33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wazazi wamepoteza sifa, watoto wanafanyiwa ndivyo sivyo

Na ANNA HENGA

UKATILI dhidi ya watoto umekuwa janga linalosikitisha na kuhuzunisha. Watoto ni moja ya kundi tete lisiloweza kujitetea, hukumbana na uonevu kadha wa kadha unaotweza utu wao.

Kisheria, mtoto ni mtu ambaye hajafikisha miaka 18. Katika misingi ya haki za binadamu na sheria, mtoto anapaswa kulindwa kwa kupatiwa malezi bora yatakayomwezesha kuwa katika misingi ya utu na maisha bora. Kimataifa mtoto analindwa kupitia mikataba mikubwa miwili ya haki za watoto, ambayo ni: Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (CRC) wa mwaka 1989 na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa mwaka 1990, yote ikiwa imeridhiwa na Tanzania.

Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ilitungwa mahususi kwa lengo la kulinda haki za watoto. Mikataba hii na sheria ya mtoto inatoa wajibu kwa Serikali, wazazi, walezi na wanajamii kwa ujumla kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili na ubaguzi.

Mbali na miundo ya kisheria, mifumo mbalimbali ya kijamii inatambua haki za watoto kama moja ya kundi tegemezi linalopaswa kulindwa na kutunzwa. Katika jamii, mtoto ni malaika, yaani hajui baya wala jema na anaitegemea jamii kumfundisha mambo yote chanya na hasi. Katika baadhi ya jamii, familia isiyojaaliwa kupata watoto huonekana kuwa isiyo na bahati.

Jamii inatambua kanuni kuu nne za ulinzi wa mtoto ambazo ni kutobaguliwa, kuzingatia maslahi bora ya mtoto, haki ya kuishi, kukua na kuendelea pamoja na kuheshimu maoni ya mtoto.

Kwa kuzingatia kanuni hizo, hali ya haki za watoto imebadilika na kuwa mbaya. Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania ya mwaka 2018 inaonesha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa ulinzi na usalama wa watoto katika jamii, jambo linalosababisha kuongezeka kwa ukatili dhidi yao.

Aina za ukatili zinazowakabili watoto ni ule wa kingono (ubakaji na ulawiti), wa kimwili (vipigo na mateso) pamoja na ukatili wa kijinsia.

Vitendo vya ukatili wa kingono vinashtua na kuacha simanzi kwani vimeongezeka mno. Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania 2018 inaonesha kuwa asilimia 91 ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto kwa mwaka 2018 ni matukio ya ukatili wa kingono. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2018 jumla ya matukio 6376 ya ukatili dhidi ya watoto yaliripotiwa kutoka matukio 4,728  nwaka 2017.

Jambo la kustaajabisha na la kushtua zaidi ni kwamba matukio ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto yanaripotiwa kutekelezwa na ndugu au walezi wa karibu kwa watoto, jambo linalochangia watoto kukosa haki kwani ndugu wengi humaliza kesi hizo katika ngazi ya familia. Watoto pia wamekuwa wakijifunza tabia zisizofaa kutoka kwa watu wa karibu, marafiki shuleni na katika jamii kwani matukio ya kulawitiana na kufanyiana vitendo vya ubakaji vimeongezeka.

Hali hii inashtua na kutoa picha mbaya ya aina ya kizazi tunachokiandaa, wazazi wamekuwa na visingizo vya kutingwa na majukumu (kuwa ‘busy’) wamepoteza ukaribu na watoto na familia zao kwa ujumla. Inashangaza na kufikirisha ni vipi mtoto anaweza kufanyiwa vitendo vya ajabu kwa muda mrefu bila mzazi au mlezi kugundua. Hii inatoa picha kwamba jamii haijali aina ya maisha wanayoyaandaa kwa kizazi kijacho, jamii haina uchungu tena juu ya utu wa mtoto.

Mzazi anaweza kumruhusu mtoto kulala na mjomba bila kujali usalama wa mtoto, mjomba anakosa utu na kumlawiti mtoto baadae anazoea tabia mbaya na kuanza kufanya kwa wengine.

Tunaweza kuona ukubwa wa tatizo na jinsi linavyotishia ustawi na maslahi bora ya mtoto. Kuna maswali mengi ya kujiuliza katika hili, jukumu la ulinzi wa mtoto tumemwachia nani?

Katika jamii kuna visa mkasa vinavyoonesha baadhi ya matukio haya yanavyotokea, sababu kuu zinatajwa kuwa ni pamoja na kukosekana kwa malezi bora kwa watoto, umasikini, imani za kishirikina na sababu za kimazingira ikiwamo umbali mrefu kutoka katika makazi ya watu na huduma za kijamii hususani shule.

Ofisa Ustawi Manispaa ya Singida anasema: “Kuna kesi ya mama anafanya biashara ya pombe. Akirudi anakuja na hawara wamelewa, yule bwana akimaliza kufanya mapenzi na mama anamgeukia binti (wanalala chumba kimoja), ambaye ni mtoto wa miaka 13.

“Huwa anaenda na wanaume tofauti na wakati mwingine wanaume wanarudi mchana na kumuingilia tena mtoto. Bahati nzuri mtoto aliokolewa na maafisa ustawi na hakukutwa na maambukizi ya VVU.”

Kama baba anaweza kumlawiti au kumbaka mtoto mchanga, mama anaweza kuishi na mtoto bila kujua changamoto anazopata na jamii inaweza kuwaacha watuhumiwa hawa kuishi huru bila kutoa ushahidi mahakamani. Je, ni nani atamtetea mtoto asiye na sauti? Lakini swali la msingi zaidi ni je, tunajenga taifa la namna gani?

Katika kuhakikisha tunakabiliana na tatizo hili, ni muda sasa umefika kila mmoja kuwajibika kwa nafasi yake kukabiliana na janga hili. Wazazi, majirani, jamii, serikali na kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kujitoa kuokoa taifa la kesho.

Kila mmoja asimame kumlinda mtoto dhidi ya ukatili na kumtetea pale haki yake inapovunjwa. Watoto ni taifa la kesho hivyo, kesho bora inategemea malezi ya sasa.

Wanafasihi wanasema: “Tusipoziba ufa, tutajenga ukuta.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles