29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Wazazi wa watoto wanaougua selimundu hufikiria zaidi kurogwa

Na MWANDISHI WETU

SELIMUNDU (sickle cell) ni ugonjwa wa kurithi ambao hutokea baada ya mwili wa binadamu kuwa na upungufu katika umbile la seli, ambapo hubadilika na kuwa nusu duara au umbile la mundu (zana ya mkulima) badala ya mduara.

Hali hii ya umbile la seli kufanana na mundu, ndio iliyosababisha iitwe iitwe selimundu au kwa jina la kitaalamu sickle cell.

Ni ugonjwa unaorithishana vizazi kwa vizazi, lakini endapo mzazi mmoja tu akiwa na vinasaba vya ugonjwa huu basi huwa ni vigumu kusababisha mtoto kuvipata, bali endapo wazazi wote wawili ikitokea wana vinasaba hivyo.

Kwa Afrika, Nigeria ni nchi ya kwanza kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na selimundu huku Tanzania ikishika nafasi ya tatu, ambapo kila mwaka watoto takribani 11,000 huzaliwa na matatizo hayo.

Kutokana na kuongezeka kwa tatizo hilo, wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas) wameamua kufanya utafiti na kutafuta njia ya kuutibu ikiwa ni pamoja na kupandikiza uboho (born marrow) na vinasaba kwenye mifupa.

Kwa kawaida, chembe nyekundu ya damu ni mviringo, husafiri kupitia mishipa midogo kabisa ya damu kwa urahisi na kwa wagonjwa wenye selimundu, chembe zao za damu huvunjika na kupoteza umbo hilo la mviringo na kuchukua umbo la ndizi au mundu.

Chembe hizo nyekundu za damu zenye umbo la mundu hukwama katika mishipa midogo ya damu mwilini na mtiririko wa damu kwenda sehemu fulani ya mwili unapopungua huku hewa safi ya oksijeni ikizuiwa na kusababisha maumivu makali ya ghafla.

Kutokana na hali hiyo, husababisha maumivu makali katika mifupa na vifundo, maumivu yasiyotabirika ambayo yanaweza kutokea mara chache au mara nyingi kama kila mwezi kwa mgonjwa mwenye matatizo hayo.

Dalili

Dalili ya kwanza huanza kuonekana kwa mtoto pindi anapotimiza umri wa miezi sita tangu kuzaliwa kwake.

Huanza kuugua mara kwa mara, kuvimba miguu, kuishiwa damu pamoja na ubongo wake kushindwa kukua ipasavyo.

Hali hiyo inapotokea, mzazi anashauriwa kumpeleka hospitalini ili aweze kufanyiwa vipimo na kuanza matibabu mapema ili kupunguza ukubwa wa tatizo.

Daktari

Akizungumzia ugonjwa huo, Daktari wa Watoto kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mloganzila, Moses Karashani, anasema sasa hivi kuna ongezeko la rufaa kwa watoto wanaougua selimundu.

Anasema watoto hao ni wale wenye umri kuanzia miezi sita hadi miaka 14 ambapo kati yao nusu ni wale walio chini ya miaka minane.

Anasema mara baada ya kuonekana kwa dalili zilizopo hapo juu, mtoto anapaswa kufikishwa hospitali mapema ili aweze kupata huduma za matibabu kwa haraka.

“Mtoto ambaye wazazi wake wote wawili (baba na mama) wana vinasaba vya selimundu, kuna uwezekano wa asilimia 25 kupata ugonjwa huo na mtoto ambaye mzazi mmoja hana vinasaba hivyo hawezi kurithi,” anasema Dk. Karashani.

Anaongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, walimua kuanzisha kliniki ya watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa huo siku ya Jumanne na Alhamisi hospitalini hapo ili waweze kupata huduma bora za matibabu.

Anasema watoto waliopewa rufaa kutoka hospitali mbalimbali nchini zikiwamo za Mkoa wa Dar es Salaam, wanafikishwa hospitalini hapo kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu.

Anasema pia wamekuwa wakipokea watoto wenye ugonjwa huo kutoka majumbani, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa.

Anasema katika siku hiyo, zaidi ya watoto 20 wanafika hospitalini hapo kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu kuanzia umri wa miezi sita hadi miaka 14, ambapo kati yao, nusu yake ni wale wenye umri chini ya miaka minane, jambo ambalo linadhihirisha ukubwa wa tatizo.

Anasema licha ya jitihada mbalimbali zinazotolewa na serikali katika kuhakikisha watoto wanapata huduma bora za matibabu, hadi sasa idadi ya watoto wanaougua ugonjwa wa selimundu ni kubwa.

“Idadi ya wagonjwa wa selimundu inaongezeka siku hadi siku, juhudi za ziada zinahitajika ili kuhakikisha wanapatiwa matibabu bora,” anasema.

Anasema watoto wanaougua ugonjwa huo, baadhi yao wanapitia changamoto nyingi ikiwamo kukimbiwa na mzazi mmoja au unyanyapaa.

Anasema wazazi wengine huamua kuwapeleka kwa waganga wa kienyeji wakiamini kuwa wamerogwa, jambo ambalo si kweli.

Anasema hali hiyo imesababisha idadi kubwa ya watoto wanaofikishwa hospitalini kulelewa na mzazi mmoja.

“Kwa sababu ugonjwa huu unahusisha udumavu wa ukuaji wa ubongo na maradhi ya mara kwa mara, baadhi ya wazazi wanaamua kuwakimbia wake zao na wengine kuwapeleka kwa waganga. Hii imechangia wengi wao kuletwa hospitali wakiwa kwenye hatua mbaya,” anasema.

Anasema katika za Marekani na India, mtoto mara baada ya kuzaliwa anafanyiwa vipimo maalumu ‘screening’ ili kubaini matatizo aliyonayo, hii huwasaidia kuanza matibabu mapema pindi anapobainika kuwa na matatizo.

Dk. Karashani anasema Chuo cha Afya ya Tiba Muhimbili (Muhas) walifanya utafiti kuhusiana na vipimo hivyo maalumu ‘screening’ katika hospitali za Temeke na Mwananyamala na kufanikiwa.

“Kwa mfano, baadhi ya hospitali binafsi nchini, wanaweka ‘full package’ ya mjamzito na gharama za malipo yake ikiwamo ya kumfanyia ‘screening’ mtoto mara baada ya kuzaliwa, hali ambayo inasaidia kujua matatizo yanayomsumbua,” anasema.

Anasema vipimo hivyo ni muhimu kwa sababu vinasaidia kujua maradhi ambayo mtoto anaweza kuzaliwa nayo.

Dk. Karashani anasema ili waweze kupiga hatua zaidi ya kuwatibu watoto, Serikali inapaswa kuboresha sera zake na kuanzisha mpango maalumu wa kuwafanyia vipimo maalumu watoto hao mara baada ya kuzaliwa.

Anasema kuboreshwa kwa sera hizo kutasaidia kuwalazimisha wajawazito kulipia gharama za matibabu zikiwamo za kuwafanyia screening watoto wakiwa wachanga.

Anasema hiyo itasaidia kutambua matatizo ya mtoto kuanzia tumboni hadi anapozaliwa, jambo ambalo pia linaweza kupunguza ukubwa wa tatizo.

Anasema lakini pia serikali inapaswa kuanzisha utaratibu wa utoaji wa elimu kwa wagonjwa wa selimundu kuanzia ngazi ya mtaa ili kuhakikisha elimu ya ugonjwa huo inawafikia watu wengi zaidi.

Hii itapunguza unyanyapaa na kuondoa imani potofu na kudhani kuwa wamerogwa.

Mmoja wa wazazi aliyezungumza na gazeti hili, Amina Omary, ambaye mtoto wake wa umri wa miaka mitano anasumbuliwa na maradhi haya, anasema awali alikua hajui kama ana ugonjwa huo hivyo alimpeleka kwa mganga wa kienyeji ili kupatiwa matibabu.

“Nilipojifungua mwanangu alikuwa anaumwa mara kwa mara pamoja na kukaukiwa damu, nilidhani amerogwa, nikaanza kuhangaika kwa waganga tofauti ili kutafuta tiba, lakini hakuna chochote kilichofanyika zaidi ya mtoto kuendelea kuugua,” anasema Amina.

Anaongeza kuwa, wakati anaendelea kuhangaika kutafuta tiba ya mtoto wake, mzazi mwenzie aliamua kumkimbia hivyo akawa katika mazingira magumu huku akihangaika mwenyewe ukizingatia kuwa hana kipato cha kutosha.

Anasema mwishowe aliamua kurudi hospitali na kuanza vipimo, ndipo mtoto wake alipogundulika kusumbuliwa na selimundu, akatakiwa kuanza matibabu haraka kwa sababu alikuwa amechelewa.

“Mimi na familia yangu tulidhani mwanangu amerogwa hivyo nikaamua kwenda kwa waganga, tuliposhindwa tukarudi hospitali na kuanza vipimo ndipo alipogundulika kwamba anaumwa selimundu,” anasema.

Anasema katika kipindi chote hicho, baadhi ya ndugu, jamaa na familia walikuwa wanamnyanyapaa mtoto wake kwasababu ya maradhi yanayomsumbua.

Anaiomba serikali kutoa elimu kwa wananchi kuanzia ngazi ya vijiji ili kila mmoja aweze kuujua ugonjwa huo na dalili zake, hii itasaidia kuwafikisha watoto mapema hospitalini.

Naye Mariam Hussein ambaye mwanawe hana ugonjwa huo, anasema elimu kuhusu selimundu haijatolewa vya kutosha, ndio maana wananchi hukimbilia kwa waganga wakidhani wamerogwa.

“Mimi mwenyewe sina elimu ya kutosha kuhusu ugonjwa huo, ndio maana tunapoona mtoto anaugua mara kwa mara tunaamini karogwa,” anasema.

Anaongeza: “Ikiwa watapatiwa elimu ya kutosha, itasaidia wazazi wengi kuwahi hospitali na wanaume kushindwa kuwakimbia wake zao.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles