LAGOS, Nigeria
CHAMA Cha Wanawake wanaofanya biashara ya kujiuza nchini Nigeria, kimetishia kuitisha mgomo kwa kile ambacho kinadai kuwa wanachama wake wamekuwa wakilazimishwa kufanya ngono na polisi baada ya kuwakamata na kuwatishia kuwafungulia mashtaka.
Chama hicho kilisema juzi kuwa asilimia 50 ya wanachama wake wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo na polisi katika mji wa Anambra katika Jimbo la Orumba Kusini.
Mmoja wa wanawake ambaye alijitaja kwa jina moja la Kaamsi, ambaye pia ni mmoja wa viongozi wa chama cha Orumba South LGA, alisema polisi wamekuwa wakiwafuata katika maeneo yao na kuwabughudhi kabla ya kuwalazimisha kulala nao.
“Polisi hawa wameshawalazimisha asilimia 50 ya wanachama wetu, wamekuwa wakija katika maeneo yetu na kutumbua kila siku.” alisema kiongozi huyo.
“Karibu siku mbili zilizopita hapa hakuna wanachama chini ya 10 kwa sababu walikamatwa na kupelekwa kwenye ofisi za polisi. Walikuwa wakitendewa vibaya…. kabla ya kuruhusiwa walilazimishwa kulipa dhamana kwa kutumia miili yao,”aliongeza kiongozi huyo.
Alisema matukio hayo yamekuwa yakitokea kila siku katika maeneo ya Umunze, Onitsha, Awka, Nnewi, Ekwulobia na kwamba wamekubaliana hakuna mwanachama yeyote atakayempa huduma polisi katika eneo hilo la Umunze na mengine katika jimbo hilo.
Alipohojiwa kama askari hao wamekuwa wakivaa sare za kazi, Kamsi alisema wanawatambua kwa vile wanamfahamu kila mteja wao na siyo lazima wawe na sare ndiyo wawatambue.