ya siku kadha za kujilinda dhidi ya mashambulizi ya mabomu, roketi na ndege zisizokuwa na rubani

Makubaliano ya kusitisha mapigano yametangazwa baada ya mazungumzo ya wanadiplomasia wa nchi hizo mbili chini ya usuluhishi wa waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov. 

Lavrov ametangaza kuwa usitishaji huo umefikiwa kwa kuzingatia “misingi ya kibinadaamu” na utaruhusu mataifa hayo kubadilishana wafungwa na miili ya waliouwawa. Pia amesema Armenia na Azerbaijan zimeafikiana  juu ya “mazungumzo makubwa” ya kusuluhisha mgogoro juu ya jimbo la Karabakh, huku Ufaransa, Urusi na Marekani zikiendelea na juhudi za muda mrefu za usuluhishi.

Ufaransa kwa upande wake imeyakaribisha makubaliano hayo, lakini ikisema yanapaswa kutekelezwa kikamilifu na kuhakikisha kuna mazingira ya kumaliza uhasama huo. Wizara ya mambo ya kigeni ya Ufaransa kupitia msemaji wake Agnes von der Muhll imesema  “lazima sasa yatekelezwe na yazingatiwe vizuri ili kuunda mazingira ya ukomeshaji wa kudumu wa uhasama kati ya nchi hizi mbili, “

Hatua ya jimbo hilo kujitangazia uhuru wake yenyewe, haijatambuliwa na nchi yoyote ikiwemo Armenia ingawa Jumuiya ya kimataifa inalichukulia kuwa sehemu ya Azerbaijan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles