24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Nusu ya Wafanyakazi duniani kupoteza kazi

Na MWANDISHI WETU 

KARIBU nusu ya wafanyakazi wote duniani wapo katika hatari ya karibu ya kupoteza kazi, Shirika la Kazi Duniani (ILO) limesema.

Kwa mujibu wa ILO, idadi ya wafanyakazi duniani ni karibu bilioni 3.3.

Ripoti hiyo mpya ya ILO inawasha kengele juu ya hali ya uchumi duniani wakati ambako kila taifa limeathirika kutokana na kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Katika ripoti yake hiyo mpya shirika hilo kongwe la Umoja wa Mataifa la ILO limesema, wafanyakazi wengine bilioni 1.6 walioko katika uchumi usio rasmi – karibu nusu ya nguvu kazi ya dunia, na wale walio katika hatari kubwa ya kuhitimisha mikataba yao ya ajira – wako katika hatari ya kupoteza riziki.

Ripoti hiyo ya ILO ni wazi inaigusa moja kwa moja Tanzania ambayo tayari imeonja changamoto ya wananchi wake kadhaa kupoteza ajira.

Japokuwa hakuna takwimu rasmi  zinazoonyesha kiwango cha watu waliopoteza ajira, lakini hatua ya hoteli kadhaa kubwa zikiwamo zile za kitalii kufungwa katika kipindi hiki ambacho nchi inakabiliana na maambukizi ya virusi vya corona ni wazi wengi wamepoteza ajira.

Visiwani Zanzibar asilimia karibu 100 ya hoteli za kitalii zimefungwa.

Sekta ya Utalii Zanzibar ni moja ya nguzo kuu za uchumi wa visiwa hivyo na Tanzania kwa ujumla, lakini tangu mlipuko wa virusi vya corona ulipoibuka mambo yamebadilika.

Kwa sasa sekta ya utalii inaelezwa kuyumba vibaya visiwani humo.

Waziri wa Utalii visiwani Zanzibar, alitangaza kuwaondoa watalii waliokuwa wamebaki visiwani humo katikati ya Machi mwaka huu.

Si katika upande huo tu, wapo pia baadhi ya wafanyabiashara ambao wamelazimika kufunga biashara zao, zikiwamo baa kadhaa.

Katika kipindi cha mwezi mmoja Marekani imepoteza ajira milioni 22.

Wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini China hawana kazi wakati virusi hivyo vikiendelea kutafuna ajira.

Uchumi wa Marekani umepungua kwa asilimia 4.8 katika robo ya kwanza.

“Kwa mamilioni ya wafanyakazi, kukosa kipato maana yake hakuna chakula, hakuna ulinzi na mipango ya baadae. Mamilioni ya biashara duniani zinapumua kwa shida,” anasema Mkurugenzi  Mkuu wa wa ILO, Guy Ryder.

“Hawana akiba au uwezo wa kutoa fedha. Hii ndiyo sura halisi inayoikabili  dunia kwa sasa. Kama hatutawasaidia sasa, watakufa.”

Tathmini ya sasa ya ILO kuhusu hali ya duniani kote inaonyesha kiwango cha athari za janga la virusi vya corona kwenye ajira.

Virusi vya corona vimeathiri watu zaidi ya milioni 3.1 duniani na kuua zaidi ya 226,000  na kufunga vitega uchumi vikubwa duniani.

” Inaonyesha nadhani kwa maneno magumu kabisa kuwa tatizo la ajira na athari zake zote zimeongezeka ukilinganisha na makadirio yetu ya wiki tatu zilizopita,” Ryder aliwaambia waandishi wa habari Jumatano.

Chama cha wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi vya England na Wales, vimetaka hatua za kimataifa kuchukuliwa ili kuwalinda wafanyakazi.

Mapema mwezi huu shirika la Oxfam lilichapisha utafiti likionya kuwa watu wengi watajikuta wamelazimika kuingia kwenye umaskini.

“Kwa mabilioni ya wafanyakazi katika mataifa maskini ambao tayari walikuwa kwenye hali ngumu hapo kabla, wakivuna chai au kushona nguo – hawana malipo ya matibau au msaada wa serikali.,”  alisema Danny Sriskandarajah, ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Oxfam. 

Anasema itakuwa ni ngumu kwa wengi kulisha familia zao wakati vipato vyao vitakapoondoka.

Mwezi wa kwanza wa mzozo wa virusi vya corona inakadiriwa kusababisha kushuka kwa asilimia 60 ya mapato ya  wafanyakazi walioko katika mfumo usio rasmi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles