29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Mtoto wa miaka 15 kortini kwa mauaji Njombe

ELIZABETH KILINDI -NJOMBE

WATUHUMIWA wanne akiwamo mtoto David Kasila (15), wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Machi 4, mwaka huu kwa tuhuma za mauaji ya watoto mkoani Njombe.


Kasila alifikishwa kwa mara ya kwanza Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Njombe, Februari 18, mwaka huu akituhumiwa kuwaua watoto watatu ambao ni Oliver Ng’ahala (5), Goodluck Mfugale (5) na Meshack Myonga (4) ambao wote ni wakazi wa Wilaya ya Njombe.


Watuhumiwa wengine ni Mariano Malekela, Edwin Malekela, Kalistus Costa wakazi Kijiji cha Matembwe, Tarafa ya Lupembe ambao wote walifikishwa mahakamani hapo Februari 19, mwaka huu kwa tuhuma za kumuua mtoto wao Rachel Malekela (7), Februari Mosi, mwaka huu.


Mwili wa mtoto huyo ulikutwa mita 50 kutoka nyumbani kwao akiwa amechinjwa.
Hadi sasa watuhumiwa saba wamefikishwa mahakamani mkoani hapa kwa matukio ya mauaji ya watoto wanane wakiwamo watatu wa familia moja.


Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Renatha Mzinga, alisema kati ya watuhumiwa 49, baada upelelezi watuhumiwa saba wamefikishwa mahakamani kwa matukio ya mauaji.


“Hata hivyo, operesheni zetu ziliendelea hadi tulipofika mikoa mbalimbali ya Mbeya, Iringa na hata Ruvuma ambako tuliweza kuwapata watu mbalimbali.


“Pamoja na msako wetu tuliendelea kuwakamata waganga wa jadi na hasa wale wapiga ramli chonganishi ambao waliweza kuchochea chuki katika mkoa wetu,” alisema Kamanda Mzinga.


Alisema Jeshi la Polisi limewafikisha mahakamani watu saba, wakiwamo watatu kwa tukio la mauaji ya watoto watatu katika Kijiji cha Ikando na mtuhumiwa mmoja kwa mauaji ya watoto watatu mjini Njombe.


Kamanda Mzinga alisema kutokana na operesheni iliyofanyika, aliwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za yeyote atakayebainika na kuwa na dalili zozote za kujihusisha kwenye mauaji hayo.


“Tunaomba wananchi waendelee kutuletea taarifa ambazo zimechujwa na taarifa ambazo zitaweza kutusaidia, sio taarifa za fitina au za kukomoa watu wakidai kuwa wanajihusisha na matukio haya.


“Kwa mfano wananchi wanaotuletea taarifa za maandishi wakieleza kuwa kuna matumizi ya gari namba zimehifadhiwa, kuna watu walioshuhudia majina yamehifadhiwa, kuna gereji zinazotumika kuficha wahalifu jina la gereji limehifadhiwa, hapo itatuletea ugumu sisi polisi kukamilisha upelelezi wetu.


“Tunaomba taarifa za kueleweka ili kuweza kukomesha mauaji haya moja kwa moja, sio taarifa ambazo zinaeleza majina yamehifadhiwa, sisi tunazichukulia kama taarifa za majungu ambazo hazina utafiti wowote na haziwezi kutuletea mafanikio
“Pia wananchi waendelee kutuletea taarifa za waganga wa jadi hasa wale wapiga ramli chonganishi ili tuwakamate na kuwafikisha mahakamani,’’ alisema.


Aliwataka wazazi na walimu kuendelea kushirikiana kuwalea watoto, huku akiwaasa wananchi waache kuamini imani za kishirikina na badala yake wafanye shughuli halali ili waweze kuhakikisha jamii inakuwa salama.


Aidha Kamanda Mzinga aliwataka wananchi wazingatie taratibu za kisheria kutatua migogoro ya ardhi na wafuate taratibu za mirathi ili kuepuka kufanya mgawanyo wa mali kwa kutumia ubabe na visasi.


Katika hatua nyingine, Kamanda Mzinga alisema Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linaendelea na upelelezi juu ya mtoto Gaudes Kihombo (7) wa Kijiji cha Ikando aliyepotea tangu Januari 6, mwaka huu na hadi sasa hajapatikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles