25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kanisa latoa mwongozo mpya wa ibada

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

KANISA la Free Pentecoste (FPTC) limetoa mwongozo kwa waumini wake kwa lengo la kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona. 

Mwongozo huo wenye vipengele 20 ni maagizo ya Askofu Mkuu wa FPCT, Stevie Mulenga, kwa makanisa na taasisi za kanisa hilo unaoelekeza Jumapili ibada iwe moja tu ama mbili kwa kanisa kubwa kwa waumini wachache. 

Akizungumza na MTANZANIA jana, Askofu Mulenga alisema waumini wameitikia, hivyo utekelezaji wa maagizo hayo umekuwa rahisi. 

“Wanatekeleza kwa sababu tumeona makanisani tulishawaambia wahakikishe kuna ndoo za maji yanayotiririka, watu wanavaa barakoa, ibada pia tumezifupisha si ndefu, harusi tulishaondoa, kama itafungwa ndoa hakuna sherehe yanatekelezwa kabisa. 

“Kuketi kwa mita moja moja tunalifanya japo lina shida shida, lakini tunalifanya, mahali pengine kwenye watu wengi tumeshaanzisha ibada mbili watu wanaweka viti mpaka nje.

“Na kwa matukio yanayotokea sasa hivi wala imekuwa si ngumu tena, hata kama mtu hakufa kwa corona, lakini kwa sababu ipo kila mtu anakubali kuvaa barakoa, kila mtu anaepusha maisha yake na imekuwa ni rahisi zaidi,” alisema Askofu Mulenga.

Mwongozo huo uliosainiwa na Katibu Mkuu wa FPCT, Mchungaji George Mwita, unaelekeza semina, makongamano na warsha zote zisitishwe zikiwemo zile za kitaifa na za kiidara. 

Aidha inaelekezwa majuma maalumu ya idara za kanisa yawe na programu moja – kuhudumu Jumapili ibadani.

“Sherehe za harusi zisizo muhimu kipindi hiki nazo zimesitishwa, maziko yawe na watu wachache na matanga katika misiba yamesitishwa kwa sasa,” inasomeka sehemu ya mwongozo huo.

Maelekezo mengine ni kuwepo kwa vitakasa mikono na sabuni za kunawia mikono milangoni makanisani na majumbani, na utaratibu wa kuketi wa mita moja.

“Salamu za kupeana mikono na kukumbatiana zimesitishwa makanisani kwa sasa, waimbaji wafuate utaratibu sahihi unaoshauriwa wa matumizi ya vipaza sauti makanisani,” ilisomeka sehemu ya mwongozo huo.

Aidha mwongozo huo unaelekeza ibada ziwe fupi za saa mbili na nusu kama mwongozo wa ibada unavyosema, Jumapili ibada iwe moja tu ama mbili kwa kanisa kubwa kwa waumini wachache.

Imeshauriwa ibada nyingine moja tu ya maombi ifanyike katikati ya juma kama Jumatano, programu nyingine nje ya ibada zinazokusanya watu wengi Jumapili na siku nyingine zisitishwe.

Vilevile ubatizo wa maji mengi ufanyike makanisani katika mazingira salama kwa wachache tu, ushiriki wa meza ya bwana uzingatie kanuni zote za kiafya kama ilivyo siku zote.

“Wanaohisi kuwa na dalili za maambukizi ya corona wanaombwa kumwona daktari, tuwe waangalifu na tafsiri potofu za kiimani kuhusu corona. Tufanyie kazi taarifa sahihi zinazotolewa na Serikali na uongozi wa FPCT kuhusu corona.

“Idara za Afya na Theolojia FPCT zielimishe waumini wa makanisa yetu kuhusu corona, tuendelee kuomba Mungu makanisani dhidi ya tatizo hili ili Mungu alinusuru taifa letu,” unasema mwongozo huo.

MAKANISA MENGINE

Hivi karibuni Kanisa Katoliki lilisema katika kupambana na corona wanaongozwa na sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali, maelekezo ya Wizara ya Afya na mengine yanayotolewa na waziri mkuu.

“Mfano kama ibada ilikuwa inachukua masaa mawili na nusu kwanini tusiifanye iwe ya saa moja, kadiri unapowaweka watu muda mfupi unapunguza hatari ya maambukizi,” alisema Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima alipozungumza na vyombo vya habari.

Kanisa hilo pia liliwashauri waumini wake kama kuna uwezekano wasogeze mbele matukio mbalimbali ikiwemo harusi hadi janga la corona liishe ili waje kufanya pamoja na sherehe.

Padri Kitima alisema kuna mazoea ya watu kuingiza shamra shamra ambayo ni hulka ya binadamu, lakini akasisitiza kuwa zinahatarisha zaidi zoezi la kuzuia maambukizi.

“Kama unadhani lazima mtoto wako apate ubatizo, kipaimara hakuna shida masharti ndiyo hayo, au nyie wachumba wawili mnasema tulishapanga kufunga ndoa mwezi wa nne, mje kanisani mtafunga mko wawii na wasimamizi kwa umbali wa mita moja moja, lakini hakuna sherehe,” alisema Padri Kitima.

Aidha alisema sakramenti zitaendelea kutolewa kwa kuzingatia maelekezo ya kitaalamu.

“Kuna sakramenti nyingine mtu amekaribia kufa huwezi kumnyima ubatizo, huwezi kumnyima kupokea sakramenti ya ndoa, lazima itatolewa, lakini unakuta ni mgonjwa na padri ameelekezwa namna ya kutoa kulingana na mazingira asiambukizwe na asiambukize wengine,” alisema Padri Kitima. 

Hata hivyo Kanisa Katoliki Jimbo Katoliki la Rulenge – Ngara mkoani Kagera, lilitangaza kusitisha ibada za misa, maadhimisho mengine yanayokusanya waumini wengi kanisani na sala za jumuiya kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Aprili 19.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, naye alitangaza kusitisha ibada zote kuanzia Aprili 26.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles