Na SAM BAHARI-SHINYANGA
MAGONJWA ya mlipuko yanayotokea nchini yanatajwa kuwa yanatoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kwa asilimia 78, sehemu kubwa ya jamii bado haielewi maambukizi yake yanavyotokea.
Baadhi ya watu waliohojiwa na gazeti hili kwa nyakati tofauti mjini hapa, walisema magonjwa ya mlipuko mengi hawayajui na wala hawajui namna ya kujikinga na magonjwa hayo.
Mkazi wa Kitongoji cha Kitangili, Neema Shabani alisema anayafahamu magonjwa ya mlipuko aina tatu, kuwa ni kipindupindu, kuhara na corona.
Alisema pamoja na kuyafahamu magonjwa machache, anafahamu njia kuu ya kujihami ni usafi wa mazingira, kuchemsha maji ya kunawa na ya kunywa.
“Njia kuu tunayotumia sisi kujihami na magonjwa ya mlipuko ni kujitahidi kufanya usafi wa mazingira na kuchemsha maji ya kunawa, pamoja na ya kunywa,” alisema.
Aliishauri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoa elimu kwa wananchi kutambua magonjwa ya mlipuko, kuchukua tahadhali na namna ya kujikinga na magonjwa hayo.
Mkazi wa Majengo Mapya, Joseph Leo alisema Watanzania wengi hawayajui magonjwa ya mlipuko na ndiyo maana huwa wanapata wakati mgumu hata kuyataja.
Alisema pamoja na jamii kutofahamu magonjwa ya mlipuko,pia haifahamu njia sahihi za kujikinga na magonjwa hayo.
Alisema binadamu ni watu wa ajabu kwa sababu hupuuza masharti ya kujihami na magonjwa ya mlipuko isipokuwa wanapoandamwa na magonjwa hayo ndipo huzingatia kanuni na Masharti ya kujihami na magonjwa.
Dk. Elliyson Maeja alikiri baadhi ya wanyama wanaofugwa na binadamu husababisha magonjwa ya mlipuko ambayo hutokea kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Alisema wanyama wengi wanaofugwa na wachache wasiofugwa husababisha magonjwa ambayo husambazwa na wanyama kwa kasi kwenda kwa binadamu na kuathiri uchumi wa mtu moja moja na taifa kwa jumla.
Akiwataja wanyama wanaofugwa na magonjwa wanayoyasababisha kwenye mabano, kuwa ni nguruwe ambao husababisha magonjwa ya (tegu na minyoo),mbwa husababisha ugonjwa wa (Kichaa cha Umbwa).
Wengine ni pamoja na paka husababisha (Corona—Covid-19) na panya husababisha ugonjwa wa (tauni) na sokwe husababisha ugonjwa wa (Ebola).
Aliwataja ndege ambao husababisha ugonjwa wa (mafua ya ndege) na ngozi ya ng’ombe ambayo husababisha (kimeta) na maziwa ya ng’ombe husababisha ugonjwa wa (kifua kikuu).
Mtaalamu wa masuala ya afya ya jamii mjini hapa, Dk Onesmo Mwegoha alisema ingawa kuna magonjwa mengine ya kuambukizwa lakini ya Mlipuko ni hatari zaidi.
Alisema kwa bahati mbaya wakati mwingine baadhi ya binadamu huamua kufuga wanyama wa porini kwa makusudi na kulazimika wanyama hao kuchangamana na binadamu kwa kiasi kikubwa.
“Ninaamini kuwa baadhi ya watu tumewashuhudia na kujionea baadhi ya binadamu wakifuga wanyama kama tumbili, nyatimaji, swala na dondoro,” alisema.