30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

AIBU MAWAZIRI KUSHINDWA KUWAJIBIKA

RAIS Dk. John Magufuli, ameonyesha wazi kuanza kukerwa na utendaji kazi wa mawaziri ambao inaonekana dhahiri wanashindwa kwendana na kasi yake.

Tangu alipoingia madarakani mwaka 2015, Dk. Magufuli alitangaza hadharani kuwa ataunda baraza dogo la mawaziri ambao ni wachapakazi.

Kwa hali hiyo, tumeshuhudia baadhi ya mawaziri wakiondolewa kwenye nafasi zao kutokana na sababu mbalimbali.

Juzi, Dk. Magufuli akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga, aliwataja mawaziri wanne ambao inaonekana wameshindwa kwenda na kasi yake.

Mawaziri hao ni wa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Dk. Magufuli alisema anakerwa na mawaziri hao kutokana na kushindwa kusimamia majukumu yao, licha ya kupewa maagizo kwa nyakati tofauti.

Kwa mfano, Dk. Magufuli alimweleza Waziri Mwijage kuwa anamkera kwa sababu amempa maelekezo sahihi kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri, walikutana ofisini kwake akamsisitiza na wakiwa kwenye ziara za kikazi, lakini utekelezaji wake umekuwa duni.

Taarifa kwamba Waziri Mwijage na wale wote waliotajwa wanaonekana kushindwa kuchukua uamuzi na badala yake kila jambo hadi wasukumwe ili hali wana sheria zinazowapa nguvu ni za kushangaza.

Bila kificho, Waziri Mwijage anaelezwa kuwa ameshindwa kuchukua hatua za kufungia viwanda ambavyo vimeshindwa kuendelezwa nchi nzima. Sasa hili nalo hadi akumbushwe wakati tayari amepewa maelekezo ya kutosha na bosi wake?

Kwa kifupi tunaona kuna tatizo la msingi kwa wateule hawa, haiwezekani kila kitu kifanywe na rais wakati wao wapo. Iweje waonekane kwenye shughuli nyingine, lakini kwenye kuchukua uamuzi wanakuwa wazito?

Takwimu zinazonyesha Tanzania ina viwanda 197, vilivyobinafsishwa lakini vimelala, havifanyi kazi. Kwa Mkoa wa Tanga kulikuwa na viwanda 100, lakini 12 havifanyi kazi, sasa hili nalo waziri hadi asukumwe?

Rais alisema wawekezaji wengine walionunua viwanda hivyo, walihamisha mitambo na kupeleka nchi jirani na kuacha magofu nchini.

Lakini pia udhaifu wa kutekeleza majukumu umeonekana kwa Waziri Tizeba. Tunatambua Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni muhimu kwa sababu inagusa maisha ya kila mtu, awe mkulima, mfugaji, mmiliki wa kiwanda cha maziwa na mambo mengine.

Waziri Mbarawa pamoja na kuchapa kazi kwenye mambo ya barabara, naye ameguswa.

Jambo linalotakiwa hapa ni kujitafakari kwa wateule hawa kama kweli wanatimiza wajibu wao ipasavyo kwa mkuu wao wa kazi na kwa Watanzania kwa ujumla. Hawajachelewa, warudi kwenye mstari.

Sisi MTANZANIA, tunawasihi mawaziri wote walioguswa na kauli ya Rais Magufuli wajitafakari vizuri ili warudi kwenye mstari wao wa utendaji kazi wa kila siku.

Tunasema hivyo kwa sababu si kila kitu hadi kifanywe na rais, ndiyo maana ameteua mawaziri ili wamsaidie kutatua changamoto zilizopo.

Inatia aibu kuona mawaziri wanalalamikiwa na bosi wao, tena kwenye mikutano ya hadhara mbele ya wananchi, licha ya kupewa maelekezo ya ndani tena kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri.

Tunamalizia kwa kusema, inatia shaka kila mawaziri kukumbushwa na rais kutimiza wajibu wao. Tuaamini kila mmoja ana wajibu wa kutimiza majukumu yake ya kila siku katika kuipeleka mbele Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles