26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MABANGO YA MSHAHARA MDOGO YAMCHEFUA JPM

 

NA OSCAR ASSENGA – TANGA

 

RAIS Dk. John Magufuli amewatolea uvivu wananchi wanaotembea na mabango

yakielezea mishahara midogo wanayolipwa katika maeneo yao ya kazi, kwa kuwataka waache kazi, waende kulima kama wanaona haiwatoshi.

Kiongozi huyo aliitoa kauli hiyo juzi, alipokuwa akizungumza na

wakazi wa Kata ya Pongwe, wakati akielekea

mkoani Tanga kwa ajili ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania, utakaofanyika  leo, Kata ya Chongoleani.

 

Akiwa katika eneo hilo, Rais Magufuli aliona moja kati ya mabango lenye maandishi ya malalamiko ya mshahara mdogo,

ndipo alipoonyesha kukerwa na kitendo hicho.

 

“Ndugu zangu niwaambie, mimi si mpole kiasi hicho kama mnavyofikiria, nasema kama mnaona mshahara ni mdogo acheni kazi nendeni

mkalime,” alisema Rais Magufuli.

Haikujulikana mara moja sekta waliyotoka watu hao, waliokuwa wamebeba mabango.

 

Wakati Rais Magufuli akisema hayo dhidi ya watu hao, kima cha chini ambacho wafanyakazi wengi wa umma wanakilalamikia ni takribani Sh 300,000 kwa mwezi, huku baadhi ya sekta binafsi zikilipa chini ya hapo.

 

Tangu mwaka 2014, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), limekuwa likipendekeza mshahara wa kima cha chini uwe Sh 720,000.

 

TUCTA kupitia kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Nicolas Mgaya, ilikuja na pendekezo hilo

kwa kile ambacho alidai wakati huo kuwa pendekezo lao la awali la kutaka kima cha chini kiwe Sh 315,000 hakutekelezwa na serikali.

 

Alisisitiza kiasi hicho kwa wakati huo kilikuwa kimepitwa na wakati, kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

 

Tangu mwaka huu mpya wa fedha uanze ni Serikali ya Zanzibar tu ndiyo iliyotangaza kuongeza mshahara wa kima cha chini kutoka Sh 150,000 hadi kufikia Sh 300,000 kwa mwezi.

 

Mbali na hilo la mishahara, wakati huo huo, Rais Magufuli ametoa neema kwa wakazi wa Kata ya Pongwe, Jijini Tanga, baada ya kumwagiza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella,

kukata eneo la shamba la katani la Amboni kwa ajili ya ujenzi wa

stendi za daladala katika kata hiyo.

 

Huku akimtahadharisha Mkuu huyo wa Mkoa kuwa agizo hilo si nguvu za soda, alisema atafuatilia ili utekelezaji wake uanze mara moja, lengo likiwa

kuwaondolea kero wananchi hao.

 

Agizo hilo lilitokana na kauli ya Diwani wa Kata hiyo, Mbaraka

Sadi, kwa Rais Magufuli kuwa wananchi na wafanyabiashara wa

daladala hawana sehemu ya kupakia na kushushia abiria, jambo linalowalazimu kutoa huduma hiyo barabarani, ambapo kunaweza kusababisha ajali.

 

Sadi alipata fursa ya kuzungumzia kero katika kata yake baada msafara wa Rais kusimamishwa na wananchi waliokuwa wakimsubiri barabarani.

 

Alisema katika kata hiyo kumekuwa na ongezeko kubwa la

daladala ambazo hazina kituo maalumu, hali inayowalazimu kuegesha magari hayo barabarani na kusababisha vurugu na ajali zisizo na ulazima.

 

“Mheshimiwa Rais, Kata yangu ya Pongwe inakua kwa kasi sana, lakini cha kushangaza pamoja na ukuaji wote huu hatuna hata stendi ya daladala, zote zinapaki barabarani, hii inasababisha ajali,

nakuomba mheshimiwa kuna eneo la shamba tunaomba tupatiwe kwa ajili

ya stendi,” alisema Sadi.

 

Awali kabla hajalitoa shamba hilo, Rais Magufuli alimuuliza Mkuu huyo wa Mkoa juu ya anayemiliki shamba hilo la katani lililopo pembezoni mwa barabara na  kisha kuagiza limegwe kwa ajili ya shughuli hiyo ya stendi

ya daladala.

 

“RC, DED, mpo hapa, sasa nisikilizeni baada kumaliza ziara yangu muanze

ujenzi wa stendi hiyo na nitaifuatilia kwa makini zaidi juu ya utekelezaji wake, haiwezekani kunakuwepo na eneo la shamba wala haliendelezwi, halafu wananchi wana shida na eneo hilo, mjenge stendi hiyo haraka,” alisema Magufuli.

 

Alisema haiwezekani wananchi wana shida ya eneo kwa ajili ya shughuli za kijamii, lakini yupo mtu mmoja anashikilia eneo ambalo haliendelezi na kwamba

katika serikali ya awamu ya tano watu wa namna hiyo hawana nafasi.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella, aliahidi

kuyafanyia kazi maagizo hayo ya Rais Magufuli, ili

kuondoa kero hiyo kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles