29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

SHIDA YA UMEME KUSINI IMEKWISHA-MAJALIWA

Na MWANDISHI WETU-LINDI


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema shida ya umeme iliyokuwa inaikabili mikoa ya Lindi na Mtwara sasa imekwisha.

Kauli hiyo aliitoa juzi wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Mtwara kwenye viwanja vya bandarini mjini humo.

“Kuunganishwa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye gridi ya taifa, kumeondoa tatizo la umeme lililokuwa likiikabili mikoa hii na mitambo ya jenerata iliyokuwepo itabakia kuwa ya akiba endapo dharura yoyote itatokea,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Alisema pengo lililokuwepo la kukatikakatika kwa umeme limezibwa kwa kupata umeme kutoka Somanga hadi Lindi.

“Umeme huu umeanzia kituo chetu cha Mbagala, umekuja Mkuranga, Muhoro, Lindi na hatimaye umefika pale Mahumbika. Na mchana wakati nikiwa Mahumbika, niliwasha kwa kompyuta kuashiria umeme wa gridi kuingia mikoa yetu ya Lindi na Mtwara,” alisema.

Akiwa Mtwara Mjini, Waziri Mkuu alikagua na kisha kuzindua mradi wa upanuzi wa kituo cha kufua umeme wa gesi asilia wenye uwezo wa kuzalisha megawati nne.

Kabla ya kuzindua mradi huo, alipita bandarini kukagua ukarabati wa mitambo ya kupokelea mafuta ya dizeli na petroli ambako alielezwa kuwa kampuni mbili za GM na Oil Com zimeanza ukarabati na kwamba mwezi ujao, bandari hiyo itaanza kupokea meli za kubeba mafuta.

“Bandari ya Mtwara hivi sasa itaanza kupokea meli kubwa za mafuta, jambo ambalo halijafanyika tangu mwaka 2014. Mwezi ujao, wakati wowote, wataanza kupakua mafuta. Kwa hiyo mji utaanza kuchangamka.

“Kuanza kupakuliwa kwa mafuta katika bandari hii kutasaidia kushusha bei ya mafuta kwenye mikoa hii na pia kiasi kitakachobakia tutakipeleka nchi za jirani za Msumbiji na Malawi,” alisema.

Alisema matengenezo hayo yakikamilika yatafanya Bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga ziwe na uwezo wa kupokea mafuta.

Pia aliitaka Mamlaka ya Bandari (TPA) iondoe urasimu na Mkurugenzi Mkuu wake awatumie vizuri watendaji walio chini yake.

Mapema walipopewa nafasi ya kusalimia wananchi, wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), walitumia fursa hiyo kuelezea kufurahishwa kwao na hatua za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungara alisema aliamua kutoka CCM kwa sababu aliamini kwamba mtu hawezi kusukuma gari akiwa ndani, ni lazima atoke.

“Tumetoka ndani ya gari na sasa tunalisukuma na linakwenda kwa kasi. Hebu angalia, ndani ya miaka miwili tu mambo yanavyokwenda kwa kasi. Kama tungebakia ndani gari lingeenda?” alihoji.

Naye Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka (CUF), aliwataka wananchi wa mikoa ya kusini wachangamkie fursa zinazopatikana kutokana na maendeleo yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.

“Kusini hivi sasa imeamka na imetoka gizani, sasa wananchi tuchangamkie fursa,” alisema.

Mbunge wa Nachingwea, Hassan Masala (CCM), alitumia fursa hiyo kuomba barabara ya kutoka Nachingwea iwekewe lami ili wakazi wake waweze kutumia fursa ya kusafirisha Korosho hadi kwenye Bandari ya Mtwara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles