Hadija Omary, Lindi
Serikali imesema imefanya marekebisho ya ramani ya mwaka 2007 ya Wilaya ya Liwale ili kumaliza mgogoro wa ardhi uliopo katika Kijiji cha Mirui na Nanjilinji A kilichopo wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara aliyoifanya katika vijiji hivyo ambapo pamoja na mambo mengine amesema ramani itakayotumika katika kuonyesha mipaka ya vijiji hivyo ni ya mwaka 1947.
“Ramani hiyo ni ile inayoonyesha mpaka unaanzia Mlima wa Nandanga kuelekea Mlima wa Nakman na kwenda kukutana na Mto Mbwenkuru na Mto Kipelele inapoanzia Wilaya za Kilwa na Liwale.
“Hii inatokana na timu ya wataalam kubaini kuwapo na muingiliano wa mipaka baina ya vijiji hivyo viwili,” amesema Lukuvi.
Aidha, amemsema nyaraka zilizotumika katika uanzishwaji wa wilaya hizo kwa kutumia GN91 ya tarehe 16/05/1947 inaonyesha Wilaya ya Liwale inapakana na Wilaya ya Nachingwea kabla ya Novemba 13, mwaka 1980 kuigawa Wilaya hiyo ya Nachingwea na kupata Wilaya ya Liwale ambapo ugawaji wa Wilaya hiyo haukuathiri mipaka ya awali ya Nachingwea na Kilwa.