ROME, ITALIA
MTAWA wa Kanisa Katoliki ambaye ni Mtanzania kutoka Mkoani Kilimanjaro, Sista Anastasia Cristian Malisa amefariki dunia kwa virusi vya corona nchini Italia ambako alikuwa akitoa huduma ya kiroho kwa takribani miaka 26.
Habari zilizochapishwa na mtandao wa Kanisa Katoliki duniani wa vaticannews ulinukuu taarifa kutoka eneo la Rieti ambako mtawa huyo alikuwa akihudumu.
Kwa mujibu wa taarifa hizo mtawa huyo alifariki Jumamosi iliyopita baada ya kusumbuliwa kwa takribani mwezi mmoja na virusi hivyo.
Shirika alilokuwa akihudumu mtawa huyo la ‘The Poor Clares’ (Suore Clarisse Apostoliche) katika taarifa yake lilieleza kuwa Sista Annastasia ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 60, alizikwa siku ya Jumatatu wiki hii.
Sista Anastasia alikuwa akifanya kazi huko Rieti katika kituo cha kulea watu wazima cha Santa Lucia.
Wakati watu maarufu na wenye umri mkubwa wakionekana kushambuliwa na virusi vya corona nchini Italia, watu wote walichukuliwa vipimo na Sista Anastasia alibainika kuwa na maambukizi ya virusi hivyo.
Baada tu ya kupimwa hata kabla siku moja haijaisha alikuwa katika hali mbaya na hivyo kupelekwa katika hospitali ya iliyoko huko huko Rieti ya San Camillo De Lellis.
Jioni ya Machi 29, hali yake ilizidi kubadilika na kupelekwa chumba cha uangalizi wa karibu (ICU).
Ilikuwa ya vita ya mwezi mzima, yenye kuchukiza kwa maisha yake. Jumamosi iliyopita, Aprili 25, alizidiwa zaidi na kufariki dunia.
“Sista aliyekuja kutoka Afrika, asiye na makuu, mkarimu, ametimiza kikamilifu wito wake kama sista wa kiroho na aliyejitolea kwa ajili ya huduma ya watoto wadogo na wazee wetu wapendwa. Bwana, kwa wema wake, amkaribishe katika Ufalme wake wa furaha, uliohifadhiwa tu kwa wateule wake” ndivyo alivyoelezewa na watawa wenzake wa shirika la Poor Clares.
Miaka nane iliyopita, Sista Anastasia aliwasili Rieti kutoka katika jiji la Assisi nchini humo humo Italia.
Wiki hii wengi waliomfahamu wakati akiwa Assisi walikuwa wa kwanza pamoja na wale wa Rieti kuandika kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook wakielekezea kuumizwa na kifo cha Sista huyo aliyekuwa na tabasamu la ukarimu.
Wengine waliandika; tutakumbuka daima upendo wako na ushuhuda wa wito wako ulioitiwa.”
ALITOKEA MOSHI
Sista Anastasia alikwenda nchini Italia akitokea Moshi, Mkoani Kilimanjaro hapa nchini wakati huo akiwa na umri wa miaka 34.
Kama Sista wa shirika la ‘Poor Clare, mara ya kwanza alifanya kazi na watoto katika shule za chekechea na baada ya hapo katika nyumba za wazee, The Casa di Riposo Santa Lucia huko Rieti.
Pamoja na yote hayo ameishi nchini Italia kwa takribani miaka 26.
Hadi kufikia Aprili 28 kwa mujibu wa gazeti la Kanisa Katoliki, Avvenire, nchini Italia viongozi wa dini wakiwamo watawa waliofariki kwa janga la corona walikuwa ni 118.
Inaelezwa kuwa watawa wanawake wa Kanisa Katoliki wako hatarini kupata maambukizi zaidi ya corona kwa sababu wengi wao wanafanya kazi katika hospitali wengine wanahudumia wazee, na wanakutana kwa karibu na jamii.
ASKOFU NJIRU WA KENYA NAYE AFARIKI ITALIA
Wakati huo huo Askofu wa Kanisa hilo ambaye anatokea nchini Kenya, Silas Njiru naye amefariki dunia mwanzoni mwa wiki hii kwa virusi vya corona.
Askofu Njiru ni askofu wa pili katika Dayosisi ya Meru nchini Kenya.
Kwa mujibu wa mwakilishi wa wamisionari wa Consolata nchini Italia, Padri Pedro Jose da Silva Luoro, baada ya kustaafu Askofu Njiro alikuwa akiishi katika makazi ya Mbarikiwa Joseph Allamano nyumba ya wazee huko Alpignano, Turin nchini Italia.
Askofu Njiru alifariki dunia Aprili 28 mwaka huu akiwa na miaka 92.