30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Kairuki atoa siku saba TIC kutembelea Ruvuma

Mwandishi wetu -Ruvuma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki, ameutaka uongozi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) kutembelea na kukagua mazingira ya wafanyabiashara na wawekezaji wazawa waliopo Mkoa wa Ruvuma ndani ya siku saba.

Agizo hilo alilitoa jana mjini Songea baada ya kutembelea na kukagua kiwanda cha kutengeneza kahawa cha Wilaya ya Mbinga cha MCCCO pamoja na DAE kwa lengo la kukagua mazingira na utendaji wa viwanda hivyo mkoani Ruvuma.

Kairuki alitoa maelekezo hayo baada ya kubaini kuwa taasisi hiyo haijawafikia wawekezaji wazawa kikamilifu, hususani waliopo mikoani ili kuwatambua na kuwaelimisha kuhusu fursa wanazotoa.

“Ninawaagiza TIC mfike katika viwanda hivi ndani ya siku saba kuanzia sasa ili kuwatembelea na kuwaeleza huduma zinazotolewa na taasisi yenu ikiwemo fursa zilizopo na endapo wataona inafaa wajisajili kwa kuwa ni suala la hiari,”  alisema Kairuki

Aidha alieleza kuwa ipo tija ya kuwatambua wawekezaji wazawa waliopo nchini kwa kuzingatia mchango wao katika uchumi wa viwanda kwa kuzingatia mwaka huu ni wa uwekezaji.

“Naelewa kuwa ipo miradi mingi iliyofikiwa na TIC zaidi ya asilimia 72, hivyo niwatake mfike haraka mkoani Ruvuma, hususan katika viwanda hivi vya kahawa ili kuvitambua na kueleza fursa na umuhimu wa kujisajili na taasisi hii ili kuendelea kuchangia na kuwa na tija zaidi katika uchumi wa nchi,” alisema.

Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa TIC, Mafutah Bunini, alisema katika kuboresha utendaji wao wamefungua ofisi za kanda saba ili kuwafikia kwa urahisi wawekezaji wa ndani na kwamba wanatoa uzito sawa kwa wawekezaji wa ndani na nje.

“Na katika hili ndiyo maana viwango vya mitaji ya uwekezaji vinatofautiana kwa wawekezaji wa nje na ndani ambapo mwekezaji wa ndani anatakiwa awe na mtaji wa dola laki moja, lakini mwekezaji wa nje ni dola 500,000,” alisema.

Meneja wa kiwanda cha kutengeneza kahawa cha MCCCO, alimuhakikishia Waziri Kairuki kwamba wataendelea kuboresha mazingira mazuri ya wafanyakazi na kuongeza thamani ya bidha zao za kahawa na kuhakikisha jamii iliyowazunguka inanufaika na kiwanda hicho.

“Tunaishukuru Wizara ya Uwekezaji kwa jitihada inazofanya za kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuondoa vikwazo mbalimbali vilivyokuwepo awali hali inayosababisha uwekezaji kukua kwa kasi,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha kutengeneza kahawa cha DAE, Danistan Komba alimpongeza waziri huyo kwa kutembelea kiwandani hapo na kueleza changamoto za masoko ya kahawa na kuiomba Serikali kuendelea kuwaangalia wawekezaji hao wazawa.

Alifafanua kuwa pamoja na changamoto za uhaba wa masoko, kiwanda kimekuwa kikishiriki maonesho ya nchi zinazolima kahawa ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Ethiopia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles