Kigali, Rwanda
BAADA ya ugonjwa wa Ebola kuripotiwa katika nchi za Afrika Magharibi sasa umebisha hodi katika nchi za Afrika Mashariki.
Kwa mara ya kwanza mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa huo hatari amegundulika Rwanda na tayari amewekwa kwenye sehemu maalumu kwa uchunguzi wa madaktari kubaini kama ana virusi vya ugonjwa huo.
Wakati ugonjwa huo ukiingia Rwanda, nchini Tanzania hali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam inaonyesha hakuna udhibiti wa aina yoyote kama ilivyoahidiwa na Serikali.
Mgonjwa aliyegundulika Rwanda ambaye ni raia wa Ujerumani aliingia nchini humo akitokea Liberia ambako ugonjwa huo sasa umekwishakuua mamia ya watu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi usiku na Waziri wa Afya wa Rwanda, Agnes Binagwaho, mgonjwa huyo ni mwanafunzi wa udaktari.
Alisema mwanafunzi huyo alibainika kuwa na dalili za virusi vya ugonjwa huo, hali iliyowalazimu madaktari kumkimbiza katika Hospitali ya King Faisoil na kulazimika kuchukuliwa vipimo.
Mbali na hatua hiyo, pia madaktari wanaotoa huduma kwa mgonjwa huyo wamewekwa katika eneo maalumu kwa ajili kufanyiwa uchunguzi.
“Mbali na madaktari wanaotoa huduma kuwekwa katika eneo maalumu, hata watu ambao walikuwa wanamsogelea nao wanafanyiwa uchunguzi wakiwa katika chumba maalumu,” alisema Waziri Binagwaho.
Hata hivyo, Ubalozi wa Ujerumani nchini Rwanda umesema kwa sasa hauwezi kuzungumzia suala hilo hadi uchunguzi utakapokamilika.
Dk. Seif alonga
Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alisema Serikali inafikiria kuviwekea viwanja vya ndege mashine maalumu zinazojulikana kama ‘Thermos Canners’, ambazo zina uwezo wa kutambua joto kwa waathirika wa Ebola.
Lakini alisema kukosekana kwa kifaa hicho, haimaanishi kwamba kutaathiri udhibiti uliowekwa na serikali.
“Tumekuwa tukiuchukulia ugonjwa huu kwa uzito wa hali ya juu tangu ulipobainika kuingia katika nchi za Afrika Magharibi, kwa sababu wizara imekuwa ikiushughulikia kama vile uko Uganda, Rwanda, Burundi au Kenya,” alisema.
Dk. Seif alisema hivi sasa uwezo wa kusimamia mipaka umeongezwa kwa kutengeneza vyumba maalumu kwa ajili ya wagonjwa wanaohisiwa kuwa na maradhi hayo, ikiwamo kuwapatia wahudumu wa afya sare maalumu za kujikinga wakati wa kuwahudumia waathirika.
Alizitaja njia nyingine kuwa ni kuwachunguza wasafiri wote wanaohitaji kuingia nchini siku 21 kabla ya kuanza safari, kubaini sehemu walizotoka kama zina maambukizi ya Ebola.
Njia nyingine zinazotumiwa kudhibiti ugonjwa huo ni kushirikiana na wizara nyingine kama Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Fedha, ambazo kwa pamoja zitaweka mikakati madhubuti ya kupambana kuhakikisha ugonjwa huo haupati upenyo kuingia nchini.
Uongozi wa Uwanja Ndege
Kutokana na hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo, MTANZANIA ilifika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na kushuhudia kwamba hakuna chumba chochote kilichotengwa kwa ajili ya uchunguzi, hasa kwa abiria wanaotoka Afrika Magharibi.
Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Moses Malaki, alisema Mamlaka ya Viwanja wa Ndege Tanzania (TAA) inashirikiana na wadau mbalimbali kudhibiti ugonjwa huo.
Alisema wadau hao wamekuwa wakikutana mara kwa mara kwa ajili ya kuangalia namna ya kudhibiti ugonjwa huo pamoja na mafua ya ndege.
“Sisi kazi yetu ni kusimamia usalama wa abiria wakati wa kupanda na kushuka ndege, lakini masuala mengine yanasimamiwa na Wizara ya Afya,” alisema Malaki.
Ndege zakwepa kutua Afrika Magharibi
Shirika la Ndege la Emirates limetangaza kusimamisha kwa muda safari za ndege za kwenda Guinea tangu Agosti 2 mwaka huu kwa sababu ya ugonjwa wa Ebola ambao umeua zaidi ya watu 1,000 katika nchi za Afrika magharibi.
Katika tovuti yake, Emirates limesema haliwezi kuwaweka hatarini abiria na wafanyakazi wake.
Wiki iliyopita Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Margaret Chan, alisema virusi vya Ebola vinatapakaa haraka zaidi kushinda juhudi za kuvidhibiti.
Homa ya Ebola ilianza Guinea na kutapakaa nchi jirani za Sierra Leone na Liberia. Mashirika mawili ya ndege ya Afrika ya Arik Air la Nigeria na ASKY ya Togo yamekwisha kutangaza kuvunja safari za kwenda nchi zilizoathirika.
Zambia nayo imepiga marufuku kuingia nchini humo watu wote wanaotoka Afrika Magharibi kama njia ya kudhibiti Ebola.
Waziri wa Afya wa Zambia, Joseph Katema, alisema raia wote wa nchi hiyo na wageni waliomo nchini humo wenye lengo la kusafiri kwenda nchi zilizoathiriwa na Ebola, safari zote zimesimamishwa hadi itakapotangazwa tena.
“Watu wote kutoka sehemu yoyote ya nchi walioathirika na virusi vya Ebola wanazuiwa kuingia Zambia hadi itakapotangazwa tena,” alisema Waziri Katema.
Virusi vya ugonjwa huo vilianza kugunduliwa mwaka 1976 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Zaire) na kuua mamia ya wananchi.
Madhara yake yalizua hofu kwa familia ambayo ingepata mgonjwa wa Ebola kutokana na kuelewa moja kwa moja kuwa uwezekano wa mgonjwa kupona ni asilimia 10 tu.
Tangu wakati huo, wanasayansi wamekuwa wakitafuta njia za kutibu maambukizi ya ugonjwa huo au kuuzuia usitokee.
Ingawa yamekuwapo mafanikio ya kuutibu, lakini uhakika ulitolewa Mei 28 mwaka huu wakati Jarida la Lancet la Uingereza lilipoeleza matokeo ya watafiti juu ya kupatikana dawa ya kutibu Ebola kwa asilimia 100.