31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

DED adaiwa kumuua mkulima kwa risasi

*Alikuwa anadai ushuru wa shamba, taharuki yatawala

*Kamati ya ulinzi na usalama yajifungia, Waziri Lugola anena

ASHA BANI-DAR ES SALAM

JESHI la Polisi mkoani Singida limesema litachukua hatua za  sheria kwa ofisa mmoja mwandamizi   wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida (jina linahifadhiwa)  anayedaiwa kumuua kwa kumpiga risasi mfugaji, Peter Chambalo.

Inadaiwa tukio hilo lilitokea juzi asubuhi wakati Chambalo  akiwa kanisani katika Kijiji cha Kazikazi Kata ya Kitaraka Tarafa ya Itigi.

Kwa mujibu wa mashuhuda,  mkulima huyo alikuwa katika mgogoro wa ardhi kwenye eneo ambalo anaendeshea shughuli zake za kilimo ambako pia alikuwa akiishi. 

Inasemekana eneo hilo  linamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.

Inaelezwa kuwa ingawa  mkulima huyo aliyeuawa alikuwa akiishi na kulipa ushuru kwa halmashauri  lakini mpaka kifo kinamfika alikuwa amechelewesha kulipa ushuru wa mwezi mmoja.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, siku ya tukio, wakiwa kanisani waliona polisi wakiwa wameongozana na ofisa huyo mwandamizi  wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni,   Ofisa Maendeleo wa Wilaya ya Itigi  aliyetajwa kwa jina moja la Luhende na Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Yusuph Thomas.

Mtoa taarifa huyo lidai maofisa hao walifika katika Kanisa hilo  la Sabato wakati ibada ikiendelea ambako mkulima huyo alipigwa  risasi usoni ambayo ilifumua ubongo na kusababisha kifo chake.

Imeelezwa kuwa hadi sasa mwili wa marehemu  umehifadhiwa katika Hospitali ya St. Gaspar Itigi kwa hatua zaidi.

Awali   mkanda wa video kwenye mtandao wa jamii ulimuonyesha Kamanda  wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike akiwa katika eneo la tukio.

Kwa mujibu wa mkanda huo, Njewike alifika katika eneo la tukio kanisani hapo na kuzungumza na wananchi huku akiwahakikishia wananchi kuwa atachukua hatua kali dhidi ya mtuhumiwa akisisitiza kwamba hakuna aliye juu ya sheria.

“Na kwanza nashindwa kuelewa …(anamtaja jina) huyo alikusudia nini, alikuwa anatafuta nini hasa kwenye kipindi hiki na kwa nini aende kwenye nyumba ya ibada na  afanye mambo kama haya.

“Nilikuwa naongea kabla ya kufika katika eneo la tukio sasa  nimefika nimejionea mwenyewe wananchi na wanaumini kwa ujumla naendelea kuwapa pole.

“Katika kitendo hiki hakuna anayekubaliana nacho, kama nilivyosema pale nikiwa barabarani kwamba nitachukua hatua zinazostahili kwa sababu hakuna aliye juu ya sheria,’’ alisema

Alisema suala hilo ukiliangalia halikuwa na utashi wala busara hata kidogo kwa kuwa katika hali ya kawaida waliokuwa kanisani hawakuwa na silaha.

Baadaye MTANZANIA ilipomtafuta kwa simu Kamanda Njewike,   kupata ufafanuzi wa kina wa tukio hilo, muda wote simu yake ilikuwa ikiita.

Hata hivyo alipopigiwa zaidi alipokea msaidizi wake na kusema kuwa Kamanda alikuwa  kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Na baada ya muda iliopopigwa tena simu yake iliita muda mrefu bila kupokea na baada ya muda simu ikazima.

MTANZANIA ilipomtafuta Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, alisema anayetakiwa kuzungumzia tukio hilo ni kamanda wa polisi na si yeye.

“RPC ndiye anatakiwa kuzungumzia suala hilo kwa sababu tukio lenyewe la kifo ni murder (mauaji), sasa na wao ndiyo wanaochunguza.

“Japo mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama lakini bado siwezi kulizungumzia kwa sababu ni tukio la kifo ambacho si cha kawaida,” alisema Dk. Nchimbi.

Pia alipotafuta Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola   kupata ufafanuzi wa tukio hilo, alisema bado alikuwa anasubiri taarifa ya kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na   ikifika kwake ndiyo anaweza kuzungumzia kwa kina tukio hilo.

 Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu  i (LHRC), Anna Henga  alisema ofisa huyo hakupaswa kuchukua sheria mkononi.

Alisema  hata kama mkulima alikuwa na makosa, ofisa huyo alipaswa kufuata sheria za kushughulika naye.

“Nimesikia hilo tukio lakini niseme tu ni kosa lililofanywa na kiongozi huyo  kwa kuwa kama kiongozi hakupaswa kuchukua sheria mkononi.

“Badala yake hata kama mkulima alikuwa na makosa ofisa huyo alitakiwa kufuata sheria iliyokuwa ikistahili.

 “Viongozi tunapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa wananchi na siyo kuwa watu wa kuvunja sheria.

“Ni lazima tufanye kazi kwa kufuata misingi ya sheria iliyowekwa,’’ alisema Henga.

Mkurugenzi wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Onesmo ole Ngurumwa,  akizungumza kutoka  Addis Ababa, Ethiopia,  alisema ni jambo la hatari kwa ofisa mwandamizi kama huyo kuchukua hatua hiyo.

Alisema hukumu ya kuua inafanywa kwa mujibu wa Katiba ya nchi na rais ndiye mwenye mamlaka ya kutia saini ya mwisho kwamba  mtu auawe au la.

“Ilipofikia ni jambo la hatari sana na isitakiwe tufike huko… watu wanaweza wakawa na hasira na wakachukua nao sheria mkononi,” alisema Olengurumwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles