Na SHEILA KATIKULA-MWANZA
BAADHI ya wananchi wameelezea jinsi walivyojifunza mambo mbalimbali kwenye uongozi wa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa alipokuwa madarakani mwaka 1995-2005.
Akizungumza na MTANZANIA, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Pamba, Jonas Mugisha, alisema alijifuza utandawazi, kujiamini na kuwa mbunifu kwa kutengeneza kitu kitakachoweza kuzalisha na kuokoa maisha yake.
“Katika utandawazi alionyesha kuwa watu watakavyoweza kutengeneza vikundi na makapuni ya wazalendo, wito wangu kwa vijana wanaotaka uongozi watambue kuwa lazima wawe na hekima na busara na kutambua unaenda kufanya nini kitakacholeta maendeleo kwenye nchi na dunia,” alisema Mugisha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Wote Sawa linalojishughulisha na kutetea haki za wafanyakazi wa majumbani, Angela Benedicto, alisema amejifunza kuwa kiongozi mkubwa anatengenezwa kwa muda mrefu.
“Nilijifunza mambo kutoka kwake alipozungumzia kwenye taarifa zake kuhusu kufanya utafiti katika mambo mbalimbali na kushirikisha viongozi wengine, unapotaka kufanya kitu lazima uwe na ujuzi na maarifa zaidi juu ya jambo unalotaka kulifanya, hata unapotaka kushirikisha watu uonekane una maarifa zaidi yao na utakapoliwasilisha kubali watu kulipokea au kulikataa,” alisema Benedicto.
Naye Meneja wa Shule ya Msingi Tulele, Hussen Magera alisema alipokea taarifa za kifo cha Mkapa kwa masikitiko kwa sababu katika kipindi cha uongozi wake alichochea kuweka mazingira mazuri kwenye sekta ya elimu kwa kuanzisha shule za kata nchini na kusimamia ufundishaji na usomaji kwa watoto.
“Katika uongozi wake alileta mapinduzi makubwa kwenye elimu kwa kuanzisha shule za kata zilizojengwa kila sehemu akiwa na lengo kila Mtanzania mwenye sifa apate elimu.
“Japo watu wengi walidhani zitakwama, lakini alisimama imara hadi leo zipo, hii ni kwa sababu aliweka mazingira mazuri, hadi hivi sasa zinafanya vizuri kama za binafsi kuanzia msingi hadi sekondari,” alisema Magera.
Aidha Meneja Msaidizi wa Shule za Msabe za jijini hapa, Nicolaus Laurent alisema atamkumbuka Rais Mkapa kwa sababu alimfanya akapenda kusoma masomo ya fasihi.
“Nina imani mwaka huu wanafunzi wa masomo ya ‘arts’ watafanya vizuri kwa sababu wamesikiliza historia ya hayati Mkapa na kutambua kuwa siyo kila kiongozi lazima awe amesoma sayansi,” alisema Laurent.