30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Operesheni ya kusaka wahamiaji haramu itende haki

Mwandishi Wetu

SERIKALI imetangaza kuanza operesheni ya kuwakamata wahamiaji haramu katika nyumba za kulala wageni, vituo vya mabasi, stesheni za reli, mahoteli, mialo ya uvuvi.

Pia imesema itapita  maeneo yote  yenye mwingiliano wa shughuli za kibiashara kutokana na watu wengi kujificha au kufanya kazi zao za kila siku kinyume cha sheria maeneo hayo.

Uamuzi huu, umetangazwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni akiwa mkoani Kigoma baada ya  kufanya kikazo kizito cha ndani na wakuu wa vyombo vilivyopo chini ya wizara yake.

Vyombo hivyo ni  polisi, uhamiaji, Zimamoto na Uokoaji, Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na Idara ya Wakimbizi.

Tunakubaliana na uamuzi wa serikali kuja na mkakati huu, kutokana na ukweli kuwa nchi yetu ndiyo imekuwa kimbilio la wakimbizi kutoka nchi jirani.

Kama tunavyojua Mkoa wa Kigoma umekuwa ukipokea wakimbizi wengi ambao wanaingia ama kwa njia halali au njia za porini na mwisho wa siku wamekuwa vinara wakubwa wa masuala ya uhalifu.

Tunatambua namna ambavyo kumekuwapo na matukio mengi ya halifu katika mikoa ya pembezoni, wapo wakimbizi ambao wanaingia wakiwa na silaha na vitu vingine vya hatari.

Mwaka huu, nchi yetu inaelekea kufanya  uchaguzi mkuu lazima vyombo vya ulinzi na usalama  vitimie majukumu yake sasa.

Kwa kuwa vyombo hivi vimepewa dhamana ya kusimamia ulinzi na usalama ndani ya nchi, vinapaswa kushirikiana kwa kila katika msako huu ambao unatarajia kuanza.

Kama tulivyosema hapo juu, mikoa iliyopo mipakani huathirika zaidi, lakini suala la kuimarisha vizuizi  vya barabarani nchi nzima na kutatoa elimu kwa wananchi jinsi ya kuwatambua watu wasio raia ni la msingi mno.

Pia tunagetemea Serikali itafanya ukaguzi  kwenye makampuni binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kubaini watu ambao wanachomekwa kimya kimya na waajiri wao.

Tumeshtushwa mno kusikia Masauni akikiri wazi  kuwa kumekuwapo na wimbi kubwa la watu kuingia nchini bila kufuata utaratibu,tunajiuliza wimbi hili limeanza lini?

Imekuwaje kumekuwapo na mwanya mkubwa kiasi hiki hadi kusababisha watu kuingia kwa kasi ya ajabu nchi ya nchi.

Tunatambua kila mtu kwa kada yake anayetaka kuingia nchini hufuata utaratibu  zilizowekwa na Serikali kwa sababu hatujawahi kusikia Serikali raia yeyote wa kigeni anayefuata taratibu ananyimwa fursa ya kuingia nchini.

Aliwataka wananchi kutowahifadhi au kuwasafirisha watu wasio raia kwani ni kinyume na sheria na adhabu yake ni kifungo cha miaka 20 au faini ya milioni 20 au vyote kwa pamoja.

Masauni alisema katika adhabu hizo pia, chombo cha usafiri kilichohusika kuwasafirisha washtakiwa kitataifishwa na kwa mwananchi atakayekutwa akimhifadhi mhamiaji haramu, adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka mitatu na faini isiyozidi laki tano au vyote kwa pamoja.

Takwimi zinaonyesha Januari hadi Desemba, mwaka jana, walikamata wahamiaji haramu 3,992 mkoani Kigoma idadi ambayo ni kubwa

Sisi MTANZANIA, tunatoa rai kwa vyombo vya dola kuendesha msako huu bila kumuonea mtu wala kumdhulumu kitu chochote.

Tunasema haya kutokana na kumbukumbu za nyuma za operesheni zilizofanyika kama vile “Operesheni Tokomeza’ ambayo ilidaiwa kukiuka taratibu nyingi na kusababisha mawaziri kadhaa kupoteza vibarua vyao.

Moja ya malalamiko makubwa, yalikuwa wananchi kuchomewa makazi yao, kupigwa ovyo na kuporwa mali zao. Tunasema katika hili hatupendi kusikia malalamiko haya yanajirudia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles