RAMADHAN HASSAN, DODOMA
MAMBO yanayochangia saratani ya koo ni pamoja na kufanya mapenzi kwa kutumia mdomo, imeelezwa.
Hayo yalielezwa jana na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Ocean Road, Dk. Julius Mwaisekege mbele ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Ummy Mwalimu ambaye alikuwa akitoa tamko kuhusiana na siku ya saratani duniani .
Dk. Mwaisekege alisema miongoni mwa mambo yanayochangia saratani ya koo ni kufanya ngono kwa kutumia mdomo ambako majimaji huwa yana madhara.
Alisema kwa sasa kuna ongezeko la saratani hiyo ambayo ilikuwa ikishika nafasi ya nne lakini ipo nafasi ya tatu kwa magonjwa ya saratani.
Waziri Ummy alisema ugonjwa wa saratani bado ni tishio nchini na inakadiriwa kuwa katika kila wagonjwa 1000 mgonjwa mmoja huugua saratani .
Alisema Tanzania kunatokea wagonjwa wapya wa saratani 55,000 kwa mwaka na takribani wagonjwa 28,610 hufariki dunia kwa mwaka, vifo ambavyo ni asilimia 52 ya wagonjwa wapya.
“Takwimu za hospitali za mwaka 2018 zinaonyesha wagonjwa wapya wa saratani waliohudumiwa kuwa ni 14,028 ambao ni asilimia 25.5 ya wagonjwa wote wanaokadiriwa kuwepo nchini,” alisema Waziri Ummy.
Alisema wagonjwa waliohudumiwa walifika kupata huduma katika hospitality za Ocean Road ni wagonjwa 7649, Bugando wagonjwa 2790, KCMC 1050, Muhimbili 1321 na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya wagonjwa 218.
“Takribani wagonjwa wapya 1000 walipata huduma katika hospitali binafsi za Agakhan, Hindu Mandal, Hubert Kairuki, Besta na Rabininsia,” alisema.
Mkurugenzi wa Uhakiki ubora kutoka Wizara ya Afya, Dk. Mohamed Ally, alisema licha ya kuutaja ugojwa wa saratani kuwa unaathiri rika na jinsia zote, aliitaka jamii kushiriki kwa ukamilifu katika kupambana na janga la saratani.
Dk. Mohamed alisema jamii inatakiwa kuwa na mtazamo chanya juu ya ugojwa huo kupunguza janga la saratani na athari zake zote ikiwa ni pamoja na kujikinga na vitu vyenye kusababisha saratani.
“Jamii inatakiwa kuelewa vyanzo vya saratani ambavyo ni virusi vinavyosababisha saratani ya mlango wa kizazi, maambukizi ya bakteria na parasaiti,” alisema.