Na Bakari Kimwanga, Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, ameshangazwa na hatua ya kushambuliwa kwake kutokana na kile anachodaiwa kutangaza kuwania ubunge wa Bunda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Amesema alichosema katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya ni kuendelea kushirikiana na wananchi wa Bunda hata kama hatakuwa mbunge wa jimbo hilo.
Kauli hiyo aliitoa Jijini Dar es Salaam juzi, alipokuwa akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu, ambapo alisema kumekuwa na upotoshwaji wa kile alichosema na kuripotiwa na vyombo vya habari (si MTANZANIA).
“Kwanza ninawapa pole wale waliokwazika na taarifa eti za mimi kuendelea kugombea ubunge, nitakuwa ni mtu wa ajabu na hata kuulizwa kwani ni nani amenizuia kugombea ubunge?
“CCM ina utaratibu wake, mimi ndiye Mbunge wa Bunda, sasa mwaka mzima eti ninatangaza nia, hili si sawasawa hata kidogo, nimesingiziwa, nilichosema katika NEC ya CCM Bunda ni kushirikiana nao hata kama nisiwe mbunge, kwani nami ni mwana Bunda na pale ni kwetu,” alisema Wassira.
Wassira alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere na pia ameshawahi kuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na baadaye kuwa Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, chini ya uongozi wa Ali Hassan Mwinyi.
Aliteuliwa kuwa Waziri wa Maji mwaka 2006 na baadaye kuhamishiwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Waziri wa Tamisemi. Mwaka 2010 Wassira aliteuliwa kushika wadhifa alionao sasa.