MATUMAINI ya kocha wa timu ya Arsenal, Arsene Wenger, kumtumia Alexis Sanchez katika michuano ya FA kwenye mchezo dhidi ya Sunderland yameyeyuka kutokana na hali ya kiafya inayomsumbua mchezaji huyo.
Hivyo hali hiyo huenda ikasababisha kuchelewa hata kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool unaotarajiwa kuchezwa wiki ijayo, ingawa itakuwa tofauti na matarajio ya kocha wa timu hiyo.
Wenger alihitaji kumjumuhisha mchezaji huyo katika wachezaji wa akiba watakaoanza kucheza Kombe la FA lakini alipata tahadhari hiyo wakati alipojaribu kumpa mazoezi ya nguvu mchezaji huyo na kuonekana kutofanya vizuri.
Kufuatia hali hiyo, kocha huyo alikiri kupata wasiwasi wa kumtumia kutokana na majeruhi ya nyama za paja.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, alijitonesha alipokuwa akijaribu kurudi kwa ushindi katika mchezo dhidi Manchester City mwezi uliopita.