Ramadhan Hassan – Dodoma
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imebainisha uwepo wa miradi mingi iliyo chini ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambayo imeshindwa kukamilika kwa wakati.
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kwa mwaka 2019, Mwenyekiti wa PAC, Nangejwa Kaboyoka alisema miradi mingi iliyo chini ya NHC imeshindwa kukamilika kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali.
“Kutokamilika kwa miradi hiyo kumeongeza gharama za ujenzi na kuisababishia Serikali hasara, kutopatikana kwa thamani halisi ya fedha iliyowekezwa na pia kuwepo kwa uwezekano wa NHC kushtakiwa na wakandarasi.
“Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie namna bora ya kuiwezesha NHC kukamilisha miradi ambayo ilikuwa katika hatua za mwisho za utekelezaji ili kupunguza hasara ambayo tayari imepatikana.
“Serikali iendelee na uchunguzi wa kina wa miradi yote ya NHC ili kubaini dosari zilizopo katika miradi husika. Baadhi ya miradi imebainika kuwa ilitekelezwa kwa gharama zisizo halisia na usimamizi wake haukuwa na ufanisi,” alisema Kaboyoka.
Alisema mapendekezo yao kwa Serikali ni kuziba mianya yote ya upotevu wa fedha za umma katika Serikali Kuu na mashirika ya umma.
“Kamati inaendelea kusisitiza kuwa ni muhimu taasisi za Serikali zikafanyia kazi kwa wakati hoja za ukaguzi zinazokuwa zimeibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Jambo hili lifanyike sambamba na uchukuaji wa hatua za kisheria na kinidhamu kwa wahusika wanaokuwa wamethibitika kuhusika kwa namna moja au nyingine katika ubadhirifu wa fedha za umma,” alisema Kaboyoka.
DOSARI ZA KIUTENDAJI TRA
Kuhusu hali ya ufanisi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kamati imefafanua kuhusu dosari za kiutendaji katika mamlaka hiyo na ucheleweshaji wa maamuzi ya rufaa za kodi na baraza husika.
“Dosari hizo zimesababisha kutokusanywa kwa mapato stahiki ya kodi ili kuongeza ufanisi wa makusanyo, Bunge linaazimia kwamba Serikali iziboreshe na kuziongezea uwezo Bodi ya Rufaa za Kodi na Baraza la Rufaa za Kodi kwa kuteua wenyeviti, makamu wenyeviti na wajumbe wa kutosha ili kuziwezesha taasisi hizi kufanya vikao vya kusikiliza na kuhitimisha kesi za kodi kwa wakati.
“Pia Serikali iongeze jitihada katika ukusanyaji wa kodi ambazo hazijalipwa na walipakodi.
“Jambo hili linaweza kufanikiwa kwa kuboresha na kukiongezea uwezo kitengo cha ukusanyaji wa madeni na mikakati ya kuhakikisha kodi zote zinakusanywa kwa wakati baada ya kufanyiwa makadirio au uthamini, hivyo kuzuia ulimbikizaji wa kodi,” alisema Kaboyoka.
UWEKAJI MIFUMO YA TPA
Vilevile Kaboyoka alisema kamati imebainisha changamoto ya kukamilika kwa wakati mchakato wa usimikaji mifumo muhimu ya usimamizi na uendeshaji wa shughuli za Mamlaka ya Bandari (TPA).
“Kutokamilika mwa mifumo hiyo kunaweza kutoa mianya ya upotevu wa mapato muhimu kwa taifa, hivyo Bunge linaazimia kwamba Serikali itumie Taasisi ya Umma ya Wakala Mtandao (E – Government) kusimamia na kuratibu shughuli zinazoendelea za uwekaji mifumo ya TPA.
“Jambo hili litasaidia kuweka uwajibikaji na kupunguza gharama ambazo Serikali imekwishaingia hadi sasa,” alisema Kaboyoka.
MAKUBALIANO YA MKOPO NHIF
Pia alisema taarifa ya CAG imebainisha kutokuwepo kwa makubaliano ya kimaandishi ya mkopo wa Sh bilioni 82 kati ya NHIF na Chuo Kikuu Dodoma kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, na kupungua kwa hali ya mtaji wa mfuko.
“Na kwa kuwa kutokuwepo kwa makubaliano hayo ni dosari ya kiuhasibu katika hesabu za mfuko, na pia kupungua kwa hali ya mtaji kunaathiri uwezo wa kifedha wa mfuko kutekeleza wajibu wake wa kisheria.
“Bunge linaazimia kwamba, Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF na Bodi ya Wakurugenzi ya Hospitali ya Benjamin Mkapa wafuatilie kwa karibu serikalini suala la makubaliano ya kimaandishi ya mkopo wa ujenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa ili kufunga hoja husika,” alisema Kaboyoka.
Kuhusu mtaji wa mfuko, NHIF ihakikishe kunakuwepo mwenendo mzuri wa mfuko, kwa kuongeza udhibiti na ufuatiliaji wa kiwango cha madai ya huduma ili kuepuka madai hewa ambayo yanaathiri shughuli zake.
“NHIF iendelee kufanya tafiti mbalimbali za kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kuwekeza asilimia fulani ya michango ya wanachama ili uwekezaji huo uje kusaidia malipo ya huduma za afya kwa wanachama pindi watakapostaafu,” alisema Kaboyoka.
UTENDAJI WA STAMICO
Kuhusu utendaji wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico), PAC imebainisha dosari kubwa za kiutendaji.
“Dosari hizo zimesababisha Serikali kutopata faida stahiki kama gawio na kodi kutoka kwa Stamico na kampuni zake tanzu.
“Bunge linaazimia Serikali kupitia Ofisi ya Msajili (TRO) wa Hazina iimarishe usimamizi wa karibu wa Stamico ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya shughuli za utendaji wa kila siku wa shirika hilo,” alisema Kaboyoka.
Pia, alisema Serikali ifanye mapitio ya mikataba yote ambayo Stamico ambayo imeingia na kampuni tanzu ili kuhakikisha makubaliano katika mikataba yanatekelezwa ipasavyo na masharti hasi yanaondolewa.
MIRADI INAYOTEKELEZWA TBA
Aidha, alisema kamati imebainisha hali ya kutokamilika kwa wakati kwa miradi inayotekelezwa na TBA hapa nchini.
“Kutokamilika kwa miradi hiyo kunaisababishia Serikali hasara kwa kuongeza gharama za ujenzi na kuwanyima wateja fursa za kutumia miradi husika kwa wakati mwafaka.
“Bunge linaazimia kwamba TBA waboreshe na kuimarisha kitengo cha usimamizi wa utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha miradi yote inaanza na kukamilika kwa kuzingatia muda uliokubalika kimkataba,” alisema Kaboyoka.
UWEKEZAJI NSSF HISA ZA VODACOM
Kuhusu Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), uchambuzi wake katika taarifa ya CAG ulibaini kuwa uwekezaji wa NSSF katika hisa za Vodacom haukuzingatia mwongozo wa uwekezaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
“Uwekezaji huo unatoa riba ndogo kuliko riba inayotolewa na dhamana za Serikali, hivyo kuikosesha NSSF mapato stahiki.
“Bunge linaazimia kwamba Serikali ifanye uchunguzi wa kina wa suala hili na kuchukua hatua stahiki kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi,” alisema Kaboyoka.
MIKATABA WIZARA YA ELIMU
Alisema kamati inashauri usimamizi wa mikataba ya ujenzi katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutokana na kuwa na mapungufu.
“Mapungufu hayo yamesababisha ongezeko la gharama za ujenzi na hivyo kuisababishia Serikali hasara na pia kutofikiwa kwa malengo ya wizara.
“Bunge linaazimia kwamba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iimarishe kitengo cha usimamizi wa mikataba ya ujenzi na ukarabati,” alisema Kaboyoka.