22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kagame ampinga Membe, UN

Bernard Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe

NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya Rwanda imepingana na shinikizo la Umoja wa Mataifa la kutaka nchi hiyo kumaliza tofauti na kuwapokea waasi wa kundi la Democratic Forces for Liberation of Rwanda (FDLR).

Juzi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, alisema waasi hao wameuandikia barua Umoja wa Mataifa (UN) wakiomba amani na kwamba wako tayari kuweka silaha chini ili kuacha mapigano yaliyokuwa yakiendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Membe alisema baada ya UN kupokea barua hiyo, ilizishirikisha Jumuiya za Kimataifa na kwa pamoja walikubaliana kumalizwa kwa tofauti kati ya serikali ya Rwanda na waasi hao na kwamba ni muda wa Serikali ya Rais Kagame kuwapokea waasi hao na baadhi yao wajumuishwe kwenye vikosi vya majeshi ya nchi hiyo.

Alisema Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa na mkutano wa kujadili namna kundi hilo litakavyoweka silaha chini na kurejea uraiani kama walivyo raia wengine na kwamba watatengewa makambi maalumu na kufanyiwa mahojiano ili kubaini chimbuko la makazi yao ili kurejeshwa makwao.

Akijibu uamuzi huo wa UN, Waziri wa Ulinzi wa Rwanda, Jenerali James Kabarebe, alisema kamwe hawatatoa nafasi ya kukaa chini na wala kukubali shinikizo la Umoja wa Mataifa pamoja na nchi wanachama wa Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu na Wanyarwanda wanaoishi nchi hizo ambao wanakiunga mkono kikundi cha waasi cha FDLR, kwa kuwa kinahatarisha usalama wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mtandao Chimpreport uliopo nchini Uganda, Kabarebe alisema zaidi ya siku mbili kumekuwa na ajenda ya siri iliyopo kwa maofisa wa UN na baadhi ya nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kukiunga mkono kikundi cha FDLR.

“Rwanda haitasita kuchukua hatua dhidi ya Azimio lolote litakalotolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuungana na wauaji au vikwazo vyovyote,” alisema.

Aliongeza kuwa mgogoro wa DRC umekuwa ni fursa kwa kundi la FDLR kufanya biashara na mataifa mbalimbali, taasisi na watu binafsi.

Alisema pia kuna uwezekano mkubwa kwa mataifa ya magharibi kuchochea mgogoro wa Mashariki mwa Kongo ili kuchota malighafi na kulinda biashara zao zisiingiliwe na kuwanufaisha wanaolinda amani nchini humo.

Kabarebe aliyasema hayo juzi, wakati akizungumza kwenye Chuo cha Taifa cha Polisi (NPC) na kuongeza kuwa kuna watu wanatumia kivuli cha kulinda amani na usalama ili kupora mali za DRC.

Kwa upande wake, Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje ya Rwanda, Louise Mushikiwabo, alisema: “Sera ya Rwanda dhidi ya FDLR haijabadilika, wasalimishe silaha zote na kuacha fikra za mauaji ya kimbari kisha warudi nyumbani kuijenga Rwanda kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa.

“Watu binafsi au nchi ambazo zinawasaidia watuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 bado wapo hadi leo. Ni aibu kubwa kwao,” alisema.

Aidha, taarifa zinaonesha kuwa tangu mapigano baina ya majeshi ya Rwanda na DRC ya Juni 11 mwaka 2012 kwenye mipaka ya nchi hizo, Serikali ya Rwanda imeongeza wanajeshi wake na kuwaweka tayari kwa lolote.

Maofisa wa Serikali ya Rwanda wanaamini kuwa kikundi cha waasi chenye makazi yake nchini DRC cha FDLR kimeungana na PS-Imberakuri na Chama cha Rwanda National Congress (RNC) hivyo muungano huo unahatarisha usalama wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Maofisa hao walisema kundi la FDLR ndilo lilihusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda na mashambulizi mengine yanayoendelea nchini DRC, ambapo kikundi hicho kilifukuzwa Rwanda mwaka 2010.

Duru za habari ndani ya Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa wakati majeshi ya Rwanda yakizidi kuimarisha operesheni mbalimbali, FDLR imekusanya vijana wanaokadiriwa kufikia 1,500 na kuwaunganisha kwenye kundi hilo.

Hata hivyo, taarifa ya juzi ya Membe iliwatahadharisha waasi hao kuwa endapo watashindwa kutekeleza maazimio hayo, majeshi ya UN yatahakikisha yanaanzisha mapigano yatakayowasambaratisha ndani ya muda mfupi.

Membe alisema UN imetaka mapendekezo hayo yatekelezwe ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi huu na kwamba harakati za kumshawishi Rais Kagame kukubali uamuzi huo zinaendelea.

Mapendekezo ya UN yametafsiriwa kuwa ni mtego kwa Serikali ya Kagame, ambaye amekuwa hataki kupokea ushauri wa kufanya mazungumzo na waasi, ingawa kumekuwa na mashinikizo mbalimbali ya kumtaka kumaliza uhasama na waasi hao na kwamba hatua ya waziri wake wa ulinzi kukataa azimio hilo ni mwendelezo wa nchi hiyo kutokuwa tayari kukaa meza moja na waasi hao.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Kwa kuzingatia historia ya Rwanda kabla na baada ya Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994, Serikali ya Kagame inamsingi wa kusita kukaa pamoja na Waasi. Hata hivyo, kwa upande mwingine na kama ambavyo ilikwishafanya katika kuwashughulikia wahusika wa mauaji hayo kupitia Mahakama za Kienyeji “Gachaha” uko umuhimu wa kuendeleza jitihada hizo za maridhiano. Kwani bila maridhiano hayo, ni dhahiri kwamba hali ya uhasama itaendelea ambayo ni hatari kwa hali ya Usalama si nchini Rwanda pekee bali pia katika nchi za Maziwa Makuu.

  2. Kianzio ni FDLR kusalimisha silaha na kuomba kupatiwa hadhi ya wakimbizi huko DRC. Ni kuwa na hadhi ya wakimbizi badala ya hadhi ya waasi kutakakotoa fursa ya mazungumzo ya kuleta amani kuweza kuwepo baina ya serikali ya Rwanda na FDLR na kupelekea FDLR kuweza kurudi nyumbani kuishi kwa amani. Ushauri kwamba wliokuwa waasi wajumuishwe kwenye jeshi la Rwanda ni usiokubalika hata kidogo kwa sababu waliokuwa waasi ni wasiohitajika kabisa ndani ya jeshi la Rwanda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles