27.6 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mhandisi Kivuko cha MV Nyerere akamatwa

Waandishi Wetu


MHANDISI Mkuu wa Kivuko cha MV Nyerere, Alphonce Charahani, ambaye aliokolewa saa 42 tangu kupinduka kwa kivuko hicho, amewekwa chini ya ulinzi kutokana na agizo la Rais Dk. John Magufuli, aliyetaka waliohusika kusababisha uzembe mpaka ajali hiyo ikatokea wakamatwe.

Taarifa kutoka polisi zimeeleza kuwa, pamoja ya kuwa Charahani yupo hospitali akiendelea na matibabu, lakini  amekamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi.

Wengine waliokamatwa ni ofisa mmoja wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini ( SUMATRA) ofisi ya Wilaya ya Ukerewe, msimamizi wa bandari ya Bwisya na Bugorola ikiwa ni pamoja na Nahodha Msaidizi wa Kivuko hicho, Francis Magayane.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna, aligoma kuzungumzia ukamatwaji wa watu hao na kueleza swala hilo linashughulikiwa na ngazi ya juu.

“Mimi kazi yangu kukamata wangekuwa wale wahalifu, hili mnajua ni la kitaifa wapo wakulisemea,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, alipoulizwa alisema msemaji wa mambo haya ni Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe.

Hata hivyo Kamwelwe alipoulizwa alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa vyombo vingine zaidi ya TBC.

Naye Waziri Mkuu, Kassim Majali, alisema baada ya Rais Magufuli kuvunja Bodi ya Sumatra na TEMESA, naye amemsimamisha Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dk. Musa Mgwatu, kupisha uchunguzi.

Dk. Mgwatu amesimamishwa kwa ajili ya kuhojiwa akiwa msimamizi mkuu wa TEMESA ambao ndiyo wasimamizi na wamiliki wa kivuko hicho.

Rais aagiza zabuni

Akizungumza na waananchi wa Ukara, Majaliwa alisema Rais Dk John Magufuli amemuagiza na kumuelekeza Waziri Kamwelwe, kutangaza zabuni ya ujenzi wa kivuko kipya cha kutoa huduma kati ya Bugorola na Bwisya Kisiwani Ukara wilayani Ukerewe Mkoa wa Mwanza.

Alisema Rais ameagiza kivuko hicho kipya kiwe kikubwa kuliko cha awali kutokana na eneo hilo kuwa na watu wengi.

Alisema uamuzi huo unalenga kurejesha huduma ya usafiri kwa wananchi wa visiwa vya Ukara na Ukerewe.

“Waziri anza kutekeleza agizo hili kuanzia kesho, Rais anataka utangaze zabuni ya kivuko kipya kitakachokuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200 na tani 50 za mizigo. Hiki kitakuwa kikubwa mara mbili ya Kivuko cha MV Nyerere,” alisitiza.

Atangaza Tume ya uchunguzi:

Majaliwa pia alitangaza tume maalum ya uchunguzi itakayochunguza chanzo cha ajali ya MV Nyerere.

Alisema tume hiyo itakuwa na wajumbe saba ambapo mwenyekiti wake ni Meja Jenerali Mstaafu George Waitara ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.

Alitaja wajumbe wengine kuwa ni Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi, Mhandisi Marcelina Magesa, Wakili Julius Kalolo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Queen Mlozi.

Wengine ni SACP Camillus Wambura na Mkurugenzi wa Idara ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashiru Taratibu Hussein.

Fedha za rambirambi:

Akizungumzia fedha za rambirambi zinazochangishwa na wananchi, alisema taarifa aliyopewa na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, zimefikia Sh milioni 310 na kusisitiza fedha hizo zitatolewa kwa wafiwa wote.

Alisema licha ya Sh 500,000 wanazopewa mara baada ya zoezi lote kukamilika, kiasi kidogo cha fedha kitatolewa kwa ajili ya kujenga mnara na uzio wa makaburi lakini kiasi kingine kitatolewa kwa wafiwa.

Vifaa vya uopoaji vyaletwa:

Awali Waziri Kamwele alimweleza Majaliwa kuwa, Wizara ya Madini imeongea na uongozi wa Kampuni ya Barrick inayomiliki mgodi wa Dhahabu wa North Mara ili kupata kutoa winchi ya kunyanyulia yenye uzito wa tani 90 ambayo itatumika kunyanyua kivuko hicho kutoka ziwani.

“Kuna Maputo ( Airbags) saba ya kujazwa upepo za uzito wa tani 18 kila moja, lakini tayari tumeshauriwa kununua tanki za maji kubwa zenye uwezo wa kuhimili tani 130 ili pamoja na winchi hiyo vitasaidia kazi kuwa rahisi na nyepesi wakati wa kukitoa kivuko,” alisema.

Mkuu wa Majeshi akabidhiwa jukumu:

Katika hatua nyingine Majaliwa alimkabidhi Mkuu wa Majeshi (CDF), Meja Generali Venance Mabeho, kusimamia zoezi la kukitoa kivuko hicho kwenye maji.

“CDF naomba usimamie jukumu hili la kuhakikisha zoezi linachukua siku chache na kuacha vikao vya kimkakati, ambavyo vinachelewesha shughuli hii kukamilika haraka,” alisema.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) Mhandisi Dk. John Ndunguru na kuivunja bodi hiyo kuanzia jana.

Taarifa iliyotolewa jana na Ikulu ilisema  Rais Magufuli amechukua hatua hiyo kufuatia ajali ya kupinduka kwa Kivuko cha MV Nyerere iliyotokea tarehe 20 Septemba, 2018 na matukio mbalimbali ya ajali za barabarani hapa nchini yanayosababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa mali za watu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles