30.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wataka jeshi lifanye utafiti wa corona

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

BAADHI ya wabunge wametaka jeshi lipewe fedha lifanye utafiti wa virusi vya corona, huku Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango akisema ushauri huo ni mzuri na ataupa msukumo hata kwa waziri ajae kama yeye hatorudi bungeni.

Akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge waliokuwa wakichangia bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Mpango alisema ushauri uliotolewa ni mzuri na ataufanyia kazi.

“Ushauri wa jeshi kupewa fedha kwa ajili ya kufanya utafiti na mimi ni mzuri na nipende kusema nitasisitiza mambo haya yapewe msukumo na ambaye atakuja kama mi sitakuwepo hapa  kwa baadae,” alisema Dk. Mpango.

Alisema wanajitahidi kutoa kipaumbele kwa wizara hiyo nyeti ndiyo maana hadi  Machi 2020 Jeshi la Wananchi limepatiwa asilimia 79.2  ya  bajeti yao na JKT asilimia  86.8 ya bajeti yao.

Pia alisema wizara imepatiwa asilimia 83.2 ukijumuisha asilimia  80.77 ya bajeti ya wizara.

Kuhusu suala la fidia, Dk. Mpango alisema wataendelea kutoa  kipaumbele cha juu kuhakikisha wanalipa   fidia katika maeneo ambayo yamechukuliwa na jeshi.

Alisema hadi Mei mwaka jana Serikali imetoa zaidi ya Sh bilioni 8.81 zimetolewa kulipa fidia, pia Sh bilioni 2.11 kulipa hati za madai kwa wakandarasi katika miradi ya jeshi.

“Niseme kwamba mimi na wenzangu tunaamini taasisi ile ni ndoto ya Nyerere, kwahiyo tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha hela zinafika kwa wakati,” alisema Dk. Mpango.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema kutokana na miradi mingi kutekelezwa, ni lazima jeshi lilinde kazi hiyo nzuri ambayo imefanyika.

“Kazi kubwa iliyofanyika ni lazima ilindwe kwa usalama wa nchi, lazima Jeshi lisimame vizuri, lazima tuwe na jeshi imara.

“Hata Rais ajae ana changamoto atatoka na nini, kwa sababu mkubwa huyu amemaliza tunamshukuru sana,” alisema Jafo.

Kuhusu corona, Jafo alisema Rais John Magufuli ameamua  yeye kama yeye, lakini ni lazima Watanzania wamuunge mkono ikiwa ni pamoja na wiki  ya nyungu.

“Hii vita haichagui silaha, wewe piga nyungu yako vizuri, kula matunda na kuna habari kwamba nyungu inarekebisha na mambo mengine, kijasho kikikutoka mambo yanakuwa pevu kweli kweli,” alisema Jafo.

Akichombeza, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema; “tunashukuru sana maarufu Mzee wa Nyungu, ushauri wako umepokewa, tunashukuru sana hata wasiojua kunyukiza sasa wanajua na wameelewa tofauti ya chungu na sufuria.”

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Bunge Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama, aliyewasilisha bajeti hiyo kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, akijibu hoja za wabunge alisema Serikali itatoa Sh bilioni 11.5 kwa tafiti mbalimbali ndani ya jeshi.     

HOJA ZA WABUNGE

Awali baadhi ya wabunge waliomba Serikali itoe fedha kwa jeshi ili lifanye utafiti wa virusi vya corona kama ambavyo yanafanya mataifa makubwa.

Wakichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka 2020-2021, baadhi ya wabunge walisema ni vyema Serikali ikatenga fedha na kulipa jeshi ili lifanye utafiti juu ya tatizo la ugonjwa huo.

Mbunge wa Kijitoupele, Shamsa Vuai Nahodha (CCM) ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika awamu ya nne, aliiomba Serikali itoe fedha ili jeshi lifanye utafiti wa corona kama ambavyo yanafanya mataifa makubwa.  

“Ushauri wangu tulipatie fedha jeshi kwa ajili ya kufanya utafiti wa maradhi makubwa ya binadamu pamoja na corona, kwani uzoefu  unaonyesha mataifa makubwa yanatumia majeshi yao na sisi haitakuwa dhambi tukifanya hivyo.

“Pia  lifanye utafiti maalumu kuhusiana na masuala  ya baiolojia. Kama siku za nyuma mataifa makubwa yaliwahi kutumia silaha za kikemikali, haitashangaza mataifa makubwa yakatumia baiolojia, kwahiyo jeshi letu lifanye kazi hiyo,” alisema Nahodha.

Pia alisema kazi ya kiongozi sio kuwatoa hofu bali ni kuwapa matumaini kama ambayo aliyafanya  baba wa taifa (Mwalimu Julius Kambarage Nyerere) na anachofanya sasa  Rais Magufuli.

“Ugonjwa wa corona unatupa tafakari kuhusu mambo mawili makubwa, kwanza kutafakari ukuu na uwezo wa Mwenyezi Mungu, linalomshinda binadamu kwa Mwenyezi Mungu linawezekana, nakubaliana na kauli ya Rais, tumtangulize Mungu.

“Hata hao wanasayansi tunasahau kwamba wameumbwa na Mwenyezi Mungu, Rais wetu anavyosimamia suala hili inaonyesha kwamba Waafrika wana uwezo mkubwa sana wa kufikiri na kutenda na nafikiri tunaweza.

“Ukiwa na kiongozi sahihi na anayefanya maamuzi sahihi kama anavyofanya Rais wetu, makubwa yatakuwa madogo,” alisema Nahodha.

Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige (CCM) aliiomba  Serikali  ipeleke fedha Nyumbu na Ngome ili ziweze kufanya utafiti na kuendeleza tafiti ambazo wanatakiwa kuzifanya kuhusiana na ugonjwa wa corona.

Vilevile mbunge huyo alitaka kuwe na sheria ya ulinzi ambayo itapanga kwa pamoja kiwango cha mishahara katika kampuni za ulinzi.

“Suma JKT na Suma Guard na haya ni moja ya makampuni yanayofanya kazi vizuri, mishahara imepangwa na Serikali na sekta binafsi na ipo ya aina mbili ya makampuni ya nje na ndani, kima cha chini kwa ndani ni 100,000 Suma Guard wanalipa 190,000,” alisema Maige.

Mbunge wa Viti Maalumu, Mariamu Msabaha (Chadema) alisema wakati nchi ikielekea katika uchaguzi, ni vyema Jeshi la Ulinzi nchini likalinda mipaka. 

“Wakati tukienda katika uchaguzi, niombe Serikali iangalie mipaka yetu.  Jeshi walinde kwa sababu tunaenda katika  uchaguzi,” alisema Mariamu.

Mbunge wa Lupembe, Joram Hongoli (CCM) aliiomba wizara kuongeza bajeti ya vijana wa JKT kwa mafunzo mbalimbali.  

“Bajeti  ya vijana wanaoingia JKT iangaliwe kwani kule  watapata uzalendo na mafunzo mbalimbali na ufundi  ili watumie ujuzi ambao wanaupata.

“Tuwawezeshe kwani wengi wanakosa mitaji na wakapata chochote cha kuanzia maisha ili waweze kujitegemea. Niiombe sana Serikali yangu kuwawezesha hawa vijana ili waweze kujitegemea,” alisema Hongoli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles