26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUM – 5: Ballali aliigomea Kamati ya Bunge

Daudi Balali
Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Balali

Na Waandishi Wetu

MIEZI kadhaa kabla ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufikwa na mauti katika mazingira ya usiri na ambayo hadi sasa yanaacha maswali mengi nchini Marekani, ofisa huyo wa juu wa serikali aliitwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi.

Habari kutoka kwa ofisa mmoja wa juu wa Bunge aliyezungumza na Mtanzania Jumatano zinaeleza kwamba, Ballali aliitwa mbele ya kamati hiyo Julai 2007 kwa mahojiano baada ya kuvuja kwa taarifa za kuwapo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma katika taasisi hiyo nyeti aliyokuwa akiiongoza.

Akiwa ndani ya kamati hiyo, ofisa huyo wa Bunge alimkariri Ballali akikataa katakata madai ya namna yoyote ambayo yalikuwa yakimhusisha yeye binafsi na ubadhirifu wa fedha kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na ule uliokuwa ukigusa ujenzi wa majengo pacha ya BoT.

Mwenendo wa uchunguzi wa utata wa kifo cha marehemu Ballali ambao umekuwa ukifanywa na gazeti hili kwa miezi kadhaa sasa unaonyesha kwamba katika hatua kadhaa za mahojiano, Gavana Ballali alifikia hatua ya kutaka maelezo kuhusu mwenendo wa utendaji wa taasisi aliyokuwa akiingoza kuelekezwa kwa wakuu wake serikalini.

Vyanzo mbalimbali vya habari vilivyohojiwa vimeeleza kuwa, marehemu Ballali aliitwa kwenda Dodoma siku chache tu baada ya kukutana na waandishi wa habari ofisini kwake ambako alitoa ufafanuzi na kujibu maswali yao kuhusu tuhuma zilizokuwa zikimkabili binafsi pamoja na taasisi aliyokuwa akiiongoza ya BoT.

Habari zaidi zinamkariri Gavana Ballali wakati akiwa ndani ya kikao cha Kamati ya Bunge kukana hata ushahidi uliokuwa ukitumiwa na baadhi ya wabunge kuituhumu BoT na yeye mwenyewe kutoka kwenye mitandao intaneti kwa kuuita ni ushahidi wa uongo ambao ulikuwa na watu ambao hata majina yao yalikuwa hayajulikani.

Wakati wa mahojiano hayo, Gavana Ballali alikaririwa pia akikataa pendekezo la baadhi ya wabunge waliomhoji la kumtaka ajiuzulu wadhifa wake kwa tuhuma ambazo alizieleza kwa machanganyiko wa lugha za Kiswahili na Kingereza ‘…they have no substance’ (zisizo na mashiko).

Marehemu Ballali katika mkutano wake na waandishi wa habari pia alitolea ufafanuzi madai ya kuwepo kwa ufisadi katika mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya BoT kwa kueleza kuwa, ujenzi wake ulikuwa bado ukiendelea hivyo halikuwa jambo rahisi kutoa gharama za jumla za mradi huo na kuwataka waandishi waliokuwa wakihoji hilo kuangalia vitabu vya hesabu vya benki hiyo.

Kuhusu tuhuma za kuwepo wafanyakazi wa BoT waliokuwa wakidaiwa kuwa na hisa katika baadhi ya makampuni yaliyosajiliwa nje ya nchi, aliwataka waandishi kuwa na taarifa za uhakika kuhusu tuhuma wanazopelekewa na wakijiridhisha ndipo wampelekee kwa ajili ya kufanyia kazi.

Pia alipinga kuwa na uraia wa nchi mbili ambazo ni Tanzania na Marekani na kwamba alikuwa akitumia fursa hiyo amekuwa akipokea mishahara miwili.

Uchunguzi wa MTANZANIA mkoani Dodoma ambako marehemu Ballali aliitwa na Bunge kuhojiwa, umeonyesha kuwa Kamati ya Fedha na Uchumi ilitekeleza matakwa ya kibunge kwa kulenga kupata ukweli kutoka kwake kwa wadhfa aliokuwa nao wa Gavana wa BoT kuhusu kashfa ya EPA.

Ripoti zilizokusanywa kutoka mkoani humo zimeonyesha kuwa marehemu Ballali akiwa mbele ya Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge hakuwa tayari kueleza kwa uwazi alichokuwa akikijua kuhusu namna wizi wa fedha EPA ulivyofanyika, walioutekeleza na vigogo walioshinikiza au kushawishi maofisa wa BoT kusimamia utekelezaji wa wizi huo.

Kumbukumbu za kibunge zilizopekuliwa na MTANZANIA zimeonyesha kuwa kamati hiyo ilikuwa chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Handeni, Dk. Abdallah Kigoda na makamu wake alikuwa Hamza Mwenegoha.

Wajumbe wa kamati hiyo walio katika kumbukumbu rasmi za Bunge walikuwa, Elizabeth Batenga, Andrew Chenge, Antony Diallo, Fatma Abdulhabib Fereji, Josephine Genzabunge, Athuman Janguo, Siraju Kaboyonga (marehemu), Eustace Katagila,  Anna Maulida Komu, Clemence Lyamba, Dk. Binilith Mahenge, Monica Mbega, Hamad Rashid Mohamed, Felix Mrema, na Mossy Mussa.

Wengine walikuwa Devotha Likokola, Damas Nakei, Richard Ndassa, Omary Nibuka, Suleiman Ahmed Sadia, Martha Umbulla, Mzee Ngwali Zubeir, Sijapata Nkayamba na Charles Muguta Kajege. Mtalaamu wa kamati alikuwa Laurence Makigi na Katibu wa kamati alikuwa Michael Kadebe.

Taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa marehemu Ballali alishindwa kujibu moja kwa moja maswali ya wajumbe wa kamati na mara kadhaa kamati ilishindwa kupata kile ilichokuwa ikikitafuta kutoka kwake.

Hali hiyo ilisababisha kukwama kwa mahojiano hayo na Kamati a Bunge na hivyo ikakubaliwa kupangwa kwa wakati mwingine kwa ajili ya kufanyika kwa kazi hiyo.

Kusitishwa kwa mahojiano hayo kulitoa nafasi kwa marehemu Ballali kurejea ofisini kwake Dar es Salaam huku jukumu la kumuhoji likiwa limeachwa kwa kamati iliyokuwa imeundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza kashfa hiyo.

Kwa upande mwingine, uchunguzi wa MTANZANIA umebaini kuwa marehemu Ballali alipoitwa na kamati hiyo iliyokuwa chini ya uenyekiti wa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo, Johnson Mwanyika kwa ajili ya kwenda kuhojiwa, alikataa.

Hata hivyo, pamoja na hatua hiyo na marehemu Ballali kukataa kwenda kuhojiwa, Kamati ya Mwanyika iliendelea na uchunguzi wake na kuandaa ripoti ambayo ilikabidhiwa kwa rais Kikwete.

Ripoti hiyo haijapatwa kuwekwa wazi hadi sasa.

Uchunguzi uliombana Ballali

Wakati marehemu Ballali akikataa kuhojiwa na kamati iliyoundwa na Rais Kikwete kuchunguza kashfa ya EPA, Ripoti ya Ukaguzi wa Akaunti ya EPA uliofanywa na Kampuni ya Ernst & Young iliyoteuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya kazi hiyo ilionyesha kwamba kashfa hiyo iligunduliwa mapema na taasisi za fedha za nje zinazoendesha shughuli zake hapa nchini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya benki za kigeni zilizoko hapa nchini zilibaini mapema kuwapo kwa ufisadi mkubwa ndani ya Benki Kuu ya Tanzania ingawa kulikuwa na juhudi kubwa za kufunika kombe mwana haramu apite licha ya kufikishiwa taarifa hiyo.

Vielelezo vya uchunguzi wa kashfa ya EPA uliofanywa na Ernst & Young na kukabidhiwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali vilionyesha kuwa BoT iliandikiwa na baadhi ya benki za kigeni kufahamishwa kuwepo kwa malalamiko juu ya malipo inayofanya kupitia benki hizo kwenda kwa wateja wake.

Hata hivyo, katika hatua ya kushangaza, taarifa zinaeleza kuwa mamlaka za juu za BoT haraka haraka ziliziandikia benki hizo kuhalalisha malipo hayo.

Uhalalisho wa mamlaka za juu za BoT kuhusu malipo hayo unadaiwa kuzidi kuzitia shaka benki hizo na hasa pale zilipobaini kuwa baadhi ya wateja wake waliokuwa wakiingiziwa fedha hizo walikuwa wapya ambao hawajulikani sawasawa mwenendo wao.

Sehemu nyingine ya ripoti hiyo inaonyesha kuwepo kwa uzembe wa makusudi uliofanywa na maofisa wa BoT wanaohusika na kitengo cha wakaguzi wa benki, (Bank Supervision Unit) ambao licha ya kupata taarifa za maandishi kutoka baadhi ya benki zilizokuwa zikiingiziwa fedha za EPA zikionyesha mashaka ya wazi ya malipo hayo, walikaa kimya huku uongozi wa BoT ukiharakisha kuhalalisha malipo hayo.

Ni baada ya ripoti hiyo kubaini madudu ya kutisha yaliyokuwa yamefanywa na uongozi wa BoT katika akaunti ya EPA, ilitoa mapendekezo kadhaa yakiwemo la kufanyika kwa uchunguzi wa kina kwa kampuni zote zilizolipwa fedha hizo kama zinaendesha shughuli zake kihalali, kushughulikia makosa ya kijinai yaliyojitokeza kwa kufanya uchunguzi wa kijinai kwa kutumia chombo makini chenye uwezo wa kufanya uchunguzi mkubwa kama huo kufuatilia makosa ya kijinai yaliyofanywa, sambamba na kuchukua hatua za haraka.

Uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete, kumuondoa katika wadhifa wake marehemu Ballali unaelezwa kuchagizwa zaidi na sehemu ya mapendekezo yaliyotolewa na wakaguzi wa Kampuni ya Ernst & Young waliopendekeza hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya watendaji wote wa BoT waliohusika na mchakato mzima wa malipo fedha za EPA.

Waliotajwa moja kwa moja katika ripoti hiyo ni Ballali, Mkurugenzi wa Fedha, Katibu wa Benki wanaotajwa katika ripoti hiyo kuwa wawili katika kipindi cha 2005/2006 na Mkurugenzi wa Sera za Uchumi (DEP) ambao nao wanatajwa kuwa wawili katika kipindi hicho.

Maofisa wengine waliotajwa na ripoti hiyo sambamba na marehemu Ballali ni aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Idara ya Mikopo (DDDD) ambao nao wanatajwa kuwa wawili, Mkuu wa kitengo cha mikopo mikubwa na ya kibiashara, Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mabenki aliyekuwapo kipindi cha 2005/2006 na Wakurugenzi wa bodi waliokuwapo kati ya Septemba na Oktoba 2006.

Usikose kufuatilia kesho ambapo tutaona jinsi Ballali alivyoondoka Dodoma na baadae kuelekea nje ya nchi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles