23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri anusurika kipigo

Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi

NA SAMWEL MWANGA, SIMIYU

NAIBU Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi, amenusurika kupata kipigo kutoka kwa wakulima wa pamba katika Kijiji cha Marekano, Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu.

Zambi alinusurika kupata kipigo baada ya kushindwa kutoa majibu ya kuridhisha kwa wakulima juu ya mbegu za pamba zisizoota.

Tukio hilo lilitokea juzi kijijini hapo, wakati Zambi alipofanya ziara ya kushitukiza ili kuona jinsi ununuzi wa pamba unavyofanyika. Pia alitaka kufahamu aina ya mizani inayotumika kununulia zao hilo.

Awali baada ya kufika kijijini hapo, wakulima walikusanyika na kuanza kumuuliza maswali, wakitaka awaeleze ni kwanini Serikali iliwalazimisha kutumia mbegu ambazo hazikuota.

Pamoja na kutaka kujua juu ya suala hilo, pia wananchi hao walitaka kujua kama Serikali itawafidia wakulima waliopanda mbegu hizo na kupata hasara.

Jambo jingine walilomuuliza ni juu ya mizani ya kupimia pamba, kwani walitaka awaeleze hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuwadhibiti wafanyabiashara wanaowaibia wakulima kwa kutumia mizani ya dijitali.

Wananchi hao walipomaliza kuuliza maswali kwa nyakati tofauti, ulifika wakati wa Zambi kuanza kutoa majibu kwa niaba ya Serikali.

Wakati akiendelea kujibu, wananchi walikuja juu na kuanza kumzomea, huku baadhi wakitishia kumpiga kwa kuwa hawakuridhishwa na majibu aliyotoa.

Kutokana na hasira walizokuwa nazo, baadhi ya wananchi walimtaka Zambi aondoke kijijini hapo kwa kile walichodai kuwa Serikali imeshindwa kuendeleza zao la pamba.

Pamoja na hao, wengine walimtaka akaifute Bodi ya Pamba kwa kuwa imeshindwa kusimamia zao hilo na kusababisha wakulima wapande mbegu zisizoota.

Kwa mujibu wa wakulima hao, Bodi ya Pamba imekuwa chanzo cha zao la pamba kuporomoka, kwani imesababisha umaskini kwa wakulima kwa kuwa wanaliuza zao hilo kwa bei ndogo.

“Tunaomba uondoke hapa, hatukutaki hata kidogo, Serikali mmetunyonya sana wakulima wa pamba, ondoka na Bodi ya Pamba na mbegu zenu ambazo hazioti,” alisikika akisema mmoja wa wakulima kwa hasira.

Kutokana na hali hiyo, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), alilazimika kuingilia kati na kuwasihi wananchi hao watulie ili wamsikilize Naibu Waziri huyo, jambo ambalo lilifanikiwa.

Akijibu maswali ya wananchi hao, Zambi alisema Serikali haina uwezo wa kuwafidia wakulima waliopata hasara kutokana na mbegu za pamba kutoota.

Hata hivyo, alisema Serikali itatoa bure mbegu za pamba kwa msimu ujao wa kilimo baada ya tathmini kufanyika.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles